JE UNATAKA BENDI YAKO IFANYE ONYESHO ZURI ?- SOMA HAPA


Hakuna siri  kuwa kwa bendi yoyote ‘live’ni moja ya mambo muhimu katika kazi mwanamuziki kwa sababu mbili. ‘Live’ ni chanzo muhimu cha mapato ya bendi na promo kubwa katika kuongeza mauzo na CD na DVD za bendi. Kwa sababu hii lazima lengo la kila show iwe ni kuhakikisha kusimamia na kulinda ubora wa kazi bendi inayofanya. Ubora wa onyesho hujenga mahusiano chanya na kumbi ambapo bendi hufanya maonyesho hapo ni kuongezeka kwa fursa za mapato zaidi. Mambo muhimu ni ya kuanza nayo ni matayarisho ya maonyesho. Matangazo ni muhimu sana, tuma mabango mengi mapema, ikiwezekana katika zama hizi tumia vyema Facebook na Tweeter kufikisha ujumbe wa onyesho. Hakikisha vyombo vya utangazaji vinapata matangazo bila kuweka ubaguzi katika matangazo kwa vyombo fulani tu, inaweza ikakuletea matatizo ya kukosa watu kwa kuwa tu umetangazwa na chombo fulani, katika enzi hizi za ‘Mabif’ si busara bendi kujikuta katikati ya Bif ambalo bendi haihusiki. Toa taarifa za maendeleo ya matayarisho yote  ya onyesho kwa waandishi kila mara. Tuma CD au DVD za muziki wako kwenye vituo vya redio na TV vyote vya mji unaokwenda kupiga muziki, bila kusahau kwenye ukumbi utakao piga, ili wazipige sana kabla bendi haijafika. Bendi ifanye utafiti, na kujua inakokwenda wanapenda kusikia nini? Kuna utani wa eneo lile? Mkasa wa kuchekesha wa lile eneo? Yajulikane na kutumiwa kwenye maonyesho.
Bendi ihakikishe inawahi kwenye maonyesho, hakuna kitu kinaudhi watu kama wateja kufika kwenye ukumbi na kukuta wasanii hawajafika. Kuwahi kufika kunasaidia kucheki kama vyombo viko sawa ili muda ulioandikwa wa kuanza onyesho usiwe muda wakuanza kutengeneza vyombo.
Onyesho lilikanza liwe moto chini, hata kama hakuna watu,  muziki upigwe kama watu wamejaa kibao, ikifanywa show kwa unyonge hata wale waliokuja hawatarudi, lakini show nzuri inaweza kukuhakikishia kupewa nafasi ya kufanya onyesho tena na habari zitasambaa kuwa onyesho lilikuwa safi. Kuwa rafiki na heshimu kila mtu, wasanii wengi hukosea hapa na kujiona nusu Miungu, wakisahau kuwa waliokuja kwenye show ndio wanaokupa unusu Mungu. Kabla ya show ni muhimu wanamuziki kula vizuri, pombe kila mara ni hasara, bahati mbaya wasanii wengi hudhani kuwa ni stimu kidogo inawasaidia kazi, hilo liko kichwani tu ukweli si huo,na kiwango cha stimu huongezeka kila mara, mwanamuziki anaeanza show na bia mbili leo atajikuta analazimika kunywa Konyagi mbili miezi michache baadae. Hakuna mtu  mwenye akili anaingia ofisini na pombe kichwani  kwa nini mwanamuziki uingie ofisini kwako na pombe kichwani? Muhimu sana bendi kutayarisha nyimbo za kuanzia show, nyimbo kama tano au nne kwa lile saa la kwanza la onyesho, bahati mbaya sana bendi siku hizi zinawea kupiga wimbo mmoja kwa saa nzima huu ni ujinga, nani anaweza kucheza saa nzima?  Muhimu kuangalia mapokezi ya watu kwa hizo nyimbo za mwanzo na kiongozi kutengeneza nyimbo nne za saa inayofuata na kuendelea hivyo, muziki unapigwa kufuata matakwa ya watu, bendi nyingi zisizo na msimamo huenda hovyohovyo hata wanamuziki wakigombea nyimbo zao zipigwe bila kujali wateja wanataka nini, onyesho lazima liwe baya hata kama mnajua kupiga vipi. Bendi ikipanda jukwaani wote ni wamoja na marafiki, matatizo mnayaacha nje, mwiko, nasema mwiko wanamuziki kutwangana jukwaani.
 Lazima kila mwanamuziki awe anaweza kujisikia chombo chake mwenyewe na kusikia wenzie hasa bassist, kwani yeye ndie anayeiunganisha bendi pamoja katika jukwaa na ndie anaeshika mkong’osio wa bendi. Kiongozi wa bendi ndie anaeongoza bendi inaenda vipi, siyo kila mtu kuamua lake. Hakuna kitu kinaudhi kama kuangalia wanamuziki wanabishana nyimbo gani ya kupiga wakati watu wakingojea utamu ambao wamelipia. Mwenye kuelewa na aelewe

Comments