Historia fupi ya muziki wa Tanzania
Kama ilivyokuwa kwa binadamu wengine, wakazi wa eneo ambalo
hatimae limekuwa nchi yetu ya Tanzania, walikuwa na utamaduni wao. Utamaduni
huu ulikuwa ukitofautiana kati ya kabila na kabila. Moja ya vipengele ilikuwa
muziki. Kabla sijaendelea ni habari hii ni vizuri tukumbuke jambo moja, ikiwa
kitu hakiko katika utamaduni wa kundi la watu, kitu hicho huwa hakina jina
katika kundi lile. Nikiuliza unambie internet kwa kabila lako inaitwaje
hutakuwa na jina hilo kwa kuwa hakuna kitu hicho katika utamaduni wa kabila
lako. Hatukuwa na ‘muziki’ katika makabila yetu kabla ya ujio wa wageni, na
hivyo hakuna kabila lenye tafsiri ya neno muziki. Lakini tuliimba, tulicheza
ngoma, tulipiga vyombo mbalimbali, ila tulikuwa na utamaduni mwingine kuhusu
kitu hiki tunachokiita siku hizi muziki. Watafiti wanatuambia tulikuwa na
Ngoma, ambayo tafsiri yake ni kubwa kuliko muziki. Ngoma ilikuwa ni chombo kile
kilichotoa muziki, ngoma ilikuwa shughuli yenyewe, kwa mfano ngoma ya mavuno,
ngoma ya mashetani na kadhalika, na pia tulicheza ngoma. Sina taarifa ya
maandiko yenye kina kuhusu hali ya ngoma katika kipindi hicho lakini tunajua watu waliimba na kucheza ngoma
kwa matukio mbalimbali, hali ambayo inaendelea mpaka leo.
WAKATI WA MKOLONI
MJERUMANI
Wajerumani ndio waliotuletea neno muziki, na katika wakati
wao ndipo kuliingia muziki wa bendi za askari na kuingizwa katika shule ya
kwanza ya serikali wakati huo, Tanga School. Katika kipindi hiki pia mchango wa
madhehebu mbalimbali kuingiza muziki na vyombo vya muziki vipya ulitoa mchango
katika kuongeza kasi ya huu muziki mpya. Pengine unaweza ikasema kuwa kipindi
hiki kwaya nazo zilianza kushika kasi, hapa kama nilivyosema mwanzo neno kwaya
pia ni jipya lililotokana na neno la Kiingereza choir. Historia intueleza kuwa
Mjerumani hakufanya jitihada za kuzuia muziki wa kiasili, hivyo basi muziki
mpya na wa kiasili ulienda sambamba
MUINGEREZA
Utawala wa Muingereza ulileta mabadiliko mengi katika muziki
wan chi hii. Askari waliotoka vitani KAR maarufu kama askari kea walirudi na
hadithi kuhusu muziki, vyombo vya muziki, na hata muziki walioukuta katika
safari zao vitani, vyombo kama akodian na magitaa makavu(yasiyotumia umeme)
yaliinhia wakati huu. Kutokana na
watu wa makabila mbalimbali kuchanganyika na miji kuanza kuzaliwa
kukaanza kuweko na utamaduni mpya. Muziki uliyokuwa unakubalika kwa makabila
yote ulianza, aina ya muziki maarufu kama Beni ilienea katika ukanda mzima wa
Afrika Mashariki. Waafrika waliokuwa wamesoma nao wakaanza kuwaiga wazungu hata
kuanza kuteengeneza Club zao ambazo zilikuwa maarufu kama Dancing Clubs. Katika
club hizi kulipigwa nyimbo mbalimbali kwa kutumia santuri na wapenzi kucheza muziki katika staili
mbalimbali kama vile Cha cha, Tango, Foxtrot, swing, waltz nakadhalika.
Inasemekana club ya kwanza Tanzanyika ilianza Tanga, ikiitwa Young Noverty
Dancing Club, na baadae Dar es Salaam ikawa na Young Generation Dancing Club.
Club hizi zilikuwa ndio chanzo cha bendi za kwanza Dar es Salaam Social
Orchestra ambayo baadae ilikuja kuwa bendi maarufu Dar es Salaam Jazz Band, na
pia kulikuweko na YMCA Social Orchestra, wakati huu ilikuwa katika kipindi cha
kati ya 1920 na 1935. Baada ya vita ya pili ya dunia 1945, Wamarekani waliweka
radio yenye nguvu katika mji unaoitwa sasa Kinshasa, redio hii iliweza kusikika
sehemu nyingi, Afrika mashariki Kati na Magharibi, na kuanza kwa lebo maarufu
ya Loningisa nchini Kongo mwaka 1947 ilianzisha kusikika na kuigwa kwa muziki
wa Kikongo kuanzia wakati huo. Lebo ya Galotone ya Afrika Kusini pia ilisambaza
santuri ambazo ziliingiza style za Jive katika nchi hii, kwa miaka mingi vijana
walikuwa na vikundi wakicheza jive, na bendi kadhaa ziliiga upigaji wa jive
ukiambatana na upigaji wa filimbi kumuiga mwanamuziki Spokes Mashiyane. Magitaa
ya umeme kwa bendi za muziki wa dansi yalianza kutumiwa kati ya mwaka 1957 na
1959, Dar Jazz tena hutajwa kama bendi ya kwanza ya muziki wa dansi kuanza
kutumia gitaa hilo, ikifuatiwa na Western Jazz na bendi nyinginezo. Kwenye mwaka 1954 Kenya ikaanza kuwa
kituo kikubwa cha kurekodi muziki, na kwa miaka mingi iliyofuata bendi za
Afrika Mashariki zililazimika kwenda Kenya ili kutoa santuri. Kuna wanamuziki
wengine mpaka leo hufikiriwa ni Wakenya au nyimbo zao kudhaniwa kuwa zilitoka
Kenya kwa mfano Frank Humplink na dada Zake ambao walitoa vibao ambavyo bado
vinasikika katika anga za muziki hadi leo, Embe Dodo, Tufurahi Harusi
nakadhalika.
BAADA YA UHURU MIAKA YA 60/70
Pamoja na mapungufu yanayotajwa ya utawala wa chama kimoja,
kulikuweko na mambo yaliyowezekana kutokana na hali ya chama kimoja kuwa na
dira inayoeleweka na hivyo kuelekeza kila kitu kadri ya matakwa ya chama. Sanaa
ya Tanzania haikukwepa mwongozo wa TANU, sehemu za kazi , vijiji , miji viliagizwa kuwa na vikundi vya
‘utamaduni’ ambavyo vingekuwa ndio vikundi vya burudani baada ya kazi na pia
jukwaa la kuelezea mipango na malengo ya chama na serikali. Zikatengenezwa
bendi za majeshi, polisi, JWTZ, Magereza, Uhamiaji, mashirika ya umma nayo
hayakuwa nyuma, BIMA, TANCUT, DDC Mlimani, UDA na miji nayo ikawa na bendi Kurugenzi Arusha Kurugenzi Dodoma. Na ni ukweli usiopingika
nyimbo nyingi maarufu kama zilipendwa zilipatikana katika kipindi hiki.
Bendi zilitunga nyimbo, ambazo zilipitia katika kamati
iliyozipitia kabla ya kuruhusiwa kurekodiwa na kurushwa hewani. Kwa upande wake
serikali nayo ikatengeza idhaa tatu katika redi ya taifa, External Service,
iliyokuwa ikitangaza kwa lugha ya Kiingereza na lugha ya nchi za kusini
zilizokuwa zikipigania uhuru wakati huo, kukaweko na Idhaa ya Biashara ambayo
ilikuwa na vipindi vikitangaza biashara mbalimbali vilivyodhaminiwa na wafanya
biashara, katika idhaa hii, uliweza kusikia muziki kutoka popote duniani,
lakini kwa makusudi kabisa kukaweko na idhaa ya Taifa ambako huku ungesikia
kila aina ya muziki wanchi hii, pamoja na kuwa kwa sasa kuna vituo vya radio
zaidi ya 80 vimeshindwa kufanya kazi hii iliyoweza kufanywa na kituo kimoja cha
Taifa, bahati mbaya kituo hicho cha Taifa kimeshapoteza muelekeo wake huu
uliokuweko awali.
Katika miaka ya mwanzoni ya 60, bendi ziliingia katika utamaduni wa kunakili nyimbo kutoka Kongo, kilichofanyika ni kuimba Kiswahili tu, kuna nyimbo kama Napenda nipate lau nafasi, Mtoto wacha kupiga mayowe na nyingi sana ambazo zilikuwa ni za kunakili moja kwa moja nyimbo za Kongo. Hali ilifikia kuwa mbaya mpaka bendi nyingine ziliingilia kati na kutunga nyimbo za kuwaasa wenzao watunge nyimbo zao....Koma koma koma kaka wewe tunga zako.. ilikuwa baadhi ya maneno ya kuwafanya wanamuziki waliokuwa wakiiga waache kuiga. Lakini pamoja na haya kulikuweko na wanamuziki waliokuwa wakiangalia na kuiga nyayo kutoka nchi za magharibi na baadae wakichanganya vyombo na melody za kiasili na kuanza muziki uliojulikana kama Afro Rock, na kuwa sambamba na nchi nyingine katika Afrika. Katika kipindi hiki mwanasiasa mmoja aliwahi kupiga marufuku muziki wa bugi, ambao ulikuwa ni maonyesho ya muziki ya mchana yaliyokuwa yakisha saa kumi na mbili, na kwa kupiga marufuku muziki huo ilikuwa ni sawa leo upige marufuku wanamuziki wa kizazi kipya, pengo aliloliweka halijaweza kujazwa tena.
MIAKA YA 80/90
Katika kipindi hiki kulikuweko na mfumo wa utawala wa
shughuli za Utamaduni ambao pamoja na kuweko Maafisa Utamaduni wa Wilaya,
Maafisa Utamaduni wa Mkoa , pia kulikuweko na Baraza la Muziki la Taifa (BAMUTA),
ambapo kulizaliwa vyama ambavyo vilifanya kazi kubwa katika kuunganisha
wanamuziki kama vile CHAMUDATA na Tanzania Taarab Association. Na itakuwa ni
makosa kutotaja show iliyokuwa kubwa sana na iliyounganisha wanamuziki wa nchi
nzima TOP TEN Show. Show hii iliyowezekana kwa ushirikiano wa
BASATA, Umoja wa Vijana, Radio Tanzania, halijawahi kutokea tena onyesho lenye
ukubwa wa aina hiyo mpaka leo. Kuvurugika kwa mfumo wa uongozi wa utamaduni kwa
kuwaondoa Maafisa Utamaduni walioko chini ya Wizara ya Utamaduni umeacha
shughuli za Utamaduni mkononi mwa wafanyabiashara pekee, ambao kwao lengo ni
kupata faida za kiuchumi, matatizo na mtokeo ya kufa kwa utamaduni si lolote
kwao.
Serikali inatakiwa ichukue mzigo huu wa kufadhili ukuaji na
uendelezaji wa Utamaduni, na kuacha shughuli za biashara ya kazi za sanaa kwa
wafanya biashara.
Comments