CHIKU KETO MDADA MWINGINE KATIKA HIP HOP TANZANIA





 Chiku Keto si jina geni sana katika anaga za muziki wa Bongofleva, alianza kujulikana zaidi hasa baada ya kuingia katika mpambano wa BSS na kutolewa kasha kurudishwa na baadae kukosa kura za kutosha na kutoka tena jambo ambalo mpaka leo mwenyewe anasema lilimuuma sana maana aliona kama kiini macho fulani. Chiku alizaliwa miaka kadhaa iliyopita katika hospitali ya Ocean Road tarehe 18 Aprili. Baba yake alikuwa Afisa Elimu kwa hiyo alikuwa katika maisha ya kuhama akifuatana na baba yake kila alipohamishwa. Hili lilisababishwa asome shule za msingi morogoro na Lindi. Alipata elimu ya sekondari katika shule ya Sekondari ya Mkonge huko Lindi, na baada ya hapo kurudi Dar es Salaam ambapo wazazi wake walirudi kuishi baada ya baba yake kustaafu. Baada ya kumaliza masomo ya sekondari alijiunga na chuo cha Uandishi cha Royal School of Journalism kilichopo Ubungo, baada ya kupata cheti, akajiunga na VETA na kufanya kozi ya ufundi wa magari kwa mwaka mmoja ambapo pia alipata Certificate ya utaalamu huo. Mzuka wa muziki ulikuwa taratibu umeshamuingia kwani 2005 aligonga hodi Baucha Records na kurekodi kibao kilichoitwa ‘Fungua Mlango’, ambacho pamoja na kukisambaza kwenye radio kadhaa, hakikupigwa kamwe. Mwaka 2006 akajitosa katika mashindano ya BSS, ambapo alifanya vyema na kuweza kuingia katika top ten ya washiriki, lakini akatolewa, na kwa mapendekezo ya ‘Chief Judge’ aliweza kurudi kwenye kinyang’anyiro lakini akatolewa tena kutokana na kutokuwa na kura za kutosha. Aliomba msaada wa uongozi wa Benchmark kwenda kurekodi wimbo ka thamani ya shilingi laki mbili katika studio za Double B, nyimbo hiyo pia haikuweza kutoka. Hatimae akajisogeza Dhahabu Records ya Dully Sykes ambapo aliweza kurekodi nyimbo kadhaa lakini hazikujulikana kutokana na kukosa mtu wa kuzisimamia katika promotion na kadhalika. Alihama hapo na kujiunga na kundi lililokuwa likiendeshwa na Chidi Benz. Aliweza kuzunguka sehemu nyingi za nchi na nje ya nchi kama supporting artist wa Chidi Benz, na katika kundi hili alilokaa miaka minne aliweza kushiriki nyimbo kadhaa zikiwemo ‘Muda umefika na Why. Aliliacha kundi hili na sasa yuko kundi la ARM Entertainment ambapo amekwisha rekodi wimbo wa Natafuta na Mzuka. Chiku amekwisha fanya kazi pia na mwanamuziki Lady Bee kutoka Kenya, mwanamuziki huyo kwa sasa amebadili muelekeo na anajihusisha na muziki wa Gospel…Chiku Keto bado yuko safarini

Comments