HUU NI MUZIKI AU KUNA KITU KINGINE?

Baada ya kipindi kirefu ambapo zimekuwa zikienea picha za wasanii wa kike wakiwa nusu watupu jukwaani, sasa picha ambazo zinadaiwa ni za wasanii wa kiume wakijitahidi tena kwa makusudi kuwaiga dada zao zimeanza kuibuka. Ni ngumu kuelezea nini huwa kinapita katika vichwa vya wasanii kama hawa kwani kilichowapelekea kutunga staili kama hii juu pichani wanakijua wao tu. Lakini ni ukweli usiopingika kuwa haya ni matokeo ya malezi.  Kuna malezi ya wazazi na baadae malezi ya jamii. Ni wazi kuna tatizo kubwa katika malezi aidha kutoka kwa wazazi au kutoka kwa jamii.
Kuna wanamuziki wawili ambao waliwahi kurekodi nyimbo ambazo mashahiri yake yalikuwa na 'matusi' ndani yake. Mmoja wa wasanii hao alisaidiwa na MAMA YAKE MZAZI kutunga mashahiri hayo, kwa tuliye kuwa tukiifahamu historia ya mama yake hatukushangazwa na habari ile, kwani alikuwa akishinda baa toka mchana na mwanae huyo wakati mdogo. Mwingine alitunga wimbo wa matusi ambao hata kusambazwa ilishindikana lakini kuna taarifa kuwa MAMA YAKE MZAZI alikuwa mmoja wa wasikilizaji waliokuwa wakichekelea matusi makubwa yaliyokuwemo katika wimbo huo. Hapa utaona tatizo linaanzia nyumbani tena kwa wazazi.
Juzi juzi nilisoma habari ambapo msanii mmoja alisema, na si mara ya kwanza kumsikia akisema hivyo, kuwa wazazi wake hawakubaliani na jinsi anavyovaa jukwaani, lakini akiwa jukwaani kwa jamii anavaa 'nusu nguo'.  Namkumbusha usemi wa zamani,'Asiyesikia la mkuu huvunjika guu'
Jamii yoyote inajukumu la kulinda maadili yake, hakuna mtu atatoka nje kusaidia kwa hilo kama ilivyo jamii ikiingiliwa na gonjwa la UKIMWI, hapo utapata msaada toka nje maana unageuka tishio kwa jamii nyingine.
Pamoja na kuwa na Wizara kadhaa, Vyama Vya Kiharakati kadhaa, Dini mbalimbali, hakuna anaeonekana kutaka kugusia swala hili, sijui pengine kwa kuogopa kuonekana 'mshamba' au mbaya. Vyombo vya habari viko kimya, kukemea japo viko mbele kueneza tatizo.
Sababu nyingine kubwa ya hali hii ni kuwa dhamana ya utamaduni na maadili ya nchi hii wameachiwa wafanya biashara, ambao kwao fedha ndio 'main agenda', na huwezi kuwalaumu kwa hilo, wanaingiza mabilioni ya fedha katika shughuli zinazoweka mazingira ya uvunjwaji wa maadili, na hasa pale ambapo, biashara zinaendeshwa na makampuni toka nje, hivyo kilichofanyika South Africa kinaonekana ni 'haki' kifanyike Tanzania kwa gharama yoyote mradi kiwe kinaongeza faida, lakini Je, Wizara zetu zinafanya nini kwa niaba ya jamii?  Kwanini basi kuwe na Wizara ya Utamaduni, au Wizara ya Akina mama na watoto, au ya Vijana?
Swali kwa wasanii wanamuziki, Je unapopanda jukwaani unaenda kuuza nini? MUZIKI au SURA?.... Hivi wanamuziki maarufu nchini....akina Rose Mhando, Bahati Bukuku, Khadija Kopa na wengi sana wengine, mbona ni maarufu na wanapata upenzi mkubwa na wanauza kazi zao nyingi bila kulazimika kukaa uchi hadharani? Sasa hili la mwanaume unapofikia kuvua nguo na kuelekeza makalio kwa wanaokuangalia kunaweza kuwa ni kwa sababu kadhaa nje kabisa na shughuli ya muziki, aidha unawanga, au unatoa matangazo ya kazi yako mpya!!!! lakini ni wazi kumetokea tatizo kuwa muziki unaofanya umeshauona umeanza kukosa upenzi unaanza kufanya kazi za kutangaza biashara ya ziada.

Comments