Historia fupi:
Kabla
ya ujio wa wakoloni, historia ya utamaduni katika nchi nyingi za Afrika
inafanana sana. Maendeleo ya utamaduni yalianza kuwa tofauti kutokana na
wakoloni waliochukua nchi tofauti. Nchi zilizokuja kutawaliwa na Waingereza
zilikuwa na safari tofauti kiutamaduni na nchi zilizotawaliwa na Wafaransa.
Waingereza walijitahidi kufuta utamaduni wa nchi walizozitawala na kuingiza
utamaduni wa Kiingereza. Mifumo ya elimu, na utawala ilisisitiza zaidi katika
kuonyesha ubora wa utamaduni wa Kiingereza, na ilikuwa ni ufahari kwa wasomi na
watu ambao wanaonekana wa kisasa kuonyesha dharau kwa utamaduni wa asili wa
kwao, na hili si siri linaendelea mpaka siku hii ya leo nchini kwetu.
Baada ya kupata Uhuru, tatizo hili lilikuwa wazi kiasi cha Mwalimu Julius
Nyerere katika hotuba ya uzinduzi wa Jamuhuri ya
Tanganyika tarehe 09.12.1962, pamoja na masuala
mengine, aliongelea kuhusu historia ya utamaduni wa Tanganyika. Naye alitamka kwamba nchi isiyokuwa na
utamaduni wake haina tofauti na mkusanyiko wa watu ambao hawana roho
iwawezeshayo kuwa taifa. Alivilaani vitendo vya wakoloni vya au kuwafanya
Waafrika waamini kwamba
hawana utamaduni
wao wenyewe; ama kuufanya utamaduni wa Kiafrika uonekane kitu cha ovyo.
Kutokana na hili, wengi wa waliokuwa wamesoma na kupata elimu ya Kizungu
waliojiona kuwa ni “wastaarabu” walijifunza kuwaiga Wazungu kiasi kwamba kuwa
Mwafrika msomi kulimaanisha kuwa Mzungu Mweusi. Suala la muziki, kama nyanja
muhimu ya utamaduni katika historia ya Tanzania, limekuwa ainisho muhimu la
migogoro ya kitamaduni, na Mwalimu Nyerere katika hotuba hii alizungumzia juu
ya muziki. Kwa maelezo yake, waliokubuhu katika elimu ya kikoloni walifunzwa
kuimba nyimbo za Kizungu, lakini siyo za Wahehe au Wanyamwezi. Walifunzwa
kucheza
“rumba”, “cha cha”, “rock ‘n’roll”,
“twist, “waltz” na
“Foxtrot”. Lakini wengi walikuwa
hawajawahi kucheza au hawakujua chochote kuhusu “Gombe Sugu”,
“Mangala”, “Nyang’umumi,” “Kiduo”,
“Lele Mama”, au
“Mganda.” Wengi wa waliosoma
wakati wa ukoloni walijua kupiga gitaa au piano, lakini walikuwa hawajui kupiga
ngoma. Haya yalitamkwa mwaka 1962, wakati ambapo
kulikuwa hakuna mitandao ya kimawasiliano, video wala televisheni, kama ilivyo
leo hii!
Baada
ya kipindi hicho kulikuweko na jitihada kubwa za serikali na Chama tawala
kuwafanya wananchi wajitambue kupitia utamaduni wao. Mambo mengi yalifanyika
kutimiza azma hiyo, wananchi walihamasishwa kuanzisha vikundi vya sanaa katika
sehemu mbalimbali, vijijini, sehemu za kazi mashuleni na kadhalika. Mashindano
na matamasha mbalimbali yalihamasishwa na vikundi vilipewa nafasi katika hafla
mbalimbali za kuanzia vijijini
mpaka kitaifa. Vikundi vya sanaa vya kitaifa vikubwa pia vilianzishwa , ambavyo matunda yake yanaendelea
kuliwa mpaka leo, kwa wasanii kutoka vikundi hivi wamekuwa waalimu wa vikundi
vingi sana maarufu hapa Tanzania, na wengine kuendelea kuwa viongozi wa
shughuli mbalimbali za sanaa nchini. Muziki ni sehemu ya utamaduni, kwa hiyo
ulipitia ngazi zote nilizozitaja hapa juu. Kutokana na hali hiyo, vikundi vya
muziki vilikuweko kuanzia ngazi za mitaa na vijiji. Shule zilikuwa na vikundi vya muziki wa bendi, kwaya,
taarab na muziki asili. Lakini licha ya mipango yote hiyo kulikuwa hakuna
mpango maalumu wa kusambaza sanaa ya nchi hii nje ya mipaka, kubwa ni kwa
sababu nia ya mipango yote ilikuwa ni kuhamasisha wananchi kujitambua.
Wanamuziki
walikuwa wakirekodiwa muziki wao katika studio za Radio Tanzania. Na kazi hizi
zilirekodiwa kwa kuelewa wazi kuwa zitakuwa kwa ajili ya matumizi ya radio tu
na kwa matumizi ya Watanzania tu, hivyo kulikuweko hata kamati maalumu ambazo
zilikuwa zikifuatilia maadili ya tungo hizo ili zikidhi hadhi ya Watanzania. Vikundi ambavyo vilikuwa vikitaka
kurekodi nyimbo zao katika santuri vililazimika kuvuka mpaka wa nchi na kwenda
kurekodi nchini Kenya ambako kulikuwa na kampuni zenye uwezo wa kurekodi na
kuchapisha santuri. Baadhi ya kampuni hizi zilikuwa ni sehemu ya kampuni kubwa
za kimataifa za usambazaji wa kazi za muziki na hivyo kuweza kusambaza kazi
hata nje ya Afrika mashariki, hili lilifanya baadhi ya wanamuziki wa Tanzania
kuanza kufahamika hata Afrika Magharibi. Wimbo Tufurahi Weekend wa Bendi ya
Afro70 uliweza kufika katika top ten nchini Nigeria muda mfupi baada ya
kutolewa 1972. Kutoka na
matatizo ya kuvunjika kwa Shirikisho la Afrika Mashariki mpaka wa Tanzania na
Kenya ulifungwa mwaka 1977 na hivyo kufunga njia pekee ya wanamuziki wa
Tanzania kuweza kutoa santuri ambazo ndizo zilikuwa njia pekee kwa wakti huo wa
kuwezesha muziki wan chi hii kuvuka mipaka ya nchi hii. Serikali ya Tanzania
iaanzisha Tanzania Film Company ilikuweza kuwezesha wanamuziki wan chi hii nao
weweze kutoa santuri. Studio zilianzia Mtaa wa Nkhruma na hatimae kuhamia
Mikocheni eneo la Cine Club, kwa sasa sehemu hiyo ni sehemu ya bar na mgahawa
maarufu. Serikali pia ilijaribu kuanzisha kiwanda cha santuri ambapo majengo ya
kiwanda hicho ndipo kilipo Chuo Kikuu cha Uandishi wa Habari!!! Bahati mbaya
malengo haya hayakutimia, na teknolojia mpya ya kanda za kaseti ikaingia
mwishoni mwa miaka ya 70. Hapo ndipo biashara haramu ya kuuza kazi za muziki
ikaanza rasmi.
Biashara huria
Kufunguliwa
kwa biashara huria kulikuja lakini kulikuja katika hali ambayo biashara ya
muziki Tanzania ilikuwa chini ya maharamia kutokana na kutokuweko na sheria
nzuri za Hakimiliki. Kama ilivyo katika jamii yoyote isiyo na sheria ya
Hakimiliki biashara hii haramu huwa ya siri sana na isiyo na mpangilio rasmi,
hivyo basi taratibu ambazo hutakiwa ziwepo katika nchi yenye mpangilio safi wa
Music Industry, hazikutengenezwa na mpaka tunavyoongea leo hakuna taratibu wala
mpango wa kuwa na taratibu hizo. Wafanya biashara hawa lengo lao kuu ilikuwa
kupata faida tu na si kuendeleza muziki, hivyo hawajawahi kuwa na nia ya kuuza
muziki nje ya nchi. Wafanya biashara hawa wamekuwa wakisisitiza muziki ambao
wanaona unauzika hapa nchini. Wakijali maneno yaliyomo katika muziki na aina ya
muziki walioona unauzika nchini, na kamwe hawakutoa nafasi kwa kazi ambazo
pengine zingeuza nje ya nchi.
Vyombo vya habari
Hakuna
ubishi kuwa vyombo vya habari vimekuwa vingi sana nchini, lakini pia hakuna
ubishi kuwa mchango wake katika kusaidia kukuza soko la muziki nje ya nchi hii
umekuwa mdogo sana. Pamoja na matatizo makubwa ya hakimiliki, lakini kumekuweko
na tatizo la muda mrefu la wafanyakazi wa vyombo vya habari kujihusiha katika
kazi za wasanii binafsi na kutumia nafasi zao kuendeleza au kuangusha
wanamuziki. Tumeona watangazaji wengi wakiingia katika kuchukua nafasi za
umeneja wa wanamuziki, na hivyo kujikuta wakifanya kazi zao huku wakiwa na
‘personal interests’. Kumekuweko na kampuni za ‘kuendeleza wanamuziki’ ambazo
zimekuwa na uhusiano wa karibu sana na vyombo vya habari, hivyo kuwa ni
mafanikio kwa wanamuziki wengine na kikwazo kwa wanamuziki wengine. Lakini pia
wote hawa wamekuwa na nia tu ya kuuza kazi hizo nchini bila kuwa na lengo wala
nia ya kuuza nje ya mipaka ya nchi hii. Rushwa katika vyombo vya habari pia
imekuwa ni tatizo la miaka mingi. Rushwa imesababisha kazi ambazo hazina ubora wowote kupigiwa debe na vyombo vya
habari kuwa ndizo bpra, nah ii kufanya hata vijana wenye nia na kipaji cha fani
husika kuanza kuiga na kuendeleza
sanaa ambazo hazina ubora uliosifiwa. Pia kusababisha kuangusha wasanii wenye
uwezo mkubwa ambao hawana au hawataki kutoa rushwa, popote penye rushwa kamwe
hakuna haki. Mara chache sana ukasikia wimbo wa kuweza kuingia katika soko la
kimataifa ukipigwa katika redio zetu ambazo nazo zote zimekuwa na utamaduni wa
kupenda aina moja tu ya utangazaji, jambo ambalo linazuia maendeleo ya kweli ya
sanaa.
Vision ya serikali
Kwa
msanii wa kawaida vison ya serikali kuhusu biashara ya muziki kwa ujumla,
haieleweki kama ipo. Taratibu za serikali zinaonyesha wazi kuwa nia ya kuu ya
serikali ni kukusanya mapato kutoka kwa wasanii na ndio kazi yao inapoishia.
Hiyo ndio kazi inayoonekana ya Maafisa Utamaduni kote nchini, ugomvi mkuu ni kuhusu
vibali na michango mbalimbali. Sera ya muziki ingekuwa chombo muhimu kwa serikali
kupanga taratibu zake kuhusu maendeleo ya muziki. Hapa moja kubwa ni elimu ya
muziki ambayo pamoja na kuwa syllabus yake ipo, utekelezaji hakuna. Ni wazi
lazima serikali ichukue nafasi yake katika hili.
Wanamuziki
Ni
wanamuziki na vikundi vichache sana nchini ambavyo vinania ya kuuza muziki wake
nje ya mipaka, mara nyingine unajiuliza kama kweli wanataka kuuza kwa mtu
yoyote. Na hili ni tatizo kubwa kuliko yote. Wasanii wengi hujitokeza na
kutangaza kuwa wanataka kuingia katika soko la kimataifa lakini matayarisho ya
kazi hayaenda na nia ya kazi yenyewe. Wanamuziki wenyewe lazima wafanye
mabadiliko makubwa katika taratibu zao, kuanzia kiutawala, kiusanii na
kibiashara.
Comments