Muziki wa Dansi umezidiwa ujanja na Taarab?


Wakati wa Top Ten Show, onyesho lililokuwa kubwa sana la mashindano ya bendi, ambapo bendi kutoka mikoa yote zilipata nafasi sawa za kuonyesha uwezo wao na hatimae kuchaguliwa Bendi Bora, vikundi vya muziki wa Taarabu havikushirikishwa  kwa kuwa vilikuwa vikipiga muziki tofauti na bendi za muziki wa dansi, palikuweko hata malalamiko kutoka kwa baadhi ya bendi ya kupinga kundi la Varda Arts ambalo lilikuwa likipiga muziki wake kufuatia mirindimo ya Kihindi kushiriki katika shindano hili. Hata vyama vya muziki wa Taarab na muziki wa dansi vilikuwa tofauti. CHAMUDATA (Chama  cha Muziki wa Dansi Tanzania) kwa ajili ya muziki wa ‘dansi’ na TTA (Tanzania Taarab Association) kwa ajili ya muziki wa Taarab. Mambo yamebadilika sana siku hizi, sioni hata sababu ya kuwa na vyama viwili kwa  kuwa tofauti  za kimuziki za makundi haya zimepotea sana

 Kila nikiingia  katika kumbi mbalimbali kuangalia na kuburudika na kazi kutoka  vikundi vinavyojitambulisha kuwa ni vya Taarab na vile vinavyojitambulisha kuwa ni vya dansi, napata maswali mengi kichwani, na kwa kweli naona makundi haya mawili yamebadilishana nafasi.

Muziki wa Taarab ulikuwa na sifa ya kuwa aina ya muziki wa kusikiliza ujumbe wake, wapenzi wake na hata wanamuziki walikuwa wamekaa na kutulia na kutafakari ujumbe unaotolewa, wakati muziki wa dansi ulikuwa ukijulikana kwa mirindimo ambayo ingekufanya usimame ucheze. Sio siri siku hizi unaweza kuingia kwenye kundi la muziki wa dansi zikapigwa nyimbo  hata tatu, usione watu wanasimama na kucheza, lakini wanasikiliza muimbaji anasema nini, na kumtuza muimbaji kwa anachoimba. Wote tunafahamu kuwa kwa sasa kuna tuzo hata za ‘Rapa” bora, ambaye ubora wake unatokana pia na maneno atakayotamka.

 Katika Taarab mambo yamebadilika, wimbo ukianza ukumbi hujaa watu wakicheza, kila mtu kwa staili yake, na siku hizi hata makundi mengine ya Taarab yana vijana wanaonyesha namna ya kucheza  wimbo husika. Ile staili ya zamani katika bendi ya kuachia gitaa la rhythm lipige peke yake imehamia kwenye taarab ambapo gitaa huachwa likipiga , tena mara nyingine vipande vya nyimbo za bendi za zamani, na watu hufurahi sana. Kwa leo sitaki kuingia katika malumbano yanayoendelea ya wapenzi wa Taarab asili wakisema wazi kuwa kinachoendelea katika vikundi vinavyotambulika kama ni vya Taarab si Taarab hapana hilo nitalisema siku nyingine,leo nataka wanamuziki wa muziki wa dansi wajiulize je wameacha kupiga muziki wa dansi na siku hizi wanapiga muziki wa kusikiliza tu?

Pamoja na kuwa muziki unakosa wachezaji kwenye ukumbi kuna swala la wacheza show kuchukua muda mwingi kucheza na tena kucheza katika eneo ambalo awali lilikuwa ni la wapenzi wa dansi, jambo ambalo linadhihirisha wazi kuwa hata wanamuziki wenyewe wameamua kuwa wao lengo lao si kuwafanya wapenzi wacheze bali waangaliwe wao umahiri wa kulisakata rumba.

Ni vizuri basi kubadili jina na kuacha kujiita bendi za muziki wa dansi, na kuwaachia wanamuziki wa muziki wa Taarab sifa hiyo

Nakumbuka zamani, wakati wa kutunga nyimbo wanamuziki wa muziki wa dansi  walikuwa wakijiuliza ‘Je, wimbo huu unachezesha?’, na wimbo ulikuwa hautolewi hadharani kama wanaona hautahamasisha kucheza, na hata kama waliridhika katika mazoezi kuwa ‘unachezesha’ ikiwa baada ya kupiga mara moja au mbili kwenye ukumbi ukaonekana ‘hauchezeshi’ wimbo ulirudi tena kwenye mazoezi.

Kunahaja kubwa ya wanamuziki wa dansi kujiuliza swali’ Wanapiga ili kusikilizwa au watu wacheze?


Comments