HISTORIA YA MUZIKI- NA KWANINI MUZIKI WETU UPO ULIPO SASA? (1)



KABLA YA  MKOLONI
Kama ilivyokuwa kwa binadamu wengine, wakazi wa eneo ambalo hatimae limekuwa nchi yetu ya Tanzania, walikuwa na utamaduni wao. Utamaduni huu ulikuwa ukitofautiana kati ya kabila na kabila. Moja ya vipengele ilikuwa muziki. Kabla sijaendelea ni habari hii ni vizuri tukumbuke jambo moja, ikiwa kitu hakiko katika utamaduni wa kundi la watu, kitu hicho huwa hakina jina katika kundi lile. Nikiuliza unambie internet kwa kabila lako inaitwaje hutakuwa na jina hilo kwa kuwa hakuna kitu hicho katika utamaduni wa kabila lako. Hatukuwa na ‘muziki’ katika makabila yetu kabla ya ujio wa wageni, na hivyo hakuna kabila lenye tafsiri ya neno muziki. Lakini tuliimba, tulicheza ngoma, tulipiga vyombo mbalimbali, ila tulikuwa na utamaduni mwingine kuhusu kitu hiki tunachokiita siku hizi muziki. Watafiti wanatuambia tulikuwa na Ngoma, ambayo tafsiri yake ni kubwa kuliko muziki. Ngoma ilikuwa ni chombo kile kilichotoa muziki, ngoma ilikuwa shughuli yenyewe, kwa mfano ngoma ya mavuno, ngoma ya mashetani na kadhalika, na pia tulicheza ngoma.
 WAKATI WA MKOLONI
MJERUMANI
Wajerumani ndio waliotuletea neno muziki kutokana na neno lao ‘musik’, na katika wakati wao ndipo kuliingia muziki wa bendi za askari na kuingizwa katika shule ya kwanza ya serikali wakati huo, Tanga School. Katika kipindi hiki pia mchango wa madhehebu mbalimbali kuingiza muziki na vyombo vya muziki vipya ulitoa mchango katika kuongeza kasi ya huu muziki mpya. Pengine unaweza ikasema kuwa kipindi hiki kwaya nazo zilianza kushika kasi, hapa kama nilivyosema mwanzo neno kwaya pia ni jipya lililotokana na neno la Kiingereza choir. Historia intueleza kuwa Mjerumani hakufanya jitihada za kuzuia muziki wa kiasili, hivyo basi muziki mpya na wa kiasili ulienda sambamba
MUINGEREZA
Utawala wa Muingereza ulileta mabadiliko mengi katika muziki wan chi hii. Askari waliotoka vitani KAR maarufu kama askari kea walirudi na hadithi kuhusu muziki, vyombo vya muziki, na hata muziki walioukuta katika safari zao vitani, vyombo kama akodian na magitaa makavu(yasiyotumia umeme) yaliinhia wakati huu. Kutokana na  watu wa makabila mbalimbali kuchanganyika na miji kuanza kuzaliwa kukaanza kuweko na utamaduni mpya. Muziki uliyokuwa unakubalika kwa makabila yote ulianza, aina ya muziki maarufu kama Beni ilienea katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki. Waafrika waliokuwa wamesoma nao wakaanza kuwaiga wazungu hata kuanza kuteengeneza Club zao ambazo zilikuwa maarufu kama Dancing Clubs. Katika club hizi kulipigwa nyimbo mbalimbali kwa kutumia santuri na  wapenzi kucheza muziki katika staili mbalimbali kama vile Cha cha, Tango, Foxtrot, swing, waltz nakadhalika. Inasemekana club ya kwanza Tanzanyika ilianza Tanga, ikiitwa Young Noverty Dancing Club, na baadae Dar es Salaam ikawa na Young Generation Dancing Club. Club hizi zilikuwa ndio chanzo cha bendi za kwanza Dar es Salaam Social Orchestra ambayo baadae ilikuja kuwa bendi maarufu Dar es Salaam Jazz Band, na pia kulikuweko na YMCA Social Orchestra, wakati huu ilikuwa katika kipindi cha kati ya 1920 na 1935. Baada ya vita ya pili ya dunia 1945, Wamarekani waliweka radio yenye nguvu katika mji unaoitwa sasa Kinshasa, redio hii iliweza kusikika sehemu nyingi, Afrika mashariki Kati na Magharibi, na kuanza kwa lebo maarufu ya Loningisa nchini Kongo mwaka 1947 ilianzisha kusikika na kuigwa kwa muziki wa Kikongo kuanzia wakati huo. Lebo ya Galotone ya Afrika Kusini pia ilisambaza santuri ambazo ziliingiza style za Jive katika nchi hii, kwa miaka mingi vijana walikuwa na vikundi wakicheza jive, na bendi kadhaa ziliiga upigaji wa jive ukiambatana na upigaji wa filimbi kumuiga mwanamuziki Spokes Mashiyane. Magitaa ya umeme kwa bendi za muziki wa dansi yalianza kutumiwa kati ya mwaka 1957 na 1959, Dar Jazz tena hutajwa kama bendi ya kwanza ya muziki wa dansi kuanza kutumia gitaa hilo, ikifuatiwa na Western Jazz na bendi nyinginezo.  Kwenye mwaka 1954 Kenya ikaanza kuwa kituo kikubwa cha kurekodi muziki, na kwa miaka mingi iliyofuata bendi za Afrika Mashariki zililazimika kwenda Kenya ili kutoa santuri. Kuna wanamuziki wengine mpaka leo hufikiriwa ni Wakenya au nyimbo zao kudhaniwa kuwa zilitoka Kenya kwa mfano Frank Humplink na dada Zake ambao walitoa vibao ambavyo bado vinasikika katika anga za muziki hadi leo, Embe Dodo, Tufurahi Harusi nakadhalika.

BAADA YA UHURU MIAKA YA 60/70
Pamoja na mapungufu yanayotajwa ya utawala wa chama kimoja, kulikuweko na mambo yaliyowezekana kutokana na hali ya chama kimoja kuwa na dira inayoeleweka na hivyo kuelekeza kila kitu kadri ya matakwa ya chama. Sanaa ya Tanzania haikukwepa mwongozo wa TANU, sehemu za kazi , vijiji , miji  viliagizwa kuwa na vikundi vya ‘utamaduni’ ambavyo vingekuwa ndio vikundi vya burudani baada ya kazi na pia jukwaa la kuelezea mipango na malengo ya chama na serikali. Zikatengenezwa bendi za majeshi, polisi, JWTZ, Magereza, Uhamiaji, mashirika ya umma nayo hayakuwa nyuma, BIMA, TANCUT, DDC Mlimani, UDA  na miji nayo ikawa na bendi  Kurugenzi Arusha Kurugenzi Dodoma. Na ni ukweli usiopingika nyimbo nyingi maarufu kama zilipendwa zilipatikana katika kipindi hiki.
Bendi zilitunga nyimbo, ambazo zilipitia katika kamati iliyozipitia kabla ya kuruhusiwa kurekodiwa na kurushwa hewani. Kwa upande wake serikali nayo ikatengeza idhaa tatu katika redi ya taifa, External Service, iliyokuwa ikitangaza kwa lugha ya Kiingereza na lugha ya nchi za kusini zilizokuwa zikipigania uhuru wakati huo, kukaweko na Idhaa ya Biashara ambayo ilikuwa na vipindi vikitangaza biashara mbalimbali vilivyodhaminiwa na wafanya biashara, katika idhaa hii, uliweza kusikia muziki kutoka popote duniani, lakini kwa makusudi kabisa kukaweko na idhaa ya Taifa ambako huku ungesikia kila aina ya muziki wanchi hii, pamoja na kuwa kwa sasa kuna vituo vya radio zaidi ya 80 vimeshindwa kufanya kazi hii iliyoweza kufanywa na kituo kimoja cha Taifa, bahati mbaya kituo hicho cha Taifa kimeshapoteza muelekeo wake huu uliokuweko awali.

Comments