RUSHWA KATIKA TASNIA YA SANAA-1


Nilibahatika kuongoza semina ya wasanii mbalimbali kutoka wilaya ya Ilala, ulikuwa ni mkusanyiko wa wasanii wakiwemo, wasanii wa filamu, ngoma, muziki wa dansi, wachoraji wachongaji na kadhalika. Hii ni  moja ya semina nyingi ambazo zimetayarishwa na Chama cha Sanaa za Maonesho Tanzania(CHASAMATA). Katika semina hii mada ilikuwa Athari za rushwa katika tasnia ya Sanaa. Nilianza kwa kueleza uelewa wangu katika swala hili, ambapo pamoja na mengine nilielezea historia ya  rushwa niliyokuwa naifahamu katika tasnia hii ambayo kwa kweli imeanza miaka mingi sana. Baadhi ya mambo yaliyoleta rushwa katika historia ya sanaa, ni mlolongo wa vibali kabla ya kila onyesho. Wakati wa enzi ya chama kimoja, ilikuwa ni makosa kufanya onyesho bila kibali kutoka kwa afisa utamaduni, hata kikundi kikitaka kutoka nje ya mkoa kilihitaji kuomba kibali cha kutoka nje ya mkoa kutoka kwa afisa utamaduni mkoa ambaye alitoa kibali hicho ambacho kiliwasilishwa kwa afisa utamaduni wa mkoa unaokwenda ambae nae alitoa kibali cha kukuruhusu kuingia mkoa wake na kuwaachia maafisa utamaduni wilaya watoe vibali vya kuruhusu kufanya kazi kwenye wilaya zao, huu ulikuwa uwanja mzuri kwa kuombwa rushwa ili uweze kuruhusiwa kufanya kazi zako. Sehemu nyingine iliyokuwa na rushwa ni redio, ambayo hapo awali ilikuwa moja tu RTD, ambayo pia ilikuwa na studio pekee ya kurekodi muziki kwa muda mrefu. Rushwa ilianza pale ambapo ililazimika kupeleka mashahiri ya tungo za muziki kabla haujarekodiwa, kamati iliyokuwepo wakati huo, iliweza kukataa au kukubali wimbo urekodiwe kwenye studio zake baada ya kusoma mashahiri hayo,bila kulazimika kutoa maelezo kuhusu uamuzi huo, hivyo bendi nyingi zilidaiwa kitu kidogo ili kuhakikisha nyimbo ambazo zimefika kwenye kamati hiyo zote zinapita zilivyo, ngazi nyingine ya rushwa ilikuwa inakuja katika kuwapa motisha watangazaji husika kupiga nyimbo katika vipindi vyao, aina ya rushwa ambayo iko mpaka leo. Watangazaji wamedaiwa kuomba fedha, vocha za simu, rushwa ya ngono, na hata wengine kutaka vikundi kutoka mikoani kuwaletea mchele, mbuzi nakadhalika.
Rushwa nyingine ilikuwa inatolewa kwa viongozi wa serikali katika kupata kibali cha vikundi kutoka nje ya nchi, kwani taratibu zilikuwa wazi kuwa kikundi hakiwezi kutoka nje ya nchi mpaka Mkurugenzi wa Utamaduni atakapopitisha kibali hicho, Mkurugenzi mmoja ametajwa kuwa alikuwa maarufu kwa kulazimisha kipengele cha kuambatana na kikundi kwenye safari za nje, na kama hakukuwa na uwezekano huo pesa ilikuwa lazima itolewe au la hakuna kibali, wasanii wengi walikosa kwenda nje au wengine waliamua kuchukua sheria mkononi na kusafiri kwa njia za panya. Tatizo hili limedhihirika kuwa bado liko baada msani mmoja kutoa mfano wa Afisa wa Wizara ya Utamaduni, kugoma kusoma na kupitisha ripoti moja ambayo ingefungua mlango wa vikundi hata 40 vya ngoma za kiasili kupata nafasi kuzuru Uchina, na kudai msanii atafute shilingi milioni moja kwa ajili ya kikao cha kuchambua ripoti hiyo, ambayo kwa sasa imerudi kwenye makabati, na hakuna wasanii waliopata nafasi ya kutumia nafasi hiyo adimu.
Pia imedhihirika kuwa bado kuna Maafisa Utamaduni wanapenda rushwa kiasi cha kuwezesha vikundi kushinda katika mashindano mbalimbali kwa makubaliano ya kugawana zawadi. Ilitolewa mifano ambapo Afisa mmoja alidai khanga 5 kati ya 20 zilizotolewa kama zawadi kwa kikundi alichokisaidia kushinda na pia alidai kupewa wheelbarrow ambayo kikundi kilishinda katika mashindano mengine.
 Katika kuchangia mada, jambo ambalo lilikuwa wazi ni kuwa rushwa ya ngono kwa wasanii wa kike ni adha wanayoipata kila mara. Katika tasnia ya filamu na michezo ya jukwaani, viongozi wa vikundi, waongozaji wa filamu, producers ndio waliotajwa kuongoza katika kuomba rushwa ya aina hiyo, na wanawake wote huombwa rushwa hiyo bila kujali umri, jambo ambalo lilimfanya mama moja mtu mzima atokwe na machozi pale alipoombwa rushwa hiyo na mvulana ambae alimuona kama mwanawe. Vikundi vidogovidogo vya mtaani vimekithiri kwa aina hii ya rushwa na hasa katika maeneo yanajulikana kama kambi au location za filamu, na mara nyingi kwa hadithi za uongo kuwa wataweza kupata kazi katika filamu kubwa. Kwa upande wa wanamuziki wa kike adha yao huanzia na producers, kisha watangazaji, na hata wafadhili wa kazi zao kiasi cha mtangazaji maarufu kudai aliamua kuachana na fani ya muziki kwa ajili ya adha hiyo. Wiki ijayo wasanii wa Kinondoni watakuwa kwenye semina ya aina hiyo hatimae Temeke, na ndipo yatatolewa mapendekezo ya jumla ya hatua za kuchukua kuondoa adha hii.

Comments