Wanamuziki kuhama kikundi hakutaisha kamwe


Kuhama kwa wanamuziki toka kundi moja kwenda kundi jingine si jambo jipya. Kumekuweko na hadithi hii kwa miaka nenda rudi. Wapenzi wa muziki wamekuwa wakilalamika kuwa kuhama huku kumekuwa kukiwapunguzia utamu wa vikundi walivyovipenda lakini hili halitaondoa tabia ya kuhama.
Wanamuziki nao wamekuwa na maelezo kwanini wanahama, kati ya sababu kubwa imekuwa ni kufuata maslahi zaidi.
Pengine kupata mwanga zaidi kuhusu hili tuangalie vikundi vyetu vya muziki vikoje. Kuna bendi au vikundi ambavyo ni mali, au vilikuwa mali za Taasisi, kwa mfano Bima Lee, JUWATA, Vijana Jazz, Magereza Jazz, Mwenge Jazz, Tancut Almasi na kadhalika, pia kulikuwa na bendi au vikundi vya muziki ambavyo ni vya watu binafsi au vilikuwa mali ya watu binafsi, Safari Sound, Mk Group, Mashujaa, African Stars, kisha kuna bendi ambazo ni mali ya kundi la wanamuziki Double M Sound, B Band, kisha kuna bendi ambazo ni mali ya wanamuziki wenyewe kwa mfano, Kilimanjaro Band au Tanzanite Band.
 Kila moja ya bendi hizi ina maadili yake na makubaliano ndani ya hizo bendi ambayo yanaweza kumfanya mwanamuziki akae bila kuwaza kuhama au awe kila unapomkuta anaota kuhama.
Bendi za kijeshi kwa kawaida hutaka wanamuziki wake wapitie mafunzo ya jeshi husika ili kupata ajira ya kudumu katika bendi hizo, hili huwa kikwazo kwa wanamuziki wengine ambao huwa hawana mpango wowote wa kujiunga na jeshi. Si mara moja tumesikia mwanamuziki katoroka wakati yuko katika kambi ya mafunzo ya kijeshi, wengine hata kuishia kuswekwa kwenye mahabusu za kijeshi kwa kukiuka taratibu za jeshi wakati wamekwishaingia katika kambi za mafunzo.
Kwa wale wanamuziki ambao huamua kujiunga na  majeshi mara chache kusikia wamehama kwani maisha yao huwa na uhakika kimshahara na hata hatima ya maisha yao ya baadae. Na pia kuhama kwao huwa inahitaji kufuata taratibu za kuacha jeshi ambazo si rahisi kiasi hicho.
Bendi za makampuni  mbalimbali kwa sasa ni chache lakini katika kipindi ambapo zilikuwa nyingi, ziligawanyika katika makundi mawili, kuna zile ambazo zilikuwa zikiwalea wanamuziki kwa heshima ileile ambayo walikuwa wakipewa wafanyakazi wengine wa taasisi hizo. Na kuna zile taasisi ambazo wanamuziki hawakuchukuliwa kama ni wafanyakazi hivyo aidha kulazimishwa kuajiriwa kwa jina la kazi tofauti. Mpiga gitaa kutajwa katika ajira yake kuwa mesenja. Hii ilikuwa inaleta hali ya wanamuziki kuona wazi hawana thamani katika kampunini hizi. Bendi za watu binafsi nazo zilikuwa na taratibu zake, haikuwa kitu cha ajabu kukuta bendi nzima hakuna mtu hata mmoja aliyeajiriwa, au kukuta ni baadhi tu ya wanamuziki wameajiriwa. Pia kulikuweko na hali ya kuwa na mkataba, katika hali hii wenye mkataba ndio waliokuwa na uhakika kidogo wa malipo, wasio na mkataba kutokuwa na uhakika wa malipo.
Katika bendi au vikundi ambavyo vilianzishwa na wanamuziki kwa makubaliano kuwa hatimae matunda ya bendi yatakuwa yanagawiwa kwa waanzilishi wote hili limekuwa likipata matatizo mara kundi linapoanza kupata mafanikio, kuna tokea kundi la wanamuziki wanaojiita waanzilishi, siku hizi hujiita wakurugenzi na wanamuziki wengine kujikuta wafanya kazi wa wenzao walioanza na kupata tabu pamoja, na mara nyingi makundi haya yameanguka chali licha ya kuonekana yanaendelea vizuri. Mwisho ni yale makundi ambayo wanamuziki wenyewe wamejikusanya na kupata vyombo na vikawa mali ya wanamuziki wote, makundi haya pia yamekuwa na migogoro ya kutokuelewana japo kuonekana wanamuziki wake wanadumu muda mrefu zaidi katika kundi bila kuhama, kwa kuwa wahusika walikuwa wanalinda masilahi yao katika mgao mzima wa bendi.
Fedha imekuwa sababu kubwa ya wanamuziki kuhama, aidha kwa kuahidiwa donge nono au maisha manono, au kuahidiwa ajira kutoka kundi ambalo hakukuwa na ajira. Dar es Salaam International ilipoteza wanamuziki wake wengi wakahama na kuanzisha Mlimani Park Orchestra kwa kuwa waliahidiwa ajira, ambayo hawakuwa nayo walipokuwa Dar International. Baadaye sana kundi la akina Max Bushoke, Fresh Jumbe, Ali Jamwaka, Bilali, walihama kwa mkupuo Sikinde na kwenda Ndekule kwa ajili ya fungu la pesa walilopewa , Bilali alirudishwa na wapenzi wa Sikinde baada ya kurudisha shilingi alfu hamsini alizopewa na kundi la Ndekule.
Lakini si pesa peke yake iliyokuwa sababu ya mwanamuziki kuhama bendi, kulikuweko na tatizo la kiusanii, msanii mzuri hujali sana kazi yake itatokaje, hivyo akikaa katika kundi ambalo anaona haridhiki na kazi inayofanyika hapo fedha huwa haina maana. Kuna wanamuziki wengi wazuri wamejikuta wakishawishiwa kuhama makundi kwa kupewa fedha nzuri lakini wakifika katika kundi jipya hujikuta hawana amani kutokana na kujikuta wanashindwa kuonyesha ufanisi wao kwa kukosa wasanii wenzao wanaofaa.  Kwa maelezo haya lazima tuelewe kuwa wanamuziki wataendelea kuhama toka kikundi kimoja mpaka kingine hata kama kuna fedha kiasi gani ambacho msanii ataahidiwa.

Comments