Wakati huu wa kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru kuna mengi mazuri ya kukumbuka lakini pia kuna mengi mabaya na ya kusikitisha. Kati ya mabaya kuna mengine yamepita tugange yajayo, lakini kuna mengine yanaendelea na ni lazima tuyaondoe. Kati ya yale ambayo yanasikitisha na ni lazima liondolewe ni hili la miaka 50 ya wizi wa kazi za wasanii.
Nchi yetu kama zilivyo nchi nyingine za Afrika ilipitia katika vipindi kadhaa kikiwemo cha kabla ya ukoloni, ambapo msanii alikuwa na nafasi muhimu katika jamii. Msanii alikuwa ni maktaba ya matukio katika jamii, alikuwa ni darasa la jamii, alikuwa ni kiungo muhimu katika matambiko ya jamii, na hata katika matibabu ya jamii na pia mburudishaji wa jamii, na jamii ilimlea kutokana na kipaji chake, na kupewa nafasi ya juu katika jamii.
Katika kipindi hicho matumizi ya kazi za sanaa yalikuwa na mipaka kutokana na kazi za sanaa kuwa na malengo na matumizi maalumu, na kutokuweko na teknolojia ya kufanya kazi hizo ziweze kutumika na watu wengi kwa wakati mmoja.
Ujio wa wakoloni pia ukawa ndio chanzo cha miji, ambapo makabila yenye tamaduni mbalimbali yalianza kukusanyika pamoja na pia wakati huo huo kuanza kukutana na utamaduni wa wakoloni, hivyo kuanza kujenga utamaduni mpya. Muziki ulikuwa sehemu muhimu ya utamaduni huu mpya. Ni jambo lililo wazi kuwa jamii huwa haina jina kwa kitu ambacho hakipo katika jamii ile, kwa msingi huo hakukuweko na muziki kama tuujavyo leo kabla ya ujio wa Wajerumani, kwani neno hili muziki lilitokana na ma neno la Kijerumani muzik. Hivyo ni vyema kuelewa muziki kwa maana iliyoko leo ulianza kuingia katika nchi hii kipindi cha Wajerumani. Wajerumani walianzisha shule (hata hilo neno shule linatokana na na neno la Kijerumani, na kupitia shule kulianzishwa brass bendi za shule zilizokuja na muziki mpya ulioletwa na wageni hawa.
Kuingia kwa teknolojia ya santuri ulikuwa ndio mwanzo wa kazi za muziki kuanza kusikika kwa watu wengi kwa wakati mmoja. Kati ya Watanzania wa kwanza kurekodi santuri alikuwa na Siti Binti Sadi ambaye katika miaka ya 20 alisafiri mpaka India kwenda kurekodi nyimbo zake chini ya label ya His masters Voice, aliweza kuuza kiasi cha santuri 700 miaka hiyo na hivyo kuonyesha jinsi alivyokuwa maarufu, ukizingatia uwingi wa watu wa Zanzibar wakati huo, na hasa watu ambao walikuwa na uwezo wa kumiliki chombo cha kupigia santuri.
Radio iliingia wakati wa ukoloni wa Waingereza, ujio wa radio ulibadilisha hali ya matumizi ya kazi za muziki. Kutokana na watu wengi kuwa na uwezo wa kusilikiliza redio, chombo hiki kikawa ni jukwaa muhimu la kutoa taarifa kwa jamii. Na ili watu waweze kusikiliza redio muziki ulikuwa, na hata sasa ni sehemu muhimu. Ingekuwa vyombo vya utangazaji ni gari, basi petroli yake ni muziki. Wakati wa mkoloni sheria ya Hakimiliki ilifuatwa na hivyo radio zililazimika kulipia mirabaha kwa nyimbo ambazo zilitumika katika vipindi vyake, na hili liliendelea hata miaka kadhaa baada ya Uhuru, lakini hili kadri ya mtangazaji mmoja aliyekuwa katika fani hiyo kuanzia miaka ya mwanzo ya Uhuru, Mwalimu Nyerere ndie aliyetoa amri ya kuzuia ulipwaji huo wa mirabaha. Sababu ya kufanya hivyo ni kuwa mirabaha kwa wakati huo ilikuwa inalipwa kwa wanamuziki wa kutoka nchi za magharibu tu, na ulipaji wa aina hiyo ulionekana ni muendelezo wa ukoloni. Bahati mbaya sana, na hatujui kwa nini, amri hii haikuagiza kuanza kulipwa wanamuziki wa hapa nchini. Kuanzia wakati huo mpaka leo vyombo vya utangazaji vimegoma kuwalipa wasanii. Si kwamba viongozi wa vyombo hivi vya utangazaji hawajui kuwa wasanii lazima walipwe bali wameamua kuwadhulumu wasanii na kuwanyima mgao katika mapato ambayo yana mchango wa kazi za sanaa.
Comments