Jana
niliingia katika duka moja la vyombo vya muziki na nikawa na maongezi marefu na
mwenye duka, kati ya mambo ambayo tulizungumzia ni tatizo la watu kuamua kufanya
shughuli za muziki na kuanza
kununua vyombo bila kutaka ushauri wa wataalamu wa mambo ya vyombo vya muziki. Nimeona leo
nizungumzie hilo. Kwanza kabisa kumekuwa na tatizo kubwa la kuweko kwa vyombo
‘feki’ katika maduka kadhaa ya vyombo vya muziki. Hivyo si kila chombo kikiwa
na nembo ya Yamaha ni kweli chombo kutoka kampuni hiyo, kwa kweli asilimia
kubwa sana ya vyombo vya muziki ni feki. Ili kugundua hilo ni muhimu kutumia wataalamu wa vyombo vya muziki. Mfano
wa karibu ni mdau mmoja anaeendesha bendi, kujikuta amekwisha nunua vyombo mara
3 katika miaka mitatu kutokana na vyombo anavyounua kutokukidhi viwango
vinavyotakiwa. Kwa taarifa zilizopo ni kuwa mara ya kwanza aliuziwa na tapeli
aliyejidai katoka Uingereza na vyombo original toka huko, kwa kuwa hakutumia
wataalamu alijikuta vyombo alivyovinunua havina sauti yenye ubora, na si muda
mrefu alikuja gundua kuwa kila kitu alichouziwa kilitengenezwa na mafundi
seremala toka Mwananyamala.
Ni
vizuri kabla ya kutumia mamilioni ya fedha kununua vyombo kutafuta wataalamu
ambao wapo kadhaa hapa nchini ukawaeleza matakwa yako nao wakakupa ushauri wa kitu
gani ununue na baada ya hapo hata kushiriki kuvifunga na kutoa semina fupi ya
utunzaji wa vyombo hivyo kwa mafundi wa bendi na pia wanamuziki wa bendi.
Si
kila mwanamuziki ni mtaalamu wa vyombo bora, si mara moja utasikia mfanya
biashara kasindikizana na mwanamuziki kwenda kununua vyombo na baada ya muda mfupi vyombo hivyo huharibika. Tatizo
jingine la ajabu kabisa katika utunzaji wa hivi vyombo, mtu akinunua gari la
shilingi milioni tatu, kamwe hawezi kumkabidhi mtu yoyote barabarani aliendeshe
gari lake. Lakini utaweza kukuta mtu ananunua vyombo vya muziki vya shilingi
milioni kumi na tano na haoni tabu kumuita ndugu yake na kumwambia awe ndie
fundi mkuu, kwa vile tu ndie huwa anabadilisha balbu nyumbani kwake. Na si
ajabu hata kidogo kukuta mafundi mitambo katika bendi nyingi ndio wanaopata
mshahara mdogo kuliko msanii mshiriki mwingine yoyote katika bendi. Hii
imetokana na kuwa mafundi mitambo wengi walianza kazi katika bendi kama wabeba
vyombo, baada ya kujua waya gani unaingia wapi, hupanda cheo na kuwa mafundi
mitambo. Matokeo ni muziki wenye sauti mbovu na vyombo kufa mapema hata kama ni
bora.
Kampuni
mbalimbali huwa na utalaamu unaozidiana katika kutengeneza vyombo. Kuna kampuni
ambazo ni mahiri katika kutengeneza vifaa vya studio, lakini vifaa vya kampuni
hiyohiyo ukitaka kuvitumia maonyesho ‘live’ aidha vitakuwa havina ubora wa
sauti au vifaa hivyo kuharibika mapema.
Kuna majina ya kampuni ambazo ni mahiri katika vifaa vya aina fulani kwa mfando Roland ni
mahiri sana kwa vinanda, ni vizuri kujaribu kupata vinanda vya kampuni hiyo
kwani huwa vinavumilia sana mikiki mikiki ya bendi zetu. Kwa bendi ambazo
zinahitaji kupata amplifaya kwa ajili ya magitaa, ni ushauri mzuri kutumia
combo aina ya Marshal au Fender, japo kweli vifaa hivi ni gharama sana lakini
kampuni hizi zina historia ya umaarufu wa kutengeza amplifaya kwa ajili ya
wapiga magitaa wa muziki wa rock, ni aina ya mashine ambazo zinaweza kutoa
sauti inayofaa kwa ajili bendi zetu. Kwa upande wa gitaa la bezi ningeshauri
mashine za Lanney kampuni hii hutengeneza mashine bora za bezi. Kuna kampuni
ambazo ni maarufu kwa utengezaji wa mixer bora kwa ajili ya maonyesho live.
Soundcrafters na Yamaha ni kati ya kampuni zenye mixer bora. Magitaa hutengezwa
na kampuni nyingi sana, lakini kuna kampuni kama Fender na Ibanez ambazo
huteneza magitaa mazuri yenye pickup zenye nguvu na ambazo zinadumu.
Pamoja
na ushauri huu ni muhimu kupata mtaalamu kwani kila kundi huwa na mahitaji
tofauti, yanayo husu aina ya muziki, ukubwa wa sehemu ambayo maonyesho yanategemewa
kufanywa na kadhalika. Vyombo vya
muziki ni gharama sana na ndio jembe la bendi, vikitunzwa vizuri vinaweza
vikatumika kwa miaka mingi bila matatizo, ni muhimu kufuata masharti
yanayotolewa na fundi mwenye uelewa
Comments