Ukosefu wa takwimu katika kazi za muziki ni ufisadiTakwimu ni muhimu katika mipango yoyote yenye maana. Tatizo kubwa linaikabiri tasnia ya muziki ni takwimu. Pamoja na kuwa kila dakika kwa masaa ishirini na nne kazi za muziki zinatumika kwa namna moja au nyingine bado takwimu za matumizi haya zimekuwa kitendawili. Hakuna mahala utaweza kwenda ukapata hesabu kamili za mapato ya sekta hii.
Kuna matumizi ya muziki makubwa katika vyombo vya utangazaji TV na radio. Kuna stesheni za radio zaidi ya 70 na stesheni za  TV  zaidi ya 25, ambazo nyingi huwa hewani masaa 24. Kwa mfano ukijaribu kuuliza wamekwishapiga nyimbo ngapi katika vituo vyao kuanzia tarehe 1 Januari 2012, kigugumizi kitaanza, wengi hawaweki kumbukumbu zozote za matumizi hayo. Kuna kampuni za simu zaidi ya nne na katika hizo siku hizi kuna huduma ya kununua nyimbo  kwa ajili ya  ringtone, huko nako ukiuliza takwimu, unaambiwa ni siri, lakini wote tunaotumia simu za mkononi, tunajua ukipiga simu utapokelewa na muziki, wengine huwa na muziki wakipokea simu, wengine hunakili muziki kwenye simu zao, na simu ziko kwa maelfu.
Ukizunguka kwenye bar na grocery hapa nchini, ambazo ziko kwa maelfu kama si mamilioni muziki unatumika kuita wateja, huko nako takwimu hakuna kabisaaa, muziki hupigwa masaa yote ambapo bar iko wazi ili kuburudisha wateja. Bar isiyo na muziki hukimbiwa na wateja. Kwenye madisco, kwenye  sherehe ambazo maDj wanalipwa kwa kupiga muziki, kote huko hakuna takwimu. Lakini kitu kimoja kiko wazi kote huku haya matumizi si bure kuna mabilioni ya fedha yanapatikana.  Kila mara habari za matumizi yasiyo ya haki katika kazi za sanaa yakiwa yanazungumziwa huwa macho yanaelekezwa kwenye kurudufu CD na DVD na vihifadhia sauti kama hivyo tu, hao watumiaji niliowataja hapo juu  hawatajwi.
Vyombo kama TV na Radio huwa hata na vipindi ambavyo huongelea matatizo ya wanamuziki kukoseshwa kipato na mara zote huzungumziwa piracy na wamachinga, lakini matumizi yasiyoya haki yanayofanywa na vyombo hivyo huwa hayatajwi.
Katika biashara ya mauzo ya kazi za muziki , kanda, CD, na DVD, kama nilivyokwisha sema hapo juu takwimu imekuwa kitu adimu. Lakini kuna mahesabu ya haraka haraka ambayo yanaweza kutoa picha ya  ukubwa wa mapato katika biashara hii. Tanzania ina watu kiasi cha milioni 40, lakini tukikisia kuwa ni asilimia kumi tu ya wananchi hawa wenye uwezo wa kununua kazi za muziki tunakuwa na soko la muziki la watu milioni 4. Kutokana na hali ya uchumi ya Watanzania, tukisie kuwa kila mtu katika hawa anaweza kununua CD 5 tu kwa mwaka, hii inatupa idadi ya CD zinazoweza kuuzwa Tanzania ni milioni 20 kwa mwaka. Kwa kuchukua kuwa bei ya CD ni shilingi 3000/-, biashara ya CD za muziki kwa mwaka inaingiza si chini ya shilingi 60,000,000,000/-. Lakini tena kwa kuwa hakuna takwimu za ukweli haya ni makisio tu.
Kuna haja ya kujiuliza kwanini hakuna takwimu? Mapato yanayopatikana kutokana na kazi za muziki huwa ni mgao wa wadau wengi kati yao ni wanamuziki, wafanyakazi mbalimbali katika biashara ya muziki, na serikali ikipata pato kama kodi.
Usiri wa takwimu unatokana na sababu za kuwa ni njia nzuri ya kukwepa kugawana na wadau wengine mapato wanayostahili. Hivyo basi ukosefu wa takwimu umeleta picha ya uongo kuwa muziki haulipi. Jitihada zinazowahusu hata watu wenye heshima katika jamii zinafanyika ili hali hii ya utata iendelee. Kuanzia mwaka 2003 kumekuweko na Regulations zilizokuwa zimetengezwa kusaidia kutekeleza sheria ya Hakimiliki ambazo zinaelekeza jinsi vyombo vya utangazaji namna ya kulipa kutokana na matumizi ya muziki, pamoja na idadi kubwa ya vyombo vya utangazaji nilivyovitaja hapo juu ni radio moja tu!!!!! ambayo inalipia matumizi ya kazi za muziki mpaka sasa. Si siri kuwa katika vipindi vya radio na TV ambavyo hudhaminiwa na makampuni mbalimbali  ndani yake kunapigwa muziki, ni akili ya kawaida tu kuwa sehemu ya mapato hayo yalistahili kupewa wanamuziki, lakini hili halitekelezwi hata na TBC ambayo Mtendaji wake Mkuu ni kutokana na uteuzi wa Rais.
Kwa upande wa kazi kama CD,DVD, na kadhalika kuanzia mwaka 2006 kumekuweko na Regulation ambayo iliwezesha kutengenezwa kwa stika (Hakigram), ambazo zingebandikwa katika kila kazi halali ya muziki na filamu. Regulation hii ambayo ililazimika kusainiwa kwa mara ya pili na Mheshimiwa Karamagi, baada ya ile ya awali iliyosainiwa na Waziri wa awali wa Viwanda na Biashara  Mhe. Ngasongwa kuibiwa kutoka ofisi za Wizara hiyo kabla hazijatangazwa katika gazeti la serikali, mnamo mwaka 2005.  Mpaka leo utekelezaji wa matumizi ya hizi stika nao umekuwa na kigugumizi. Stika hizi zingesaidia wasanii kuelewa takwimu ya kazi zao zinazosambazwa na pia kusaidia kuzipa mamlaka husika na kodi takwimu sahihi ya soko la kazi za muziki.
Ni muda umefika na kupita kwa serikali kuiangalia sekta hii ambayo ni chanzo kikubwa cha pato la serikali na ambalo likilindwa vizuri litatoa kipato kizuri kwa wanamuziki na wahusika wengine wote na kuongeza idadi kubwa ya ajira kwa marika yote.

Comments

Anonymous said…
Ni nani mwenye jukumu la kuhifadhi hizi takwimu, kuzifuatilia, na kuzifanyia kazi?