Pamoja na maelezo mazuri ya Serikali kuwa inawajali wasanii,
kuna maswali kadhaa ambayo yanajitokeza na kuleta maswali makubwa zaidi. Idara
ya Utamaduni imekwisha hama Wizara zaidi ya kumi toka nchi hii ilipopata Uhuru,
kwanini?, Mwaka 1995 na pia mwaka
2010,Idara hii ilisahauliwa kutajwa wakati wa kutangaza Baraza la Mawaziri
baada ya Uchaguzi Mkuu, mwaka 2010 tulipewa taarifa kuwa jambo hilo lilitokea
kwa bahati mbaya mwaka 1995 hapakutolewa maelezo yoyote, ila kimya kimya
ikaelezwa Utamaduni utaendelea kuwa chini ya Wizara ya Elimu.
Kuanzia kipindi cha miaka ya 90, Serikali ilifuta ngazi kadhaa
za uongozi katika Utamaduni,
kulikuweko na nafasi ya Kamishna wa Utamaduni haiko tena, kulikuweko na nafasi
ya Afisa Utamaduni Mkoa, nayo haiko
tena. Wako Maafisa Utamaduni wa Wilaya na Manispaa, lakini hawa sasa wako chini
ya TAMISEMI, Wizara tofauti na ile inayohusika na Utamaduni. Haichukui akili
kubwa kuona tatizo lililo wazi linatokea.
Nimeshawahi kumsikia Afisa Utamaduni mmoja Jijini Dar es
Salaam akitamba kuwa yeye hababaishwi na Baraza la sanaa La Taifa, na ni kweli
kwani hayuko chini ya Wizara ya Utamaduni.
Shughuli za pamoja za Kitaifa zilnazohusu Utamaduni ni ngumu
kuzifanya sasa, Mashindano ya Kitaifa ya kazi za sanaa hayasikiki tena, pia
hata shughuli zinazohusika na maslahi ya pamoja ya wasanii kama vile ulinzi wa
haki za wasanii kwa mfano Hakimiliki umekuwa hobela hobela maana hakuna ajenda
ya pamoja kwa viongozi hawa wanaotegemewa kuwa karibu kabisa na wasanii.
Maafisa Utamaduni wa Wilaya wamekuwa zaidi ni wakusanyaji wa pato la Wilaya
bila kuwa na mchango kwa wadau waliomo katika tasnia mbalimbali za Utamaduni
wilayani mwao. Miaka ya nyuma sana Afisa Utamaduni alikuwa kimbilio la msanii,
aliweza kutafuta vifaa vya muziki kwa wanamuziki, kutafuta maeneo ya kufanyia
mazoezi kwa wasanii wasio na nafasi. Community Centers zilikuwa chini ya Afisa
Utamaduni na kuwa mahala ambapo pako chini ya serikali na maalumu kwa shughuli
za sanaa. Community Centers hazipo tena baada ya kugeuzwa aidha ofisi za Manisipaa
au kukodishwa kwa watu binafsi kuongeza pato la serikali za mitaa bila kujali
vijana waliomo katika Manispaa wanapewa sehemu maalumu kufanya shuguli zao za
sanaa.
Ukiangalia Bajeti ya TAMISEMI unajiuliza ni asilimia ngapi ya bajeti hiyo ilienda katika
shughuli za Utamaduni? Utamaduni ukilelewa vizuri ni chombo chenye nafasi
nyingi sana za ajira, huweza kuongeza pato la eneo husika kwa kuhamasisha
maendeleo, kuleta uzalendo, ubunifu wa mambo mbalimbali ya Utamaduni huweza
kuhamasisha Utalii katika Utamaduni, sehemu ya Utalii ambayo kwa bahati mbaya
sana haijatumika kikamilifu katika kuongeza kipato cha nchi hii kwa ujumla.
Si ajabu siku hizi kusikia wasanii wakisema tutaenda kumuona
Rais atusaide katika hili au lile, ni jambo la kusikitisha kuwa matatizo ya
wasanii dawa mpaka kumuona Rais, wasanii wangapi wanaweza kupata nafasi hiyo
katika nchi hii yenye watu milioni zaidi ya 40?
Ni muhimu kuangalia upya mfumo huu wa utawala katika nyanja ya
Utamaduni
Comments