Wanamuziki wa Tanzania na utamaduni wa kuiga nyimbo


Si jambo la ajabu kukuta mwanamuziki wa Tanzania kachukua wimbo wa mwanamuziki kutoka nje ya nchi hii na kuweka maneno ya Kiswahili na kuutambulisha kama wake. Katika siku za karibuni msanii anayejulikana kwa jina la Timbulo alikiri katika radio kuwa ni kweli amechukua nyimbo Domo Langu na Waleo wakesho, kutoka kundi la X Maleya  la huko Cameroon. Japo aliwahi kukataa kabla jambo hilo na kudai alikuwa kazitunga nyimbo hizo zamani ila kachelewa kuzitoa. Swala kama hili liliwahi kumkumba mwanamuziki TID miaka michache iliyopita. 
Lakini ni ukweli wenye ushahidi  kuwa matukio kama haya si mageni hata kidogo katika historia ya muziki wa Tanzania.  Katika miaka ya sitini,  nchi hii ilikuwa na vikundi vingi sana vya muziki, karibu kila wilaya ilikuwa na bendi ya muziki, Tanu Youth League ambayo ilikuwa jumuiya ya vijana ya chama cha TANU ilikuwa moja wapo ya vyanzo vikubwa vya bendi kwani matawi mengi ya wilaya ya TANU yalikuwa na vyombo vya muziki, na hivyo kuwa na bendi. Jambo moja lililokuwa wazi ni kuwa bendi zilikuwa zimekithiri kwa kunakili nyimbo za bendi kutoka Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Kati ya bendi zilizokuwa maarufu kwa hili zilikuwa Dar es Salaam Jazz Band na Kilwa Jazz Band, nyimbo zao za kuiga bado zinapigwa sana hadi siku hizi na wengi hudhani ni tungo za bendi hizo. Wengi tunaufahamu wimbo wa  Ahmad Kipande na Kilwa Jazz ‘Moyoni naumia’, huu ulikuwa utunzi wa Tabu Ley na aliuita ‘Mokolo na kokufa’, nyimbo nyingine kama  Mapenzi yanani vunja mgongo, Pesa nyingi nimepoteza, Na kadhalika zilikuwa moja kwa moja tungo za OK Jazz.  Hali ilikuwa mbaya mpaka serikali ililazimika kuingilia kati na kikao cha wanamuziki kilifanyika pale Lumumba kwenye ofisi za TANU ambapo Waziri husika aliwaomba wanamuziki waanze kutunga nyimbo zao. Baada ya hapo Kilwa jazz walitunga wimbo wenye mashahiri yakisema.’Koma koma koma kaka we tunga zako’.
Hata bendi uinayosikia kama Afro 70, pia iliingia katika mtego huu wa kunakili nyimbo, wimbo, Umoja wa Kinamama, ulikuwa moja kwa moja kutokana na wimbo Georgette wa TP OK Jazz. Vijana jazz Band nayo inaingia katika orodha hii kwa wimbo wao uliotumika katika kusherehekea miaka kumi ya Umoja wa Vijana  wa CCM, ambao nao ulikuwa wimbo wa TP OK Jazz.
Wote tunakifahamu kibwagizo kilichokuwa kikitumika na band ya African Stars, kikisema, Twanga Pepeta hatutaki shari Tunatesa’ ambacho ilitoholewa toka kwa kibwagizo alichokuwa akitumia Defao wakati wa staili ile ya Kiwanzenza.
Bila kubisha hali ya kutohoa nyimbo ni kubwa sana kwa zile bendi ambazo hupiga moja  kwa moja muziki kutoka Kongo. Kwa siku hizi kuanzia uvaaji, uchezaji, na hata kutembea vinaigwa. Vibwagizo huwekwa maneno ya Kiswahili, melody au vipande vya magitaa  au madaraja katika nyimbo hurudiwa vilevile ambavyo vimepigwa na Kofie, au wanamuziki mahiri wa vikundi vya Wenge. 
Wanamuziki wa nyimbo za enjili ni mabingwa mno wa wizi wa namna hii, wengi wamepata umaarufu hata kupata tuzo kwa nyimbo ambazo si zao, katika upande wa nyimbo za enjili muziki kutoka Afrika ya Kusini ndio umekuwa ghala la kuchota melody na uchezaji.
 Muda umefika na kupita wa wanamuziki wetu kuacha kuiba nyimbo au vipande vya nyimbo za wanamuziki wengine. Na muda muafaka wa serikali hii kufanya lile lilifanywa na serikali ya miaka ile mwishoni mwa miaka ya 60

Comments