John F Kitime-mwanamuziki |
Mwaka 2012 ndio huoo umetokomea, ni vizuri kuangalia
yaliyopita ili kujitayarisha na yajayo. Muziki wa nchi yetu ulitawaliwa na
muziki wa Bongoflava, Taarab, muziki wa bendi, matarumbeta, muziki wa Enjili,
na muziki wa kiasili. Si siri kuwa muziki wa Bongoflava ndio uliokuwa ukitawala
katika vyombo vya habari na sehemu nyingi za maonyesho ukifuatiliwa na muziki
wa Taarab na muziki wa enjili.
Katika muziki wote huu jambo lililokuwa wazi ni kuwa waimbaji ndio
waliokuwa wakipewa kipaumbele katika tasnia hii. Waimbaji katika aina zote za muziki uliotajwa hapo juu ndio
waliotajwa na kupewa sifa kwa ubora wa muziki. Kumekuweko na mashindano kadhaa
ambayo yote yamejikita katika kutafuta vipawa vya waimbaji japo mara nyingi
yamejitambulisha kama mashindano ya kusaka vipaji mbalimbali. Hakuna ubishi
muziki wa dansi na muziki wa asili ndio muziki uliopewa muda mchache sana
katika vyombo vya habari. Na hata katika muziki huo, bendi ambazo zimejikita
kufuata mipigo ya Kikongo vilipewa nafasi zaidi ya bendi ambazo zimejichagulia
njia nyingine za muziki wao.
Kuna sababu kadhaa ambazo zimefanya muziki wa bongoflava
kuchukua nafasi zaidi katika vyombo vya habari, la kwanza ni uwingi wa kazi za
bongoflava zinazorekodiwa. Karibu kila mji una studio ya aina moja au nyingine,
na katika studio hizo kazi nyingi zaidi zinazorekodiwa ni aina hiyo ya muziki,
hivyo kutokana na uwingi wa kazi hizo ni wazi kabisa ndizo ambazo zitaendelea
kutawala anga la vyombo vya habari, na pia ni kutokana na mfumo wa vyombo vyetu vyote kujikita
katika mfumo wa aina fulani tu za muziki.
Kwa mtizamo wangu heka heka za muziki wa Enjili zilipungua
2012. Yale matamasha makubwa ya muziki huo yalipungua sana, na hata nyimbo za
kushtua jamii hazikuwa nyingi kama
ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Muziki wa Taarab haujaleta mabadiliko kimuziki, mengi
yaliyofanywa katika 2012 ni marudio tu ya ubunifu uliofanyika nyuma. Kama vile
uanzishwaji wa kucheza show katika taarab, upigaji wa gitaa na kuliachia pekee
yake kama ilivyokuwa kwa bendi kuachia gitaa la rhythm miaka kabla ya tisini na zile video za kucheza mbele za viwanja vya hoteli.
Kumekuweko tu ubunifu wa misemo na mipasho, jambo tena ambalo limesababisha
kuenziwa zaidi kwa waimbaji tu katika fani hiyo pia.
Bendi ziko katika wakati mgumu, wakati wanamuziki wengi wa
bendi wakilalamika kuwa muziki wa bendi haupigwi, kumekuweko na jitihada ndogo
za bendi kurekodi nyimbo mpya, maelezo mengi yamekuwa ni kuhadithia enzi ambapo
muziki wa bendi ulitawala na kuona kama hiyo ni sababu tosha ya muziki huo
kurushwa hewani. Bendi chache zilizorekodi hazijaja na nyimbo zilizoweza kuteka umma wa wa
Tanzania na hivyo kusababisha muziki huu kukosekana katika anga za muziki.
Matangazo mengi ya muziki wa dansi yamekuwa ni kutangaza rap mpya au kupatikana
kwa msanii mpya, lakini kiujumla hakujakuwa na kitu kipya katika muziki wa
bendi.
Muziki asili pia umekosekana kwenye vyombo vya habari kwa
kuwa si vikundi vingi vya muziki huu vyenye uwezo wa kulipia gharama za studio
ambao muziki huu unastahili kurekodiwa. Studio nyingi zimejengwa kwa ajili ya muziki wa aina ya Bongoflava tu, zile studio za kuweza kuruhusu kundi la
muziki wa asili kurekodi gharama yake huwa ni kubwa sana.
Kundi la Makirikiri
lilitakiwa kuwa elimu tosha kwa wasanii wa muziki wa Kiasili, kuwa na muziki
huo ukifuata taratibu nzuri ya kurekodiwa unauza vizuri sana, bahati mbaya kuna vikundi sasa vimeacha
muziki na ngoma zao, vinaiga uchezaji wa
Makirikiri.
Pengine watu watasema nimesahau muziki wa kwaya, sijausahau,
kwa kweli muziki huu umebaki hasa
kwenye muziki wa Enjili. Hapo zamani ulikuwa ukitumika sana kwenye siasa na
kampeni , lakini kwa mwaka 2012 hali imekuwa mbaya kwa muziki huu.
Pamoja na kuwa wengine wangeweza kusema tunasonga mbele
katika muziki, kwangu mimi naona tunarudi nyuma kitaaluma. Tasnia inaingiza
pesa nyingi zaidi, na hata kuna wasanii walioingiza pesa nyingi sana, lakini kwangu hilo si kipimo cha maendeleo
katika tasnia hii.
Kama nilivyoanza kusema washika maikrofon wamekuwa ndio
alama ya muziki wa Tanzania. Muziki ni zaidi ya kuimba. Katika kuimba sauti nzuri
ya muimbaji ni muhimu, na ninashukuru kwa hilo tunao waimbaji wazuri wengi
sana, lakini ule muziki
unaomsindikiza muimbaji ni muhimu sana kwani ule hauna mipaka wala lugha, na
ndio unaoweza kutufungulia mlango wa soko la kimataifa. Wengi tunapenda sana
muziki wa kutoka Kongo, Nigeria, South Africa, pamoja na kuwa hatujui hata moja
wanaloliongelea tunaupenda muziki huo kutokana na mpangilio wa vyombo vyao.
Kutokujali wapigaji katika mfumo wa nchi yetu ndio unatupelekea kuwa watu wa
‘copy and paste’ wa upigaji wa muziki wa nchi nyingine. Ukiorodhesha nyimbo
zote zilizotikisa nchi hii kwa mwaka 2012 utagundua asilimia kubwa ya muziki
uliotumika ulikuwa ni wa kunakili kutoka muziki wa nchi nyingine, Nigeria,
Congo na Afrika Kusini ndio wamekuwa waalimu wetu wakuu. Ushauri kwa maproducer
wa Bongoflava, kuangalia pia muziki wetu wa asili humu ndani ya nchi ili tuje tumalize
2013 na kitu chetu ambacho Wanaigeria, Wakongo nao pia waige toka kwetu.
Inawezekana sana maana wimbo wa Weekend wa Afro70 uliwahi kuweko katika kumi bora 1972, Nigeria.
Muziki wa Enjili pamoja na kuwa ndio unaotegemewa
kutufundisha maadili, ulikuwa na kasoro moja kubwa nayo ni kukosa maadili kwa
kucopy na kupaste. Nyimbo nyingi zilizokuwa maarufu na kuteka hisia za maelfu
ya watu zilikuwa ni kuiga moja kwamoja kutoka Afrika ya kusini. Najiuliza je
ndio kilichopunguza moto wa muziki huu 2012? Kulikuwa hakuna za kukopi?
Wanamuziki wa Enjili kama ilivyo kwa ushauri kuhusu Bongoflava, ni muda wa
kurudi nyuma na kutumia raslimali ya utamaduni iliyoko kuleta mabadiliko na
kukuza soko la muziki huo.
Tasnia ya muuziki wa Tanzania katika tafiti moja wapo
umeitwa ‘the radio-driven
contemporary music industry’. Kwa maneno rahisi, tasnia ambayo imekuwa
inaendeshwa na radio. Radio zimekuwa na uwezo wa kumpandisha na kumshusha
mwanamuziki, kumtafutia soko, kumzibia soko na kadhalika. Hali hii
ikisindikizwa na rushwa ambayo imetapakaa katika jamii yetu, unapata picha kuwa
kungeweza kukawa na sura bora au tofauti ya muziki hali isingekuwa ilivyo. Kuna
ripoti za watu kutoa hongo nyimbo za wenzao zisipigwe, hongo ili nyimbo
zipigwe, visasi vya kuzuia nyimbo zisipigwe na kadhalika. Na katika jamii
ambayo imekuwa na kawaida ya kutegemea vyombo vya habari kujua muziki gani mpya
na mzuri, uwanja huu si uwanja ulio tambarare hata kidogo. Bahati mbaya inaonekana
wenye vyombo hivi wako mbali na ukweli unaoendelea katika vyombo vyao au kwa
kutokujua au kupuuza. Janga hili limevikumba hata vyombo ambavyo vinaendeshwa
na taasisi za dini. Wanamuziki wa muziki wa Enjili nao pia wanalia kudaiwa
rushwa na watangazaji wa radio za Enjili!. Nakumbuka siku niliyopata nafasi kuongea na kiongozi mmoja
wa dini ambaye Kanisa lake linaendesha kituo cha radio, nilipata mshangao baada
mkuu huyo, kuanza kutetea watangazaji wake badala ya kuamua kufanya uchunguzi
wa tuhuma.
Umefika muda wa
radio kuanza kujigawa kimuziki. Ni kichekesho mji kuwa na vituo vya radio 30 halafu vyote vinapiga aina hiyohiyo ya muziki, wakati kuna aina mbalimbali za watu. Ajabu ni
kuwa wenye radio wanajua kuwa katika nchi nyingine unaweza kukuta radio
iliyoamua kupiga aina fulani tu ya muziki, Jazz Radio, Country music Radio,
Classic Music Radio, lakini hilo limekuwa gumu kwao kutekeleza hapa. Kuwe na utofauti, Wasikilizaji tuko wa aina tofauti.
Vyombo vya
habari viijitahidi kupata wataalamu husika wa aina tofauti za muziki, muziki
unaviingizia vyombo hivyo mabilioni ya fedha, vyombo vya habari viupe heshima yake. Bila muziki hakuna
radio.
Magazeti
yamekuwa mstari wa mbele katika kutangaza aina mbalimbali za wasanii na sanaa.
Pamoja na hongera kwa kazi nzuri lakini bado kuna nafasi kubwa ipo tupu, hakuna wataalamu wa
uandishi wa habari za muziki. Hivyo habari nyingi za muziki zinaandikwa na
waandishi kama wapenzi wa muziki na si wataalam wa uandishi wa muziki, jambo
ambalo liko tofauti na uandishi wa michezo kwa mfano soka. Unaweza ukasoma
habari ya soka ambapo mwandish atakueleza nafasi za wachezaji, kama ni faulo,
ni nini kilisababisha, na kama ni goli lilikuwa ni la kichwa au kona au
penalty, hili haliko katika muziki. Utaambiwa tu bendi ilipagawisha, au msanii fulani ateka nyoyo za wapenzi, na
maelezo ya juu juu kama yale, kunahitajika kuanzishwa mafunzo ya elimu ya
uandishi wa kazi za sanaa. Hili litapunguza hata vurugu kama zilizotawala mwaka huu
ya wapiga picha kufikia hata kulala chini ili tu wapate picha ya nguo za ndani
za msanii na hayo ndio kuwa maelezo makuu ya onyesho zima la muziki.
Ikiwa kulikuwa
na mchango wa serikali katika muziki, basi ulikuwa mdogo au ulikuwa ni kwa
shughuli maalumu lakini si kwa kutengeneza mazingira ya kuwezesha unafuu kwa
wanamuziki kwa ujumla. Idara ya Utamaduni imeendelea kupata bajeti ndogo ambayo
imefanya Baraza La Sanaa La Taifa kuendelea kubaki Dar es Salaam tu,
likibangaiza kuweko kwa kutegemea kutoa vibali mbalimbali kwa wasanii, na nguvu
zake kuonekana Dar es Salaam tu. Na kwa kuwa hakuna Maafisa Utamaduni Mkoa, na
Maafisa Utamaduni Wilaya na Manispaa wako chini ya serikali za mitaa hivyo kuwa
wizara tofauti na Waziri wa Utamaduni, nguvu za serikali katika utamaduni ni 0. COSOTA chombo ambacho shughuli yake ilikuwa ni kulinda hakimiliki za wasanii na ambacho kilikuwa chini ya wasanii, kwa kinyemela kabisa kimerudishwa katika mikono ya serikali, lakini bado kinakusanya mirabaha 'kwa niaba ya wasanii' huku kukiwa na bodi isiyo na uwakilishi wa wasanii kuanzia 2007. Swali utakusanyaje pesa kwa iaba yangu lakini huniruhusu kujua ni kiasi gani umekusanya, unazitumiaje na ukiulizwa unakuwa mkali!!!!!!? Kuna wasanii wamekuwa wakidai kurudishiwa COSOTA, ushauri wangu wasanii wakae wajipange na kuelewa vizuri sheria ya Hakimiliki kabla ya kujitwishwa zigo hilo la miba.
Katika miezi 6
ya mwisho ya 2012 kumejitokeza spidi kali ya Mamlaka ya Ukusanyaji wa Mapato
kutengeneza mazingira ya kukusanya mapato kutokana na mauzo ya kazi za muziki
na filamu. Kimsingi kulipa kodi ni wajibu wa kila mwananchi na wasanii ni wananchi pia, lakini taratibu zake ndio zinanipa utata,
hasa pale ambapo kwa muda mrefu imekuwa ikitangazwa kuwa njia hii itasaidia
wasanii kwa kupunguza kuibiwa. Sentensi hii inaonyesha wazi anaeiongelea aidha hajui mfumo wa
biashara ya kazi muziki, au kwa makusudi anapotosha ili kuficha kitu. Wasanii wengi huwa wamekwishalipwa kwa kazi ambazo
zimesambaa na ziko barabarani zinaibiwa, wanaoibiwa ni wasambazaji. Hivyo kulinda kazi hizo
unamlinda msambazaji si msanii. Pia kuanza kukusanya kodi kwa kazi hizi
kumepewa jina ‘kurasmishwa kwa
kazi ya usanii’, kuna mabilioni wasanii wanatakiwa walipwe na watumiaji wa kazi
za sanaa, kama radio na TV, mapromota, waajiri na kadhalika hakuna anaeliongelea hilo wala hakuna anaetamka
takwimu hizo. Kuna kazi ya kurudisha mitaala ya masomo ya sanaa mashuleni,
kurudisha vyuo vya walimu wa sanaa, kurudisha maafisa utamaduni kuwa chini ya Wizara ya Utamaduni kuwawezesha kufanya kazi
zao kadri ya sera ya Utamaduni, na mengine mengi ya aina hiyo ndio ningeona kurasimisha
kazi za sanaa, lakini kukusanya kodi tu kwa kazi ambazo hata hivyo mikataba yake mingi
inautata na kuita urasimishaji si sahihi.
Katika nchi nyingi critics au watu ninaoweza kuwaita kiswahili wakosoaji, huwa ni muhimu katika maendeleo ya sanaa, watu hawa hupata heshima kutokana na kuweza kuangalia mapungufu katika kazi za sanaa na kuyasema, jambo ambalo hupelekea wasanii kujirekibisha na kutengeneza kazi bora zaidi. Hapa kwetu kutoa ushauri ni kutafuta matusi, toka kwa wasanii wenye kazi husika, vyombo vya habari na hata sehemu ya jamii, umefika muda wahusika kuchukua uchambuzi kama changa moto za kuboresha kazi.
Niliyoyataja
hapa yote yako wazi ninachotegemea ni kuona 2013, hatua zinaanza kupigwa
kurekibisha, ili wanamuziki wa nchi hii nao wapate nafasi sawa na wengine wa nchi nyingine.
John Kitime
31.12.2012
Sinza, Dar es Salaam
Comments