KUSAMBAA KWA MATUKIO YA KUKAA NUSU UTUPU HADHARANI-MTIZAMO WANGU

Katiki kipindi cha miaka michache iliyopita taratibu kumeingia mdudu katika tasnia nzima ya sanaa ya kuona kuwa msanii wa kike kuwa nusu mtupu ndio maendeleo, na pengine hiyo ndiyo dalili ya mafanikio. Mtizamo huu ambao vyombo vya habari haviwezi kukwepa kuwa ndio vimekuwa mstari wa mbele kuusambaza, japo vyombo hivyohivyo kwa njia ya ajabu sana vimekuwa pia mstari wa mbele kulaani. Utaratibu huu ulianza polepole ukiwa umepambwa na maelezo kuwa hiyo ni njia ya kurekibisha tabia, au mara nyingine kwa kisingizio cha 'kuonyesha majuu walivyochanganyikiwa',  picha za mnato na  video zimeweza kutafutwa kwa udi na uvumba na hata kwa matangazo ya hadharani ya kuahidi fedha nyingi kwa vitu hivyo,na baada ya hapo kupenyezwa kwenye vyombo vya utangazaji mpaka watoto wadogo wanaweza kupata taarifa hizo bila hata kuhangaika. Video za muziki za wasanii maarufu duniani zimekuwa zikirushwa bila hata kuangalia maadili yaliyomo humo yanaendana na hadhi ya nchi yetu? Naweza kusema kwa sasa polepole inakuwa ngumu hata kwa watoto kukwepa kupata picha, video na taarifa hizo hata kama utamfungia mtoto ndani, TV itamletea au mazungumzo mazito ya vipindi vinavyoendelea siku hizi katika radi nyingi kati ya saa 3 asubuhi na saa 7 mchana. Bila hata kuweko na chembe ya staha hali hii imekuwa kubwa kwa kisingizio kikubwa cha uhuru wa kutoa habari.
Sasa imefika hatua ya wasanii wengine wanaamini kuwa jamii haina tatizo na jambo hilo kiasi cha mtu kukaa utupu katika jukwaa wakati akiangaliwa na maelfu ya watu, na kwa vile teknolojia imekuwa, kiukweli ni kukaa utupu kwenye macho ya ulimwengu mzima!!!!!. Imefika wakati, tena kwa kweli wakati umepita, ni lazima kufungua mdomo na kusema kuwa sasa imezidi. Hata nchi ambazo tunaziiga, huwa zina staha zake kutokana na mila za huko. Picha hizi za utupu zisiwe zinapatikana kiholela hivi, kama ni vipindi vya TV basi zichambuliwe zile picha za wakubwa zihamishiwe vipindi vya usiku wakati watoto wamelala, magazeti yenye picha za aina hii yatafutiwe njia za kuratibu kuwa wanunuzi ni watu wazima tu, kama inavyojaribu kufanywa kwa pombe na sigara  na ikiwezekana picha nzito siyo zinakuwa ukurasa wa mbele ambapo hata watoto wanaona mara moja. Jambo la ajabu ni pale unapopiga picha saa tisa ya usiku kisha unaweka katika gazeti unauza asubuhi na kudai unamrekibisha mtu tabia, kiukweli unasambaza tu yale yaliyokuwa siri usiku na kuyaweka hadharani hata kwa watoto.
Kwa ndugu zangu wasanii ambao pengine mna 'role' models wenu ambao mnawaiga kwa kila kitu, kumbukeni kuwa utamaduni wetu na wao bado ni tofauti sana, teknolojia inatufanya tujione kama tuko sawa, hatuko sawa. Athari za vitendo vyenu mtakuja kuviona pale mtakapozinduka na kujikuta nanyi ni binadamu kama wengine, umaarufu ni njia tu inapita. Hivi inakuwaje umeshazeeka halafu mjukuu wako anakuja na picha yako uliyopiga wakati ukijiona huji kuzeeka. Au umeshamua kubadilika unataka kujenga familia yenye staha lakini picha zako zinakusuta kila mara?
WATANZANIA WOTE KWA UJUMLA WETU TUZINDUKE TUNAKOKWENDA SI KUZURI. WAZAZI, WAALIMU, MAJIRANI, VIONGOZI WA DINI, VIONGOZI WA SIASA, VYOMBO VYA HABARI NA WOTE KWA UJUMLA TUJITAMBUE KUWA SISI NI WATANZANIA KWANZA

Comments

husseinchuse said…
kweli inabidi tuzinduke maana ishakuwa kero