Nyimbo zetu za live ni ndeeeeeeeeeeeeeeefu




Juzi nimeingia bendi tatu tofauti za rafiki zangu katika muziki. Kitu kimoja ambacho nilikuta ni kawaida katika bendi hizo ni urefu wa nyimbo zao. Niliweza kufuatilia muda wa nyimbo moja wapo na ilikuwa na urefu wa dakika 50. Zilibaki dakika kumi tu ili itimie urefu wa saa moja kwa wimbo.
Historia ya urefu wa wimbo imekuwa inaenda sambamba na kuboreshwa kwa teknolojia.  Wakati santuri za kwanza zinaanza kutumika kwenye mwaka 1900, teknolojia haikuruhusu wimbo kuzidi urefu wa dakika 5, iliwekwa sheria ya kiufundi kuwa wimbo usizidi dakika 3 na sekunde 45. Hivyo watunzi walilazimika kutunga na kuhakikisha ujumbe na muziki vinakamilika katika muda huo. Hivyo nyimbo nyingi maarufu zilizorekodiwa katika wakati huo zilikuwa na urefu usiozidi muda huo. Nyimbo kama Chaupele Mpenzi, Embe Dodo, Majengo Siendi Tena, zote hazizidi muda huo lakini wote tunakubali kuwa zinajitosheleza kwa ujumbe na muziki kiasi kwamba zinaigwa na wanamuziki wa leo, japo nyimbo hizo zilizorekodiwa zaidi ya miaka 40 iliyopita.
Teknolojia ya santuri ilizidi kuwa bora kiasi cha kuweza kurekodi nyimbo za hata dakika 20 za muziki kwa upande moja wa santuri, teknolojia hiyo iliyowekwa hadharani na kampuni ya Columbia Records iliwezesha nyimbo nyingi kuwekwa katika santuri moja na ikaitwa LP (Long Play).
Wakati huo huo kukawa na santuri ndogo zilizopewa jina la SP(Short Play) ambazo zilikuwa na uwezo wa kurekodi muziki wa dakika 7. Kwa miaka mingi kwa sababu hii nyimbo nyingi zilirekodiwa zikifikiwa na urefu ambao haukuzidi dakika 8. Kuingia kwa teknolojia ya Kanda za kaseti ambazo ziliweza kuwa na urefu wa mpaka kuweza kurekodi dakika 60 kwa upande mmoja, nyimbo zilizorekodiwa zikaanza kuwa ndefu. Muziki wa Taarab ulianza kuwa na sifa ya kurekodi nyimbo ndefu, kiasi cha kuwa na nyimbo 4 tu katika kanda nzima ya dakika 60.
Nakumbuka mkutano mmoja kati ya wanamuziki na kiongozi wa redio mmoja lilichofanyika Leaders Club ambapo wanamuziki wa muziki wa dansi na wale wa Taarab walikuwa wakilalamika kuwa redio hiyo haipigi nyimbo zao. Moja ya sababu alizozitoa kiongozi huyo ni kuwa nyimbo ni ndefu mno, kwani ikiwa ana kipindi cha dakika 30 ataweza kupiga nyimbo 2 tu za Taarab kutokana na urefu wa nyimbo hizo na hata hivyo mtangazaji hataweza kuongea chochote katika kipindi kama hicho.
Ujio wa teknolojia ya CD na DVD umewezesha nyimbo kuwa na urefu hata wa masaa kadhaa. Aidha teknolojia hiyo imewezesha CD moja kuwa na nyimbo nyingi sana ikiwa zitakuwa ni za muda mfupi.
Katika muziki kwenye jukwaa bendi zilikuwa zikipiga wimbo na kujitahidi usizidi dakika 15. Katika kipindi fulani niliwahi kuwa katika bendi ya Orchestra Makassy, wakati huo marehemu Dr Remmy alikuwa na mkataba maalumu ambapo alikuwa anapewa  muda wa saa mbili katika kila onyesho ambapo alikuwa akiimba nyimbo zake. Alikuwa na nyimbo ambazo zilikuwa ndefu sana kiasi cha kupiga nyimbo mbili au tatu tu katika muda huo aliopewa hili lilisababisha wanamuziki wengine kulalamika katika kikao cha bendi kuwa lazima afupishe nyimbo zake.
Vijana Jazz chini ya Hemed Maneti kulikuwa na mikutanao kadhaa ya kuhakikisha nyimbo hazizidi dakika 15 kwenye onyesho, sababu kubwa ni kuwa wimbo hata uwe mzuri vipi wasikilizaji na hasa wachezaji huuchoka ukiwa mrefu mno, na hivyo kukosa watu wa kucheza. Jambo ambalo naliona wazi kila  nikitembea katika bendi nyingi, watu aidha hucheza kwa kipindi kifupi na kuondoka katika eneo la kuchezea, ni wazi si rahisi mtu kucheza kwa wimbo mmoja kwa dakika 50.
Naona imekuwa kawaida kwa bendi siku hizi kupiga wimbo kwa zaidi ya dakika 40, na kama kuna stage-show basi wimbo mmoja unaweza hata kuzidi hata urefu wa saa moja na dakika 15. Tatizo la wimbo kuwa mrefu mno ni kuwa hatimae unakuwa haueleweki ulikuwa na ujumbe gani mwanzoni, na ndipo kunaingia ufundi wa kutunga maneno ya papo kwa papo kiasi cha kuwa baada ya mwezi wimbo huwa tofauti na ulivyokuwa awali.


Comments