JE TUNAENDA MISIBANI KUUZA SURA?

Katika kipindi cha  kuanzia 2011 hadi sasa, tasnia ya sanaa hapa Tanzania imepata bahati mbaya ya kuwapoteza wasanii kadhaa kwa vifo. Mungu amewapenda zaidi na hawako nasi. Kama ilivyo kawaida ya binadamu simanzi imetushika kwa kuondokewa na wapenzi wetu. Lakini kuna mambo ya kushangaza nimeanza kuyaona ambayo naona ni vema niseme.
Kwa mtizamo wangu kila mtu ana njia zake za kusikia uchungu kwa msiba wa binadamu mwenzie , rafiki au ndugu. Wengine hulia na kuzimia, wengine hutafuta mahala pa kificho wakatoa chozi zito kisha wakajitokeza mbele za watu wakiwa wamekwisha pangusa machozi na kubakia na uchungu wao moyoni. Wengine huonyesha  uchungu wao kwa kusaidia kufanikisha kwa njia moja au nyingine msiba wa mpendwa wao bila usoni kuonyesha dalili zozote za kuumia, japo moyoni anaugulia kwa machungu, namfahamu mtu mmoja ambaye huogopa kwenda msibani maana hujisikia uchungu mpaka 'presha' humpanda
Kinachoonekana sasa ni taratibu watu fulani kuwa mapolisi wa nani kasikitika vipi katika msiba. Utasikia tuhuma, ‘Fulani hakuweko msibani’, ‘Fulani alivaa nguo nyekundu msibani”, ‘Oh nilimuona kacheka msibani’, ‘Hakutoa mchango mkubwa’ na kadhalika. Pamoja na jambo hilo kwa juu juu kuonekana kuwa ni jambo zuri la kuhamasishana, matokeo yake ni kuongeza unafiki na kugeuza msiba mahala pa kuuzia sura. Watu wanalazimika kukaa kona ambapo wataonekana kuwa walikuweko, au kuna kulia kwa ziada kuonyesha kuwa una uchungu zaidi, kutoa kauli hata za uongo kuonyesha ukaribu na marehemu, na mwisho msiba unageuka mahala kama piknik fulani. Nadhani tuache utamaduni wa kunyoosheana vidole baada ya msiba na kumuachia Mungu shughuli za kuhukumu.

Comments