TUPIGE VITA YA KWELI MADAWA YA KULEVYA


Usiku wa leo mawazo yangu yalilazimika kurudi nyuma miaka kadhaa wakati janga la Ukimwi linaingia nchini mwetu. Mawazo haya yamekuja kutokana na coments za watu baada ya mimi kuweka post kwenye Facebook ya kuomba wenye uwezo wamsaidie mzazi wa mwanamuziki mwenzangu katika matibabu ya mwanae. Ukimwi uliingia humu nchini na kupewa majina mengi, jina la zamani zaidi lilikuwa Juliana, kutokana na mashati yaliyokuwa yameandikwa jina hilo, na wakati huo hadithi ilikuwa ugonjwa huo unatokea ile kona ya Uganda, kulikuweko mpaka mawazo ya kudai mpaka na nchi hiyo ufungwe ili janga hilo lisije kwetu. Mabango barabarani, kwenye vyombo vya habari kauli mbiu ilikuwa ukimwi unaua. Hili liliongeza uwoga ambao matokeo yake yako mpaka leo hii ambapo kuna dawa mbalimbali za kupunguza makali ya ugonjwa huu. Wagonjwa wa ukimwi walikufa kwa mateso makubwa ya kudhalilisha na wengi walitupwa kama mzoga wa mnyama kwa uwoga kuwa hata kuwagusa kutasababisha maambukizi, yote haya kutokana na matibabu kutojulikana na pia kutokana na uelewa mdogo wa jamii kuhusu ugonjwa huu. Kila aliyeupata ugonjwa huu alionekana kaupata kwa kuwa alikuwa ‘malaya’ au si mwaminifu katika ndoa yake, familia ziliona mgonjwa anazitia aibu, marafiki pia walimkimbia mwenzao wasionekane kuwa walikuwa wanaelewana na mgonjwa, na pia watu waliogopa kumtunza mgonjwa kama huyu, hivyo mgonjwa alikuwa anakufa kisaikolojia kwa upweke, na pia kimwili kwa ugonjwa. Pamoja na hali hiyo ugonjwa uliendelea kutafuna Malaya na wasio Malaya. Taratibu watu walipopata uelewa kuhusu ugonjwa huu na kuanza kusaidia na kutokuwakimbia na kuwalaani wagonjwa wa Ukimwi.
Tatizo la ugonjwa utokanao na madawa ya kulevya nao uko katika hatua za kwanza hapa kwetu kiasi watu wengi hudhani mtu anajitakia tu ,akiamua tu kuacha anaweza akafanya hivyo, bahati mbaya madawa ya kulevya hubadili mfumo wa utendaji kazi wa ubongo.. ‘Drugs contain chemicals that tap into the brain’s communication system and disrupt the way nerve cells normally send, receive, and process information. There are at least two ways that drugs cause this disruption: (1) by imitating the brain’s natural chemical messengers and (2) by overstimulating the “reward circuit” of the brain.’ Hili hufanya kuacha kuwa kugumu hata pale mtumiaji anapotambua kuwa analazimika kuacha kutumia madawa hayo.
Hivyo mtumiaji ni mtu ambaye ni mgonjwa na anahitaji matibabu kama mgonjwa mwingine maana ubongo umeshachanganywa.Kwa bahati nzuri utafiti wa kisayansi umegundua njia ambazo madawa ya kulevya huudanganya ubongo ili kumfanya mtu awe tegemezi wa madawa haya. Na bahati mbaya tatizo la utumiaji wa madawa ya kulevya linakuwa kubwa taratibu nchini mwetu, ni muhimu tukaungana wote kuelimisha watoto wetu ndugu na jirani wasiingie kwenye mtego wa kuonja vitu hivi ambavyo utegemezi wake huharibu kabisa maisha ya mtu.
Wahenga walisha sema hujafa hujaumbika, tusilaani tusaidiane.

Comments