Mapenzi
kazini mara nyingi ni tatizo, hasa pale maamuzi ya kikazi yanapoanza kuingiliwa
na mahusiano ya kimapenzi. Katika
mabendi kadhaa tatizo hili limejitokeza na mara nyingine kuvunja bendi kabisa.
Tatizo linakuwa kubwa zaidi pale ambapo kiongozi wa bendi ndie mmoja wa
wahusika. Najua watu mawazo yao yanalenga kwa viongozi wanaume kuwa na mpenzi
mfanyakazi mwanamke, kiukweli hali si lazima kila mara iwe hivyo kama
ntakavyowaeleza baadae. Nianze na matukio yaliyonikuta miaka mingi iliyopita
nikiwa katika bendi moja ambapo kiongozi wa bendi alijikuta katika mapenzi
mazito na mcheza show katika bendi. Mheshimiwa huyu alikwisha kabisa kiasi cha
kutumia muda wa mazoezi akiwa guest house na huyu binti hasa kwa kuwa alikuwa na
mke nyumbani kwake. Kiongozi aliacha kabisa kufanya mazoezi na hata binti pia
akawa akija kazini ni kama anakuja kwa kiongozi. Kuna siku tulikuwa na
onyesho Morogoro, binti akagoma kuja, kiongozi alikuwa kama mgonjwa akamtuma
mcheza show mwanaume ambembelezee binti aje kazini, binti akatoa sharti kuwa
lazima apewe shati ambalo kiongozi alikuwa analivaa sana, lilikuwa aina ya
shati linaitwa shati la ndege, kwa miaka hiyo wajanja tu ndio walikuwa wanavaa mashati aina hiyo,
kiongozi akalituma hilo shati binti hatimae akaja kazini kalivaa lile shati.
Kutokana na kukosekana displine katika show na bendi kwa ujumla, taratibu bendi
yetu ikaanza kukosa watu.
Kama
nilivyosema mwanzo kuna akina mama siku hizi wanauwezo wa kifedha sana hivyo
huwa na uwezo wa kununua vyombo na kuanzisha bendi. Ngoma inakuja Mama
mkurugenzi akianguka kwenye penzi la mmoja wa wanamuziki, amri zote zina hamia
kwa mzee, ambae sasa hata kwenye bendi anakuja anapotaka anasema analotaka na
kufanya analotaka. Mara mbili tatu nimekuta mwanamuziki kijana anampata mama
mwenye uwezo, na kumsomesha kuwa anaweza kuendesha bendi itakayokuwa tishio katika nchi. Hapo utakuta mama
haelewi chochote hata ukitaka kumshauri. Atapelekwa kwenye duka la vyombo
Kariakoo na kuonyeshwa vyombo ambavyo bila kujua ataghiribiwa na kutoa fedha mara mbili au tatu ya
bei halisi, wakati huohuo kwa kuwa anayechagua vyombo si fundi vinachaguliwa
vyombo vibovu au ‘fake’, vikashindwa kabisa kutoa muziki ambao mama
alihadithiwa ungetokea. Na mara nyingi mama wa watu akajikuta kila mwezi
anaenda kununua spika mpya wakati mapato sifuri, muda mfupi baade husikii tena hadithi ya bendi. Kutokana na ukungu wa mapenzi, mtu
anashindwa kuona utapeli anaofanyiwa, wakati watu wote pembeni wanashangaa na
wengine kumcheka. Katika kundi la namna hii mara nyingi huwa hakuna muziki
wowote wa maana unaoweza kutokea, mwanamuziki anaweza kujisifia tu kwa bosi kumbe hana lolote ni utapeli tu wa mapenzi, lakini huwa ni mradi ambao hutumia fedha
nyingi sana na kila siku kukawa na ahadi ya siku moja mambo yatakuwa ‘bie’.
Baadae wataanza kutafutwa wabaya wa bendi ikiwemo wanayoiloga bendi na hatimae kimyaaaa. Huruma
sana.
Lakini
pia kuna wakurugenzi wanaume ambao hujikuta katika mapenzi na wafanyakazi wao
wa kike. Mara nyingi hili ni hatari. Kubwa la kwanza ni mfanyakazi kujiona
hawajibiki kwa viongozi wa bendi. Kiongozi wa bendi mmoja alikumbwa na mkasa wa
binti kutokuwa na nidhamu akamtaarifu kuwa atamshtaki kwa mkurugenzi
kuwakeshamshindwa kwenye bendi, akajibiwa,’We utashtaki umevaa nguo, mi ntajibu
mashtaka sina nguo’. Mwenyewe akafyata mkia. Mzee mmoja mwenye bendi maarufu japo kajiwekea kautaratibu, mcheza show mpenzi wake akiaanza kuota mapembe kazini anamtimua kazi haraka. Tabu nyingine huja pale mkurugenzi
wa bendi anapoajiri wanamuziki wa kike kila akiingia katika uhusiano nao, hapo unakuta
ni kama ana wake wengi katika bendi, huo ugomvi na wivu unaoendelea katika wafanyakazi
unaleta fujo katika utawala wa bendi na malalamiko kutoka kwa wanamuziki wengine wazuri ambao si tu wanaona wanadhalilika bali wanajikuta wanagawana mapato na watu ambao kwa kweli hawastahili…….inaendelea
Comments