Bendi
huwa ni kundi la watu, na ili mambo yaende vizuri huwa na viongozi mbalimbali.
Katika maisha yangu ya kuwa mwanamuziki nimekwishakutana na viongozi wa aina
nyingi sana, ambao kwa wapenzi wa muziki huonekana watu wenye busara na wastaarabu
lakini kwa wanamuziki watu hao wanaweza kuwa ni Ze Komedi kwa wanabendi na mara nyingine watu wa kutisha sana.
Nikisema viongozi hapa nina maana kuanzia wenye bendi, maarufu siku hizi kama
Wakurugenzi, zamani walikuwa wanafahamika pia kama Wenyeviti kwa kuwa bendi
nyingi zilikuwa katika mfumo wa klabu. Pia kuna viongozi waliojulikana zamani
kama Makatibu wa bendi ambao nafasi yao siku hizi imechukuliwa na mameneja wa
bendi. Pia kuna Band leaders, wanamuziki ambao huongoza bendi lakini sio wenye
bendi, hawa walijulikana kwa majina kama Vie, hasa wakiwa Wakongo, Marais wa
Bendi (prezida), Mkuu wa bendi na kadhalika.
Vituko
nitakavyosimulia ni vile ambavyo nimeshuhudia na vile ambavyo nimehadithiwa
lakini nimeweza kupata ushahidi kuhusu tukio. Labda nianze na wale wakurugenzi
ambao ndio wenye vyombo halafu wanataka kuwa wanamuziki. Hawa kwa kweli ni
kundi la wasumbufu sana kwa uzoefu wangu. Miaka mingi iliyopita mheshimiwa
mmoja aliweza kununua vyombo ambavyo kwa siku hizi visingefaa hata kwa mazoezi
lakini viliwezesha mimi na wanamuziki wenzangu tukawa tunamuabudu mheshimiwa huyu. Yeye
alikuwa na baa kadhaa na akaruhusu tuwe tunafanya mazoezi katika baa yake
mojawapo, sijui kwanini ghafla nae akataka kujifunza kupiga gitaa la rhythm,
kwa kweli mazoezi yalikuwa yanasimama mara alipofika, maana alichukua
gitaa na kuanza kuomba aonyeshwe namna ya kupiga. Nimpe sifa kwamba
hakutusumbua bure akaweza kupiga kwa mbali wimbo mmoja wapo na hapo ndipo
akadai lazima awe anaipiga katika maonyesho tuliokuwa tunafanya, na wakati huo
kulikuwa na mtindo wa kunyamazisha gitaa la solo ili lile gitaa la rhythm
lisikike, mheshimiwa hakuwa hata anataka wimbo ufuatiliwe kwa mpangilio, alitoa amri kuwa
katikati ya wimbo akikonyeza tu basi aachiwe nafasi awe anapiga rythm awe anasikika peke yake.
Haikuchukua muda mrefu tukamkimbia nakumuacha na vyombo vyake.
Kuna Mkurugenzi mmoja wa heshima sana aliwahi
kuchukua bendi yake ikaenda kwenye ziara nchini Kenya, na kusafiri miji mingi
sana, na alipoona kuwa mapato ni kidogo, basi akanunua sufuria ili wanamuziki
wawe wakijipikia chakula kwa unga na maharage aliyokuwa akinunua, na malazi yalikuwa kwenye jukwaa mara baada ya kumaliza muziki. Hakukuwa na malipo mengine, bendi
ikaanza kusambaratika hukohuko Kenya, kwa kweli hata nae aliweza kurudi nchini kwa chupuchupu,
lakini hakubadilika kwa kuwa nilipiga bendi ya kiongozi huyo, nakumbuka siku ambayo
mimi na wenzangu wawili tuliacha bendi band. Ilikuwa sikukuu ya Idd, na
kulikuwa na kawaida ya bendi kupiga muziki kuanzia saa 9 mchana mpaka saa 2 au
3 usiku. Tukiwa tunaendelea na muziki katika ukumbi wa Makonde Bar Mikocheni, kiasi
cha saa moja na nusu usiku kiongozi akaingia na kundi la rafiki zake na
wasichana wao, wakacheza sana ilipofika saa 2, akatuambia tufunge muziki,
akampa kila mtu shilingi 3 twende kula kwa mama ntilie jirani kisha tuanze tena
muziki ambao uendelee mpaka saa 7 usiku. Kwa kuwa kulikuwa hakuna matangazo
ilikuwa kama ni party tu ya kiongozi na watu wake, tatizo lilizidi baada ya dansi kukawa
hakuna usafiri wanamuziki tukalazimika kutwanga mguu kila mtu kwake. Kesho yake
tukamrudishia yunifom za bendi.
Viongozi
wengine hupatikana katika njia za ajabu sana, kuna wakati tulikuwa na kikundi ambacho
kilikuwa kimekabidhiwa vyombo na tawi la TANU Youth League, tatizo letu lilikuwa mahala pa
kufanya mazoezi, bwana mmoja ambaye alikuwa mganga wa kienyeji akatupatia
nafasi katika nyumba yake aliyokuwa kapanga kwa ajili ya shughuli zake za
uganga. Ilikuwa na nafasi kubwa natuliweza kufanya mazoezi, ukarimu huu ulirudishwa kwa sisi kumteua kuwa
mlezi wa bendi. Loh mheshimiwa haraka akaanza kutuingiza kwenye mtego wa
ushirikina kwa maelezo kuwa kwa kuwa vyombo vimelala kwake lazima tuanze kuoga
dawa zake kukwepa wabaya wake wasiopenda mafanikio ya kazi zake na za rafiki zake. Ilifika wakati
tukaanza kumpa chochote tulichopata kwa kuogopa kulogwa nae. Salama yetu ilikuja
siku alipomtaka binti moja mapenzi na binti alipokataa akatoa nyoka aliyekuwa
anatembea nae mfukoni akamtisha naye, binti akakimbilia polisi, mheshimiwa
akajakubebwa juu juu japo nyoka alimuachia ili kukosekane ushahidi, nasi
tukahamisha vyombo siku hiyo hiyo.
Nakumbuka bendi moja ambayo tulianza wote tukiwa marafiki, tukila pamoja ugali ambao
ulikuwa ukipikwa na fundi mitambo wakati mazoezi yanaendelea, bila kujali
kiongozi wala mbeba spika. Kiongozi wetu alipatikana kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa na uhusiano na mwenye vyombo, lakini wote tulijisikia kama ndugu na mambo hayo yalienda hivyo mpaka siku moja tulipoenda
kupiga katika ukumbi wa Jeshi Morogoro mjini, ambapo watu walijaa sana kwenye dansi
letu na tukapata shilingi 70,000/- hivi wakati huo kiingilio kilikuwa shilingi
50/-. Kiongozi akapagawa, akahama kutoka kwenye guest house tuliokuwa tumefikia
na kuhamia hotelini ili kulinda fedha. Tuliporudi Dar sheria zikabadilika,
akaitisha kikao na kutoa amri kuwa lazima aamkiwe shikamoo, na kila mtu, kwa
kuwa yeye ndie kiongozi, na kuanzia hapo ikawa ukitaka kuongea nae lazima
umtaarifu katibu wa bendi kwanza nae ndie anamtaarifu kiongozi wa bendi shida yako,
inaweza ikaonekana kama mchezo wa kuigiza lakini hadithi hii ni kweli kabisa.
tatizo kubwa la kiongozi huyu ni ushirikina, hakuwa anaamini kuna kitu kinaweza kufanyika bila tunguli. Hata tulipokuwa tumerekodi nyimbo RTD, siku zinapigwa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha misakato, alikuwa na katibu wake wanafukiza madawa kwenye redio iliyokuwa ikitangaza na kupiga nyimbo hizo!!!!!Siku ya kuacha bendi hii ilikuja baada ya bendi kwenda katika ziara Tanga na nikapata
malaria kali siku ya kurudi. Kulikuweko na treni ya kutoka Tanga kuja Dar,
viongozi walikuwa second class, makapuku tuko third class, ambayo kwa wakati
huo ilikuwa hata sehemu ya kukaa ni tabu. Jitihada zote za wenzangu kuomba
nisafiri na viongozi second class kwa vile naumwa zilielekea kugonga ukuta
mpaka pale walipoanzisha fujo kubwa kwenye treni nikahamishiwa chumba cha ma
Vie, niliposhuka salama Dar es Salaam nikaapa na bendi basi.....(itaendelea
Comments