BONGOFLEVA NA BEAT ZA KINAIJERIA

-->
Katika siku za karibuni wanamuziki kadhaa wa Tanzania wamekuwa wakija na nyimbo mpya wakiiga ‘beat’ za kutoka Nijeria. Ningependa kuwapa taarifa fupi kuhusu 'beat' hizo. Katika nchi za Afrika Magharibi, hasa Ghana na Nigeria, kwa miaka mingi walikuwa na mtindo wao wa Highlife ambao vijana wa huko wameuendeleza na kuwa mtindo ambao unatamba sana Afrika, na si mara moja wamerudia nyimbo za zamani na kutikisa Afrika,  wimbo kama  Sawa saware ambao uliandikwa na Rex Lawson mzee wa Kinaijeria aliyefariki mwaka 1971, ni wimbo ambao mzee huyo alianza kuupiga miaka 50 iliyopita, umechukuliwa na vijana na kupewa umri mpya kwa kuuboresha bila kuuharibu, au ukiusikiliza wimbo Sweet Mother wa Prince Nico Mbarga ambao  ulitikisa Afrika kwa kufanya mauzo ya zaidi ya santuri  milioni 13, utakuta pia vijana wa Kinaijeria wamechukua utaalamu wa mapigo hayo na kuja na mtindo unaotikisa Afrika. Ushauri wangu ni kuwapa hamasa vijana wanamuziki wa Tanzania kuwa kuna ghala limejaa 'beat kali' katika historia ya muziki wa nchi hii pia, ukijumlisha na ‘beat’ za makabila zaidi ya 120 utaona kuwa bado kuna silaha kibao za kuweza kutumia ili kuingia katika mpambano wa kutafuta nafasi katika soko la muziki la kimataifa. Lazima hapa niwasifu wale vijana ambao wameligundua hili na tayari nimekwisha sikia nyimbo kadhaa zenye 'beat' za Kizaramo, safi sanaaa, pia nawashauri kaangalieni Sangula la Wapogolo mpate mambo mapya kule. Producers fanyeni homework ili kupata beat mpya za ubunifu wenu asili. Naambatanisha wimbo original wa Sawa saware muone kazi ilivyokuwa awali

Comments