Makala hii nilikwisha itoa kabla, lakini kutokana na hali hii kujitokeza tena naona nirudia tena kuiweka hapa..............
Imani ya uchawi ni utamaduni ambao umekuweko katika jamii
zote za binaadamu kwa maelfu ya miaka. Historia na maandiko ya dini
mbalimbali yanatukumbusha hilo na kulilaani. Huwa inategemewa kuwa kadri
maendeleo na elimu yanavyoongezeka ndio imani hiyo inavyopungua na
kupotea, lakini ni wazi safari bado ni ndefu kwani ukipita katika mitaa
mingi utaona vibao vikiashiria waganga wanaoweza kutibu magonjwa
mbalimbali, na hata kutangaza ‘kusafisha nyota’, ‘kuondoa majini’ na
kadhalika.
Tasnia ya muziki kwa kuwa ni sehemu ya jamii, haijakwepa
kuguswa na tatizo hilo. Kutokana na mimi mwenyewe kufanya kazi katika
bendi mbalimbali niliona na kusikia vituko vingi vilivyohusishwa na
imani ya uchawi. Mara ya kwanza kuanza kuona vitimbi hivi ‘live’ ni
nilipojiunga na bendi moja ambayo ilikuja kuwa maarufu sana wakati wake.
Kwa mara ya kwanza nilishuhudia kiongozi wa bendi yangu akiwa na katibu
wake wakiwa wanafukiza kwenye radio majani fulani wakati kipindi cha
Misakato kikiwa hewani. Misakato kilikuwa ni kipindi kilichokuwa hewani
kila Jumanne saa tatu na robo asubuhi, katika redio ya RTD,
kikiporomosha nyimbo mpya zilizorekodiwa na pia kutoa maelezo kuhusu
wanamuziki walioshiriki. Siku hiyo vibao ambavyo tulikuwa tumerekodi vilikuwa vikirushwa hewani kwa mara ya kwanza, ndipo viongozi wangu hawa nikawakuta wakiwa katika shughuli ya kufukiza radio, kwa
imani kuwa kwa kufanya hivyo, vibao hivyo vitatikisa wasikilizaji wake.
Baada ya hapo vituko vingi viliendelea hatimae tulimzoea kiongozi wa
bendi yetu kuwa ni mshirikina. Kuna wakati aliletwa mganga ambaye
alidaiwa aliwahi kuifanya timu moja maarufu ya soka, ishinde kikombe na
kuwa bingwa wa Taifa na alichukuliwa kwa mkataba na bendi na kazi yake
ikawa ni kukaa mlangoni akijifanya ni muuza machungwa. Yeye alidai kila
anapomenya chungwa kwa kuunganisha maganda basi na wateja nao wataingia
katika ukumbi kwa kuunganika, huyu alikaa kiasi katika bendi na tukaweza
hata kusafiri nae kwenda mikoani. Harakati za bendi kutafuta umaarufu
kwa uchawi zilipeleka mpaka bendi ikasafiri hadi kwenda Mpanda, ambako
viongozi wa bendi walikwenda kwa mganga na kufanya mambo yao
yalioyohusisha na hata kumchinja mbuzi ambaye nadhani masharti yalikuwa
ni sisi wanamuziki wote tule kipande cha mbuzi yule wa kafala. Sijajua
hatima ya nyama ya mbuzi yule maana wanamuziki walifanya mgomo wa kumla
yule mbuzi. Kiongozi wa bendi katika safari hiyo, alichanjwa shingo yote
na akawa na mikrofon ambayo wengine wote tulikatazwa kuitumian na
sikuona mtu akiigusa mpaka nilipoacha bendi. Ushirikina
una matatizo ya kufanya watu wasiaminiane hata kwenye bendi yenyewe,
haikuchukua muda mrefu bendi ilipoanza kupoteza umaarufu, Kiongozi wa
bendi akaaitisha mkutano na kutuambia kuwa kuanguka kwa bendi kunatokana
na mmoja wetu kuiloga bendi, hapo ikatolewa tishio kuwa mtuhumiwa
asipojitaja mwenyewe na kuomba msamaha mganga atamfanya awe kichaa.
Jambo ambalo liliungwa mkono na wote kuwa kama ni kweli kuna mtu namna
hiyo basi apate uchizi. Hakuna aliyekumbwa na tatizo hilo mpaka leo.
Miezi
michache baadae, wanamuziki wawili walioamua kuacha bendi walirudisha
uniform zao shati zikiwa zimechanywa kwenye kwapa na suruali kuchanywa
kwenye maungio ya miguu kwa imani kuwa hizo ndizo sehemu zenye jasho kwa
hiyo zingeweza kutumiwa na bendi kiuchawi kuwaharibia maisha.
Katika
mizunguko kwenye bendi mbalimbali, nilikuwa katika bendi ambapo siku
kukiwa na mpambano wa kupiga bendi zaidi ya moja katika ukumbi mmoja,
basi hapo mganga maalumu lazima atafutwe ili kuilinda bendi isimalizwe
na wapinzani. Ilikuwa inaaminika kuwa katika mpambano wa bendi, uchawi
hutumika kuimaliza bendi ambayo itakuwa haina kinga. Kwa siku hiyo ndani
ya spika kuliwekwa tunguli na hirizi mbalimbali tayari kwa mpambano.
Kwa
ukweli kabisa hata wanamuziki kutembeleana zamni ilikuwa ni vigumu,
kwani ukionekana mwanamuziki wa bendi nyingine katika ukumbi, basi bendi
iliyo jukwaani haina raha, anaweza hata akatumwa mtu kufuatilia kila
utakachofanya. Na ilikuwa vigumu kuruhusiwa kugusa vyombo vya bendi
nyingine kwa wasiwasi wa kuwa unaweza ukaloga kile chombo.
Kulikuwa
na hadithi nyingi kuhusu ni kiasi gani bendi ziliweza kufanya ili
kupata wateja. Kuna bendi ambayo ilisifika kuwa kila wakimaliza kupiga
walipita katika kumbi na kuokota vizibo vya chupa, mifupa, na hata
kupata maji toka chooni kwenda kuloga ili wale walioingia wasiingie
bendi yoyote kasoro yao. Bendi nyingine zilidaiwa kuwa ziliweka mkataba
ambapo zililazimika kutoa kafala ya mtu kila mwaka, hivyo viongozi wa
bendi kufiwa na watoto, na hata wanamuziki wageni katika bendi hizo
kukutwa na mauti ambayo, kwa chinichini yalidaiwa ni katika kutoa
kafala.
Bendi
mbili ambazo zilikuwa na upinzani mkubwa katika jiji la Dar es Salaam
zilidaiwa hata kutaka kuweka uchawi katika chanzo cha maji Dar es Salaam
, na kujikuta wakitaka kuumbuana hadharani kuhusu hilo.
Kama
nilivyosema imani ya uchawi huleta kutokuaminiana na hata madhara
makubwa ya kutuhumiana mambo ambayo mara nyingi hayana ukweli wowote.
Kuna mwanamuziki niliyejaribu kumshawishi aingie katika bendi niliyokuwa
nikipigia , alikataa katakata kwa kuwa alidai mmoja wa wanamuziki
katika bendi ni mchawi. Mwanamuziki mmoja aliwahi kuhadithia jinsi
alivyopita uchochoro wa nyumba ya mwanamuziki mwenzake akashangaa
kusikia jina lake likitajwa na mwenzie aliyekuwa chumbani kwake na
kusema,’ Nyota ya …….izimike kama kaa hili’, akadai alichungulia katika
ufa na akakuta mwenzie anatumbukiza kaa la moto kwenye maji. Ugonjwa wa
ukimwi ulipoanza kuuwa wanamuziki kwa mara ya kwanza mara nyingi
ulihusishwa na uchawi. Rafiki yangu mmoja nilipomtembelea wakati akiwa
hoi kitandani akanambia,’Nikupe siri? Mi ntakufa lakini nauawa na
wanamuziki wenzangu kwenye bendi. Nimepata mganga kanitajia na majina
kabisa’. Miezi michache baadae mwanamuziki huyu kabla hajafariki
alinambia,’Mjomba sijalogwa wala nini, udude huu, unaniua udude’.
Alifariki siku chache baada ya kunambia haya. Mungu amlaze Pema peponi
Mjomba.
Kitu
ambacho kimenishangaza karibuni tuhuma kuwa kuna wanamuziki wa kizazi
kipya wanaendeleza imani hii ya ushirikina. Producer maarufu amejitokeza
na kuwakanya wasifanye mambo hayo kwenye studio yake. Na siku chache
baada ya hapo tena mwanamuziki mwingine wa muziki huo kawataja ambao
aliwaita wabaya wake wanaomloga.!!!!!!! Nikaona loh kumbe shughuli bado
inaendeleaaaaaaaa.....UZOEFU WANGU NI KUWA WANAMUZIKI WOTE WALIOAMINI NA KUSHIRIKI KATIKA USHIRIKINA ILI KUJIPATIA UMAARUFU WALIISHIA KUWA WANAMUZIKI WA KAWAIDA TU NA HATA KUPOTEA KABISA TOKA KWENYE ULIMWENGU HUO, UKICHUNGUZA UMAARUFU WAO HAUKUTOKANA NA USHIRIKINA LAKINI ULITOKANA NA UBORA WA KAZI ZAO, JAPO KUNA WAKATI HATA WAO WALIONA WAMEKUWA MAARUFU KWA AJILI YA USHIRIKINA. KAMA UNA KIPAJI,UNAFANYA MAZOEZI INAVYOTAKIWA, UNAFUATA TARATIBU ZA UENDELEZAJI NA UTAWALA WA KAZI ZAKO INAVYOTAKIWA HUO NDIO UCHAWI MKUBWA WA KUFANIKISHA KAZI ZAKO...
Comments