RUSHWA KWENYE MUZIKI

RUSHWA ni mdudu anayesumbua sana jamii ya Tanzania. Kwa mtazamo wangu, rushwa inakuwa ngumu kupiga vita zikiwemo sababu kadha wa kadha, kwa mfano, kuna watu ambao kwao rushwa wala si kosa bali ni taratibu za kawaida za maisha, mtu ambaye alimuona baba yake maisha yake yote tangu mtoto, akitoa rushwa na mambo yakawa yanaenda vizuri sana, pengine hata vyeti vyake vya shule na hata kazi anayofanya ilitokana na baba yake kutoa rushwa na yeye analijua hilo, na amefanikiwa, mtu kama huyu rushwa ndio utaratibu bora wa maisha yenye mafanikio, kamwe hataipiga vita. Kuna wengine ambao si wala rushwa lakini rafiki zao na ndugu zao ni wala rushwa, na wanaishi vizuri kutokana na mapato ya rushwa kamwe hawawezi kupiga vita rushwa. Kuna wale ambao ni wengi, ambao wakijaribu kutoa taarifa kuhusu rushwa maisha yao yatakuwa magumu, kwa mfano, mtu huyu akienda kulipa kodi kwa njia ya rushwa analipa robo ya bei ambayo angelipa kama angelipa kihalali, huyu kamwe hatapiga vita rushwa. Kuna wale ambao wanaogopa kuwa wakitoa taarifa kuhusu rushwa jamii itawaona kuwa ni wambeya wanaoingilia yasiyowahusu. Na kuna wanaohofu kuwa wakitoa taarifa kuhusu rushwa watajifungia milango yao ya maendeleo kwani wanajikuta shughuli zao zimezungukwa na mazingira ya rushwa kila wanakogeuka. Hiyo ndio rushwa Tanzania.
Tasnia ya sanaa, kwa kuwa ni sehemu ya jamii ya Tanzania, haijakwepa donda ndugu hili la rushwa. Rushwa katika tasnia hii haijaanza leo, ilianza tokea kipindi cha Uongozi wa mwalimu Nyerere ambapo shughuli za sanaa zilihitaji vibali mbalimbali ili kuweza kufanyika. Hili liliwapa watu wachache madaraka ya kuamua hatma ya vikundi vya sanaa na wasanii binafsi. Maafisa utamaduni walikuwa watoaji wa vibali vya kila onyesho la sanaa, na walikuwa na uwezo wa kukataa kutoa kibali bila sababu yoyote, na ilikuwa ngumu kwenda kukata rufaa popote zaidi ya kumbembeleza afisa huyo. Ililazimika msanii uwe na kibali kwa kila kitu utakachofanya, hata mazoezi sehemu nyingine yalikuwa lazimayapate kibali toka kwa Afisa utamaduni, kwa mfano kulihitajika kibali cha kutoka nje ya mkoa, ambacho alilazimika kupata kwa Afisa Utamaduni wa Mkoa wa Mkoa wake, kisha kukiwakilisha kwa Afisa utamaduni wa mkoa unaokwenda na huko utapewa kibali cha kuingia katika Mkoa, ambacho utaenda nacho kwa Afisa Wilaya ili kupata kibali cha kufanya shughuli katika Wilaya yake, yote hii ilikuwa mianya mikubwa ya rushwa. Wasanii wengi wa zamani watakueleza adha waliokuwa wakipata pindi kundi lao likipata mualiko nje ya nchi, ili kupata passport ilikuwa lazima kupata vibali husika toka kwa maafisa wa Wizara ya Utamaduni, hapa rushwa hutajwa sana, katika utafiti wa makala haya bahati mbaya sana kiongozi mmoja anaeheshimika sana katika tasnia ya utamaduni anatajwa kuwa alikuwa kikwazo kikubwa kwa wasanii na kila mara kuomba rushwa au kulazimisha nafasi za kuandamana na kikundi katika safari. bahati mbaya mpaka leo baadhi ya maafisa wa utamaduni wanaendeleza tabia hii chafu.
Nchi hii ilianza na radio moja ambayo baada ya Uhuru ilikuwa mali ya serikali. Kwa muda mrefu studio pekee za kurekodi zilikuwa kitengo katika redio (TBC na baadae RTD). Ili nyimbo ziweze kurekodiwa kulikuweko na utaratibu wa kamati za kusoma mashahiri ya nyimbo kabla ya kurekodi. Hapa ndipo palipoanzia rushwa, kamati haikujulikana mipaka yake, na wasanii walikuwa wakikutana tu na watangazaji walioko kitengo cha Music and Drama cha radio na hao ndio waliokuwa na uwezo wa kukubali au kukataa kurekodi nyimbo. Rushwa kubwa ilianzia hapa, na baada ya nyombo kurekodiwa ndipo ikaanza rushwa ambayo iko mpaka siku ya leo, ambapo wanamuziki walitoa rushwa ili nyimbo zao ziweze kupigwa redioni. Katika enzi hizo nyimbo zililzimika kupigwa ili zifahamike na bendi iweze kufanya naonyesho.........INAENDELEA

Comments