UZINDUZI WA VICTORIA SOUND

Victoria Sound imezindulia katika ukumbi wa Mango Garden usiku wa tarehe 1.3.2013 . Saa sita na nusu usiku bendi hiyo ilipanda jukwaani na kuanza kuwaonyesha wapenzi walio jazana Mango Garden kile ambacho bendi imetayarisha. Hakika uingiaji wa bendi hii kwenye jukwaa ulikuwa wenye ubunifu, ukanikumbusha uingiaji stejini kama huu wakati Muumin alipoizindua Bwagamoyo Sound katika ukumbi wa Vatican Hotel Sinza miaka kadhaa iliyopita. Mashabiki wa bendi hii ambao walijitayarisha kwa mambango na sharashamra nyingi waliongeza uchangamfu katika uzinduzi huu. Kwa mara nyingine tena Waziri Sonyo alionekana jukwaani akiwa na ule uimbaji wake wa sauti ya juu kuonyesha kuwa bado anakipaji cha uimbaji. Kulikuwa na mambo kadhaa ambayo Muumini atatakiwa ayazingatie ili kujiweka sawa katika mpambano huu aliyojikita. Kwanza lazima kufanyia kazi tatizo sugu la kukosekana kwa muziki ulio balanced, mafundi mitambo wengi hudhani vyombo kulia kwa nguvu ndio kuonyesha ubora wa ufundi wao, kinachotokea ni kelele ambazo hufanya kusikiliza muziki inakuwa adhabu badala ya starehe. Pili ni lazima afanye tena mabadiliko katika muziki wake kwani bado unafanana sana na bendi ambazo ziko hewani, hili ni jambo la hatari kwani watu wanaweza kuona hakuna jipya kimuziki. Wacheza show watalazimika kufanya mazoezi makali ili kujifua zaidi.

-->

Comments