Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) limewaagiza viongozi wa Mashirikisho ya
sanaa hapa nchini kufuatilia kwa karibu matukio ya ukiukwaji wa maadili
yanayoendelea katika Sanaa hivi sasa na kuchukua hatua kwa wanaobainika
kufanya hivyo. Mbali na BASATA kuwakemea vikali
wasanii wanaotumia majukwaa kwa kuidhalilisha Sanaa wao wenyewe na
watazamaji pia limeyataka mshirikisho kushirikiana na vyama vyao kuwaita
wale wote watakaohusika na uvunjwaji wa maadili ili kuwakanya katika
hatua ya kwanza na kama wasipoacha tabia hizo Baraza litawafungia
kujishughulisha na kazi ya Sanaa hapa nchini.
“Shirikisho la Muziki limeagizwa kuangalia tungo za wanamuziki zenye
maneno yenye lugha isiyofaa, Shirikisho la Sanaa za Ufundi limeagizwa
kuwachukulia hatua wasanii wachoraji na wachongaji wanaotengeneza Sanaa
zinazokiuka maadili. Aidha Shirikisho la Sanaa za Maonyesho wameagizwa
kufuatilia wasanii wote wanaocheza bila staha majukwaani. Na mwisho Shirikisho la Filamu limeagizwa kuwaita, kuwaonya na
kuwachukulia hatua wasanii wote katika fani ya Filamu wanaovaa nusu
utupu bila kuzingatia husika katika kazi za Sanaa,” Aidha Baraza limewaagiza wamiliki wa kumbi zote za burudani kuzingatia
maadili pale ambapo Sanaa zitakuwepo jukwaani na kwamba baraza
halitasita kuufungia ukumbi wowote utakaokiuka agizo hilo. Pia vyombo vya usalama vimeombwa kuhakiki muda wa vibali vya
maonyesho na bila kuchelewa kuwachukulia hatua stahiki wasiozingatia
muda wa maonyesho. Na wamiliki wa vyombo vya Habari na
Wahariri wamekumbushwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wasimamizi wa sanaa kwa
kutokurusha wala kutangaza maonyesho ambayo kwa njia yoyote yanachangia
mmomonyoko wa maadili ya Taifa letu. Kwa
suala hili, Baraza linaziomba mamlaka zinazohusika na usimamizi wa
uendeshaji wa vyombo vya habari nchini kuingilia kati na kuvichukulia
hatua vyombo vya habari ambavyo kila siku vimekuwa mstari wa mbele
kueneza wimbi la mmomonyoko wa maadili hapa nchini na kushusha hadhi ya
Tasnia/Sekta ya Sanaa nchini. Sanaa ni kazi na Sanaa ni kioo cha
Jamii.
Comments