UNAJUA KWANINI BENDI ZETU ZINAKUFA MAPEMA?




Nchinga Sound
Tanzanite Band
Watoto wa tembo
Muziki wa bendi umekuweko katika jamii yetu kuanzia miaka ya 30. Historia inatuambia kuwa baadhi ya bendi za mwanzo ni  YMCA Social Orchestra na Dar es salaam Social Orchestra, bendi hii ya pili ilikuwa ndio chanzo cha bendi maarufu iliyokuja tokea baadae Dar es Salaam Jazz Band, bendi ya kwanza ya aina yake kutumia gitaa la umeme. Kama yanavyoonekana majina yake Social Orchestra, vikundi hivi vilikuwa ni sehemu ya shughuli baada ya kazi. Haikuwa ajira bali shughuli waliyofanya waliopenda kupiga muziki. Kipindi kati ya 1950 na 1960 miji ndio ilikuwa inaanza kujengeka na hivyo watu wa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi walijikuta wakiishi  pamoja mijini, vikundi mbalimbali vilianzishwa vikiwa na malengo ya kukusanya watu waliotoka sehemu mmoja ili kusaidiana katika shughuli kama harusi, vifo na shughuli za namna hiyo, hatimae kulianza kutengenezwa vikundi vya sanaa na hata bendi zenye wanamuziki kutoka sehemu moja na hapo kukawa na bendi kama Rufiji Jazz iliyoanzishwa na wanamuziki toka Rufiji, Ulanga Jazz,  ya watu wa maeneo yale ya mkoa wa Morogoro, au Western Jazz iliyoanzishwa na akina Iddi Nhende kutoka mkoa wa Tabora na kuwa na  wanamuziki wengi kutoka magharibi ya Tanzania hasa mikoa ya Tabora na Kigoma,na vivyo hivyo Kilwa Jazz na kadhalika. Bendi hizi awali zilikuwa katika mfumo wa  klabu. Kulikuweko na kamati za kuendesha klabu na bendi zilitafutiwa sehemu ya mazoezi, wanamuziki walisaidiwa mengi na wanachama wa klabu ikiwemo malazi, chakula na hata posho kwa wale ambao walikuwa hawana ajira, na hatimae kuwatafutia ajira wawee kujikimu. Mazoezi ya vikundi mengi yalifanyika baada ya saa za kazi kutokana na wanabendi wengine kuwa na kazi zao.
Ujio wa wanamuziki wa utoka Kongo mwanzoni mwa miaka ya 60 ulianzisha kubadilika kwa mfumo katika uendeshaji wa bendi hizi. Kukaanza kuweko na utamaduni wa wanamuziki kutegemea maisha kutokana na kupiga muziki. Mifumo ya utawala  wa bendi nayo ikabadilika na kufuata mifumo iliyokuwa imezoeweleka huko Kongo. Kwa wale wanamuziki waliokuwa na vikundi lakini hawakuwa na vyombo waliweza kuwashawishi wenye fedha kuingia katika biashara hiyo kwa kununua vyombo na hatimae kuanza bendi. Kitu kilichokuwa wazi mapema ni kuwa wanamuziki hawakutaka kuingiliwa na wenye vyombo katika utawala au uongozi wa wa bendi. Hivyo bendi zilikuwa na viongozi kama Band Leader ambaye alikuwa kiongozi mkuu wa bendi, kisha kulikuwa na Stagemaster/Bandmaster ambaye ndie alikuwa akiangalia nidhamu wakati wa mazoezi na hata wakati wa dansi na kuongoza mwenendo wa dansi kwa kuchagua nyimbo ipi ipigwe saa ngapi.  Kuonyesha jinsi utawala ulivyokuwa unafuata ngazi nitatoa mfano mmoja binafsi. Nilijiunga na Vijana Jazz mwishoni mwa mwaka 1989, na baada ya miezi miwili nilipewa jukumu la kuwa Stagemaster, tulikuwa na gari la kupeleka wanamuziki kazini, kuna siku tulimpitia Hemed Maneti nyumbani kwake, yeye ndie alikuwa Kiongozi Mkuu wa bendi, lakini siku hiyo alikuwa anaumwa, tulipopita kwake alikuja kwenye basi na kuniomba ruksa asiende kazini kwa kuwa anaumwa. Ukikumbuka kuwa bendi ilikuwa ni kama yake, mimi nilikuwa na miwili tu kazini, lakini kwa kuwa nilikuwa Stagemaster alilazimika kunipa taarifa kuwa anaumwa. Ni jambo ambalo lilikuwa na maana nyingi sana katika utawala wa bendi, mwanamuziki gani angenidharau ikiwa Kiongozi Mkuu alikuwa anakuja,tena mbele ya wanamuziki wote kunitaarifu kuwa anaumwa?
 Katika mtiririko huu, mwenye vyombo, tajiri, alikuwa anakutana na wanamuziki wakati wa kupeana mkataba wa kuanza kazi baada ya hapo mwanamuziki anajua hatima yake iko chini ya Kiongozi wa bendi, na utaingizwa kwenye bendi kwa ushauri wa uongozi wa bendi kwani ndio unajua unahitaji muimbaji wa sauti ya ngapi, au unahitaji mpigaji wa kiwango cha aina gani. Jambo ambalo tajiri anaweza kutokujua kabisa na kuona mwimbaji ni muimbaji tu. Hii iliwezesha wanamuziki kuheshimu uongozi wao wa bendi. Mfumo huu uliendelea hata zilipoanzishwa bendi za mashirika ya umma, muajiri hakuingilia taratibu za uongozi wa bendi bendi labda kwa kupitia mikutano rasmi na viongozi wa bendi, ambapo nao walipeleka misimamo wa uongozi wa juu kwa wanamuziki. Bendi nyingi ambazo wenye mali amekuwa wakiingilia au kugeuka ni viongozi wa bendi matatizo makubwa yamekuwa yakitokea ambayo hudumaza bendi. Hapa sababu ni rahisi, wanamuziki mkiwa wenyewe hamjiangalii kuwa nani maarufu, bali mnajipima kuwa nani anajua nini, mtu nje ya kundi anaanza ikiwemo wenye bendi huanza kuingiza upenzi katika kutoa maamuzi, jambo ambalo huleta tabu. Nimekwisha ona wenye mali wakiwa wapenzi wa aina fulani ya muziki hivyo kulazimisha bendi kupiga muziki wa aina hiyo tu, na hivyo kuzuia bendi kukua kimuziki. Tatizo kubwa zaidi ni wenye bendi kuingilia uongozi wa bendi na kuanza kufanya viongozi wa wanamuziki hawafai na hivyo kuanzisha utamaduni wa wanamuziki katika bendi kudharau uongozi ambao ndio uko karibu nao, na hapo mwanzo wa mwisho wa bendi huwa wazi. 
Bendi ina mvuto wa aina yake. Unaweza kumkuta mtu mwenye kampuni kadhaa, akiwa na waajiriwa wengi na kamwe  hafanyi kitu chochote kuonyesha kuwa yeye ndie  mwenye mali, wala kujihusisha na maisha ya wafanyakazi wake, mara nyingine wafanya kazi wengi wala hawamjui kwa sura bosi wao, lakini mtu huyuhuyu akianzisha bendi anageuka na kutaka kila mtu amfahamu kuwa yeye ndie mwenye bendi,  ataanza kujihusisha kwa karibu na maisha ya wanamuziki, nimeshawahi kulalamikiwa na familia moja baada ya mzee kukaribisha kundi la wanamuziki wake nyumbani kwake wakawa wanashinda hapo wanakula hapo, na yeye mwenyewe, ambaye alikuwa afisa mkubwa kwenye shirika moja akipita sokoni kununua nyama  na vitunguu kwa ajili ya chakula cha wanamuziki wake, na kubadilisha kabisa hali ndani ya nyumbani kwake. Mzee mwingine kwa wale wenye kumbukumbu alikuwa anajitokeza mpaka kwenye luninga akijisifu kwa kwenda Ufaransa kuwanunulia wanamuziki wake nguo, jambo ambalo ungemtajia kuwa angelifanya kwa wafanyakazi wake wa vitengo vingine angekuona mwendawazimu. Wema huu si faida bali ni hasara kubwa katika uhai wa bendi. Bendi nyingi nzuri zimekufa kutokana na kutokuwa na mfumo mzuri wa uongozi na hivyo kutokueleweka nani kiongozi wa kundi, kati ya Mkurugenzi mkuu wa kampuni, meneja wa bendi na Kiongozi wa bendi.
Aina nyingine ya bendi ni  zile ambazo wanamuziki wamejikusanya na hata kuweza kukusanya vifaa wenyewe. Bendi hizi ambazo zinajitawala zenyewe zimekuwa na historia ya kudumu kwa miaka mingi, kwanza kwa kuwa wanamuziki wanajua mali ile ni yao na kila kipatikanacho wanakijua(transparency), hivyo wakati wa shida huwa shida kwa wote na wakati wa raha huwa raha kwa wote, bendi hizi mara nyingi huja kufa vyombo vikisha chakaa, na huwa vigumu kukubali kuishi katika mfumo uliotajwa hapo juu. Mifano hai ni Kilimanjaro Band (awali iliitwa Love Bugs-1960s, kisha Revolutions na hatimae Kilimanjaro Band), pia Tanzanites(awali Barkeys). Bendi zote hizi zina umri wa zaid ya miaka 30.
Pengine ningeongea kidogo kuhusu utengenezaji wa bendi. Ukiwa na fedha zako na unataka kuunda bendi, lazima ukumbuke kuna mambo ya msingi lazima  ujiulize, Je, unataka kutengeneza bendi kwa ajili ya nini? Unataka ikuingizie fedha? Au unataka kuona vijana wakipiga muziki wa kukufurahisha tu? au kutangaza jina au biashara yako na kadhalika. Kwa kutengeneza bendi nzuri ya kukusaidia katika malengo yoyote utakayokuwa umeamua kati ya hayo hapo juu, ni vizuri ukamtafuta mwanamuziki mmoja (responsible), na kumueleza nia yako na kumuachia uhuru wa kutafuta wasanii wenzie. Hapa makosa makubwa huwa yanatokea kwa watu kukusanya kamati ya washauri, na kuanza kupanga wasanii wa kuwapata, hii ina matatizo makubwa, unaweza ukapata wasanii wazuri maarufu lakini hawana mtizamo mmoja kuhusu muziki, na pili hili huleta matatizo katika mahusiano yao na  uongozaji wa bendi. katika hali hii wanamuziki wote wanajiona ni viongozi na wanawajibika kwa Mkurugenzi, bendi inakuwa haikaliki na kifo cha bendi ni wazi tu kitatokea mapema, au kunakuwa hakuna maendeleo ya kimuziki, unakuwa na bendi yenye wanamuziki wana majina makubwa lakini haina wapeni wa kudumu. Nimetaja hapo juu kuwa ni muhimu kutafuta mwanamuziki (responsible) kwa kuwa watu wengi wamejikuta wakiangukia kwa wanamuziki wanaojua kujisifu sana na mwisho  wa siku hakuna matunda, akina mama wengi wameangukia katika mtego huu wa kununulia vyombo vijana mabingwa wa kujisifu ambao hata ukimwambia atoe ushahidi wa kazi alizowahi kufanya huishia kutoa ushahidi wa kujisifia zaidi.
Vyombo vya muziki ndilo jembe la kazi, lakini si kila mwanamuziki anajua vyombo bora. Hili ni tatizo sugu, hapa nchini asilimia kubwa ya vyombo vya muziki ni’fake’, hivyo kuandamana na mtu asiye na ujuzi wa vyombo utaishia kununua makopo ambayo miezi michache baada ya kununua yanakuwa ni ya kutupwa wakati mamilioni ya fedha yamekwisha tumiwa. Hata kama vyombo vyote mtaani vingekuwa si bandia , kuna kazi ya kufanya kabla ya kununua vyombo. Maswali ya kujiuliza ni aina gani ya muziki unataka kupiga, unategemea kupiga katika kumbi za ukubwa gani na maswali mengine kama haya, majibu yake yatakupa aina ya vyombo vya kununua , uwezo wake na kadhalika. Kimsingi kabla hujatumia fedha kununua vyombo tafuta wataalamu, utatumia fedha chache na kupata vyombo vitakavyoishi miaka mingi zaidi………….

Comments