List fupi ya Hall of Fame yangu

Shikamoo Jazz kazini

Katika siku za karibuni tumekuwa tukisikia kitu kinaitwa Tuzo za hall of Fame, katika shughuli zilizopita karibuni za Kilimusic Awards 2012, Tuzo hii ilitolewa kama ifuatavyo; Tuzo ya HALL OF FAME ilienda kwa JKT, Tuzo ya HALL OF FAME kwa mtu binafsi ilienda kwa  KING KIKII na pia tena  HALL OF FAME kwa mtu binafsi ipia litolewa kwa  Hayati REMMY ONGALA.
Je HALL OF FAME ni nini? Hall of Fame, Walk of Fame, Wall of Fame, Walk of Stars au hata Avenue of Stars imekuwa aina ya njia ya kuonyesha kuwathamini watu walioonekana kutoa mchango mkubwa katika tasnia fulani. Zamani ilikuwa zaidi na maana ya msanii aliyefahamika zaidi ’Famous’ lakini katika miaka hii imekuwa kuwa ‘celebrity’ au ile hali inayojulikana hapa kwetu kama kuwa Super Star  ni kigezo tosha cha kuweko katika tuzo zilizotajwa hapo juu.
Katika sehemu nyingine Hall of Fame huwa ukumbi hasa uliojengwa ambamo ndani yake kunawekwa sanamu za wale ambao wamefanikiwa kuonekana kufaa kutuzwa. Na Walk of Fame huwa ni sehemu ambazo majina au picha za wahusika huchorwa au huandikwa ardhini.
Leo ningependa kutaja baadhi ya watu ambao wangefaa kuingia katika Hall of Fame katika tasnia ya muziki hapa nchini. Kwanza lazima kukubali kutokana na tatizo la nchi yetu kutokujali kuweka kumbukumbu za watu maarufu mara nyingi huwa vigumu kupata taarifa sawa ni nani hasa anastahili kuwekwa katika Hall of Fame.
Kati ya watu ambao kwa mtazamo wangu wangestahili kuweko katika Hall of Fame wa kwanza ni Marehemu Frank Humplick na dada zake, jina hili linaweza kuonekana geni kwa watu wengi lakini ni watu wengi wanakumbuka wimbo kama Kolokolola, Frank Humplick alikuwa Mtanzania ambaye nyimbo zake alizorekodi kuanzia miaka ya 50 hadi 60, lakini nyimbo zake za toka miaka hiyo zinapigwa mpaka leo na bendi nyingi Afrika Mashariki. Ni bahati mbaya Tanzania haijatumia vizuri sifa za Mzee huyu kiasi cha kwamba wengi hudhani nyimbo hizi zilipigwa na Mkenya hususan Mzee Fundi Konde.  Hall of Fame ingemwendea Mzee Salum Zahoro, mzee huyu yumo katika shughuli za muziki kuanzia mwishoni mwa miaka ya 50, mpaka LEO. Mzee Zahoro kwa sasa anapiga na kuimba katika bendi yake ya Shikamoo Jazz, akiimba nyimbo zake za miaka hiyo utadhani ni kijana wa miaka ishirini wakati yuko katika umri wa miaka 70. Mzee huyu wengi wa zamani wanamkumbuka akiwa na bendi yake ya Kiko Kids, bendi iliyokuwa maarufu Afrika ya Mashariki nzima, ikiwa na makao yake makuu Tabora. Ni vizuri kukumbuka kuwa katika miaka hiyo vyombo vya habari havikuwa vingi na bora kama ilivyo sasa, hivyo ilikuwa ni lazima uwe msanii mahiri sana kuweza kufahamika na kuheshimika kanda hii yote. Mzee Salumu Zahoro alikuwa akipiga mandoline wakati bendi nyingine zote zimehamia kwenye kupiga magitaa ya umeme, na mpaka leo ndie mwanamuziki peke yake anaepiga mandoline kwenye muziki wa dansi. Hall of Fame haiwezi kumkwepa Bi Shakila, ambaye sauti yake haijabadilika sana kwa zaidi ya miaka 40 ambayo amekuwa katika fani ya muziki haswa wa taarabu. Hall of Fame pia haitamkwepa Mabruk Khamis maarufu kama Babu Njenje kwanza kwa kudumu katika bendi moja kwa miaka zaidi ya 34, pili kwa kuwa ndiye kinara wa uimbaji wa mtindo wa mduara. Hall of Fame yangu ingependa mutaja John Ndumbalo, huyu alikuwa sound engineer aliyerekodi nyimbo nyingi ambazo bado zinatambaa akiwa RTD na baadae TFC. Tuliowahi kufanya nae kazi tunakumbuka alivyokuwa haoni tabu kukesha usiku kucha lakini asubuhi akiamka na kusikiliza kazi yake kama haikumfurahisha kuamua kuifuta na kuanza upya.
Mwisho Hall ya Fame bila Marijan Rajabu itachekeshe, mwanamuziki huyu aliyezikwa katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam , alikuwa si mtunzi tu, ambaye nyimbo zake zinaendelea kupendwa mpaka leo lakini pia alikuwa alikuwa muimbaji mahiri na mpiga gitaa mkali pia.







Comments

Anonymous said…
ninakubali. Pia, Salum Abdallah; mbaraka mwinyishehe; Shem Karenga; John Ondolo Chacha; Gurumo na Mabera.
Anonymous said…
Nimeikubali Hall/Walk of Fame yako.
R. Mloka