Mchawi wa vyama vya muziki ni wanamuziki wenyewe-Part 1


Uongozi wa kwanza wa CHAMUDATA-Toka kushoto waliosimama- Mabela, Mkwega, Maneti, Chidumule, Mzelu Waliokaa Farahani, Mapili, Ubao, Hoza
Katika historia ya muziki hapa nchini, kumekuweko na vyama vingi vya muziki. Miaka ya nyuma kulikuweko na vyama kama Dar es Salaam Musicians Association, baadae wakati lilipokuweko Baraza la Muziki la Tanzania(BAMUTA), kulianzishwa vyama kama Tanzania Taarab Association(TTA),  na  Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA). Baadae katika enzi ya Baraza La Sanaa La Taifa, kumekuweko vyama kama Tanzania Folk Music Development Association(TAFOMUDEA), Tanzania Rappers Association (TRA), Tanzania Women Musicians Association(TAWOMA), Union of Tanzania Musicians (UTAMU),Tanzania Disco Music Association (TDMA), Tanzania Musicians Network (TAMUNET), Tanzania Urban Music Association (TUMA) na vingine vingi. Pia siku hizi kuna Shirikisho la Muziki Tanzania ambalo linategemewa kuwa ni muungano wa vyama vyote vya muziki nchini.
Pamoja na idadi kubwa ya vyama vya muziki kama ilivyotajwa hapo juu  ni vyama vichache sana ambavyo vimetajwa vinaweza kuitwa viko hai.
Bila kusita nasema kuwa wachawi wa maendeleo ya vyama hivi ni wanamuziki wenyewe. Nichukue mfano wa CHAMUDATA chama ambacho ni kati ya vyama vikongwe katika tasnia hii, chama hiki kiliasisiwa mwishoni mwa miaka ya 80 kilidumu muda mfupi tu katika hali ya amani, kabla ya kuingia katika wimbi zito la mgogoro uliokiingiza katika miaka ya  90 na kukiweka katika hali ya kuwa na makundi mawili ya viongozi na  kila moja likidai kuwa ndilo linaloendesha chama, kundi moja likitembea na mikwaju kuzuia mikutano kufanyika bila ruksa yao. Kitendawili hiki kilikuja tenguliwa na Waziri wa Elimu na Utamaduni wakati huo aliyetoa amri ya kufanyika kwa uchaguzi wa chama hicho na hatimae uchaguzi ukafanyika mwanzoni mwa mwaka 1993. Mara tu baada ya uchaguzi mgogoro mpya uliibuliwa. Miaka hiyo CHAMUDATA kilikuwa ni chama cha wanamuziki wa muziki wa dansi tu kama lilivyo jina lake. Siku ya uchaguzi kuna bendi kadhaa ambazo aidha  wanamuziki wake hawakuhudhuria mkutano huo au walikuja wawakilishi wachache tu wa bendi mkutanoni, uchaguzi ulipofanyika Mwenyekiti na Katibu Mkuu walitoka Vijana Jazz, pamoja na kuwa katika kamati kuu kulikuwa na wanamuziki kutoka JKT Jazz Band, Police Jazz band, JUWATA Jazz na kadhalika, kampeni ilianzishwa kuwa CHAMUDATA ni chama cha Vijana Jazz Band. Mgogoro wa kwanza ukaanza, hatimae Katibu Mkuu akijitoa ili kuwezesha chama kwenda mbele. Ikaja mada mpya, chama hakiwataki wanamuziki wa Kikongo, hili likafika mpaka kuandikiwa makala kubwa katika gazeti maarufu wakati ule , gazeti la Mfanyakazi, na kusababisha hata kufanyika kikao kati ya CHAMUDATA na Mkurugenzi wa Uhamiaji, tatizo hilo lilitokana na juhudi za CHAMUDATA wakati huo kutaka kupata idadi kamili ya wanamuziki nchini, hivyo fomu zilitumwa kwa bendi zote kujaza zina wanamuziki wangapi na kama ni wananchi au wageni. Bendi zenye wanamuziki wageni zikagoma kutoa taarifa. CHAMUDATA ilipofuata taarifa zao Uhamiaji  ndipo tuhuma hizo zilipoanza hasa baada ya mfanyakazi mmoja wa ukurugenzi huo kutuhumiwa kuwa kuwataarifu wanamuziki kadhaa wageni  kuwa CHAMUDATA  ina mpango wa kuwafukuza nchini. Tatizo hili lilikiweka chama katika hali mbaya kwa muda mrefu sana.
Mwaka 1997, CHAMUDATA iliweza kuanza kufanya mazungumzo na wafadhili kutoka Norway, mazungumzo haya yalizaa ufadhili wa mkutano mkubwa wa siku nne wa wanamuziki karibu 250, kuweza kuishi na kupata semina mbalimbali pale Bagamoyo. Kati ya mipango mingine iliyopangwa na kuanza kutekelezwa ni mpango wa kuwapatia wanamuziki wa Tanzania, radio yao, studio yao, gazeti lao, na kuwezesha kusambaza kazi zilizorekodiwa katika studio yao huko Norway kwa kupitia kampuni ya huko inayojulikana kama KKV.
Ila jambo moja ambalo wafadhili waliona lina dosari ilikuwa ni katiba ya CHAMUDATA, waliona haiwapi wanachama uwezo wa kufuatilia vya kutosha haki zao katika chama, hivyo basi fedha zikatolewa na kuwezesha kamati ya kutayarisha katiba mpya ifanye kazi. Makubaliano na wafadhili yalikuwa CHAMUDATA ikamilishe katiba yake kupitia ngazi husika na wafadhili wangeanza kutekeleza ahadi yao ya kuleta studio, kufungua radio, na kuwezesha kuanzishwa gazeti.
Kwa kifupi ni jambo la kushangaza lakini siku wafadhili walipokuja na vifaa vya studio, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CHAMUDATA walikataa kupokea vifaa hivyo kwa kudai kuwa wafadhili walikuwa wanawaburuza kubadili katiba yao. Jitihada za serikali kupitia Wizara ya Utamaduni kuwashauri viongozi wa CHAMUDATA kubadili mawazo ziligonga ukuta, licha ya chama hicho kupewa miezi sita ya kurekibisha mambo yake, hakuna lililofanyika, hatimae wafadhili wakafunga virago vyao.  Mpaka leo CHAMUDATA imebaki kuwa na migogoro isiyoisha.

Comments