Marehemu Kassim Karuona wa Tabora Jazz, mmoja wa wapiga rythm aliyekuwa bora Tanzania. |
Katika mfumo wa awali bendi za Tanzania, zilikuwa zikitumia si
chini ya magitaa matatu, Solo, rythm na Bass, nasema matatu kwa kuwa kulikuwa
na bendi ziliwahi kufanya majaribio ya kuwa na mgitaa zaidi kama ntakavoeleza
hapo chini. Gitaa la solo lilikuwa na sauti ya juu, huku rythm ikiwa na sauti
nzito kidogo ya kati, na mwisho Bass likiwa na sauti nzito kuliko magitaa
mengine. Kimuundo gitaa la rythm na la solo hakuna tofauti. Yote yana nyuzi
6,lakini katika kutyuni kwenye amplifier, gitaa la rythm hunyimwa treble kiasi
na kuongeza bass zaidi kuliko gitaa la solo ambalo huwa na treble zaidi ya
magitaa mengine. Inasemekana kaka yake Dr Nico, ndie aliyeanzisha mtindo wa
kuongeza gitaa la nne lililoitwa second solo. Hili lilikuwa likipigwa kwa
mifumo mbalimbali katika bendi mbali mbali. Bendi nyingine zilitumia second
solo kama gitaa lililokuwa linajibizana na solo, na bendi nyingine lilikuwa
linajibizana na rythm. Bendi ya Cuban Marimba chini ya Juma Kilaza liliongeza
ubunifu na kuongeza gitaa la 5 na kuliita chord guitar, kadri unavyoongeza
magitaa unahitaji ubunifu zaidi katika utunzi ili kuweza kutoa nafasi magitaa
yote yasikike na pia kila gitaa lipige kitu chake lakini kiwe na uhusiano na
magitaa mengine. TP OK Jazz ilibadili mchezo kukawa na solo mbili, Mzee Franco
akipiga solo na pia wapigaji kama Mavatiku nao wakipiga solo katika wimbo
huohuo lakini wakigawana vipande vya kupiga.
Lakini leo tuzungumzie gitaa la rythm. Chombo hiki bado
kinapigwa katika bendi nyingi lakini umaaarufu wake umeshuka sana. Naona
wapigaji wake hawapewi umuhimu, na unaweza kuingia katika asilimia 90 ya bendi
ukamuona mpiga rythm lakini husiki anapiga nini kutokana na kelele
zinazoruhusiwa kuendelea katikati ya muziki. Katika kipindi cha miaka ya 60 na
70, gitaa hili lilikuwa na umuhimu mkubwa na wapigaji wake waliweza kubuni
staili zao wenyewe. Kati ya wapiga rythm maarufu namkumbuka Satchmo, hilo ndio
lilikuwa jina la kisanii la Harrison Siwale mpiga rythm wa Jamhuri Jazz, yeye
alikuwa na staili peke yake ya kupiga rythm, sikumbuki kusikia mtu mwingine
akipiga rythm ya aina yake kabla ya hapo. Rythm yake ilitawala nyimbo za
Jamhuri wakati huo. Kumbuka wimbo kama Mganga no 1 na 2, au Blandina. Marehemu
Mzee Kasim Kaluwona nae alikuwa na staili tofauti ya upigaji uliyoifanya Tabora
Jazz kuwa na staili yake peke yake, kumbuka gitaa lake katika wimbo Asha, au
Dada Lemmy. Charles Kazembe akiwa na Morogoro Jazz anakumbukwa katika upigaji
wa rythm kwenye nyimbo kama Wajomba Wamechacha, yeye alifuata upangiliaji wa
nyuzi za gitaa kama alivyokuwa anafanya Vata Mombasa wa Lipualipua, yaana
kuweka nyuzi mbili zenye unene sawa katika gitaa lake, uzi namba 1 na namba 4.
Hao ni wachache tu kulikoweko na wengi marufu, wote wakijitahidi kuwa na staili
yao, Butiama Jazz ilikuwa tofauti na Western Jazz, au mipigo ya Mzee Chachil wa
Urafiki. Kama nilivyosema hapo juu katika kipindi hiki huko Zaire kulikuwa na
mipigo mbalimbali ya gitaa la rythm, ikiwemo kitu kipya kilichoanzishwa ambapo
katika ufungaji wa nyuzi ,wapiga rythm wakauondoa uzi namba nne na kuweka uzi
namba moja, hivyo kukawa na nyuzi namba moja 2 katika gitaa, hapo ndipo akina
Vata Mombasa wakaweza kuleta utamu mpya katika upigaji wa rythm. Wakati huo
Orchestra Kiam wakawa wanajivunia kupiga rythm kwa spidi kali sana,vibao kama
Kamiki, Bomoto ni ushahidi wa kazi hizo. Utamu wa ufungaji wa nyuzi kwa staili
hii uliweza kusikika vizuri katika gitaa lililopigwa mwanzo kabisa wa wimbo
Andoya. Leo vionjo vya upigaji huo vinarudi kwa njia ya ajabu sana. Vikundi vya
taarab vimeanza 'kuachia rythm' gitaa moja kubaki linapiga peke yake, japo wao
hupiga gitaa la solo lakini staili ni ile ya enzi, na ukweli Taarab wameteka
wapenzi wengi wa dansi. Ni ushauri utakaofaa kwa bendi zetu kurudisha hadhi ya
gitaa hili katika bendi zao.
Comments