MUUMIN AONDOKA TWANGA KWA RAUNDI NYINGINE

Muimbaji wa siku nyingi, Muumin Mwinjuma 'Kocha wa Dunia' ameondoka katika bendi ambayo ameitumikia kwa kipindi cha karibuni, bendi ya African Stars-Twanga Pepeta. Muumin anaelekea kwenye bendi nyingine mpya ambayo haijulikani sana iitwayo Victoria band, ambako atakuwa na kazi ya kuinyanyua ifikie kiwango cha bendi alizokwisha pitia. Kupitia kwenye website ya www.saluti5.com Muumini alitoa maelezo mengi kuhusu kuhama kwake yakiwemo haya ....
“Kibinaadamu najua ziko sehemu kadhaa ambazo tulikwazana lakini sitapenda mazuri mengi niliyoyapata pale yafunikwe na mabaya machache, itakuwa ni ukosefu wa fadhila, naomba wote watakaoumizwa na kuhama kwangu wanisamehe na tulindiane heshima.
“Haitakuwa jambo jema mimi au Twanga Pepeta tukaanza kupita huku na kule na kuchafuana, bado naichukulia Twanga na Aset kwa ujumla kama nyumbani kwangu” alisema Muumin.
Alipoulizwa ni kwanini ameihama Twanga wakati aliahidi kumalizia muziki wake kundini hapo, Muumin alisema amezingatia vitu viwili.
Kwanza ni dau alilopewa Victoria Sound, pili ni uchanga wa bendi aliyojiunga nayo. “Naiona Victoria kama bendi changa ambayo haitaweza kuwa bendi shindani kwa Twanga Pepeta, kamwe nisingethubutu kujiunga na bendi yeyote shindani kwa Twanga” alisema Muumin aliyetunga wimbo Penzi la shemeji katika albam ya Dunia Daraja.
Aidha, Muumin aliongeza kuwa anaamini kuwa kuondoka kwake Twanga Pepeta hakutaacha pengo lolote kwa vile ina mkusanyiko wa wanamuziki wenye vipaji vya hali ya juu.
Muumin amesema changamoto aliyonayo sasa ni ya kutengeneza nyimbo nzuri kwa bendi yake mpya ili kuitoa katika hatua moja kwenda hatua nyingine.

Comments