Kwa Mheshimiwa
Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo.
WIZI WA KAZI ZA SANAA.
Mheshimiwa nategemea usalama na unaendelea vizuri na kazi. Mimi si mgeni kwako, nimeshafika ofisini kwako tukaongea mengi sana kuhusu sanaa na hasa wizi wa kazi za sanaa. Ilikuwa ni mapema baada ya wewe kuteuliwa tu kuwa Waziri wa Wizara yetu. Nilitoka ofisini kwako nikiwa na furaha na matumaini, lakini naona muda unakwenda maumivu yako palepale. Nimesikia tena si mara moja hata Mheshimiwa Rais ‘akilaani’ wizi wa kazi za sanaa, lakini kila mara napata picha kuwa serikali haijaamua kumaliza tatizo hili. Mambo mengi yananihakikishia ukweli wa picha yangu hii.
Kwa kweli wengine tuliposikia kuwa safari hii wasanii tuko Wizara moja na Habari tukaelewa tatizo letu la kuibiwa na vyombo vya habari litaisha, miezi imepita na sasa miaka inaanza kuhesabika hakuna dalili zozote za kuonyesha mabadiliko ya unafuu wa wizi huo. Hebu tuanze na TBC, chombo ambacho kiko chini ya Serikali yenyewe.
Kuanzia katikati ya miaka ya 90 wakati huo ikiwa RTD, taasisi hii ilianzisha biashara ya kuuza kanda za muziki unaojulikana kama zilipendwa, pia kulikuwa kunauzwa kanda za ngoma za makabila mbalimbali, na pia kanda za vipindi maarufu kama vile Pwagu na Pwaguzi. Hili halikuwa tatizo , tatizo ni kuwa baada ya kupata fedha za mauzo hayo, TBC hawakushughulika kabisa kukumbuka kuwalipa wasanii ambao ndio walikuwa watunzi, waimbaji, na wapigaji wa vyombo, na waigizaji mbalimbali vya kazi hizo, haihitaji busara kubwa kuona huu ulikuwa wizi wa wazi ukiendelezwa na chombo cha serikali, na kwa vile risiti za serikali zilitolewa, serikali yetu wenyewe ilikuwa inafanya biashara ya Piracy au uharamia wa kazi za muziki. Aibu hii iliendelea hata baada ya kuanza kutekelezwa kwa sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki No7 ya 1999.
Risiti ya manunuzi ya CD |
Ganda la nje la CD zitokazo TBC |
Pamoja na waraka huu naambatanisha picha ya ganda la CD lililotengenezwa bila hata kujali thamani ya kazi zilizomo katika CD hiyo ambayo ina nyimbo za bendi niliyoshiriki kuwemo. Pia naambatanisha nakala ya risiti ya manunuzi ya CD hiyo.
Aibu iliyoje chombo cha serikali kinavunja sheria zilizotungwa na serikali yenyewe. Si hivyo tu, kuanzia mwaka 2003 Regulations kuhusu malipo kwa ajili ya matumizi ya kazi za muziki zimekuwa tayari, ungelitegemea kuwa TBC Radio na TV zingekuwa mstari wa mbele kutekeleza sheria na kuanza kulipa kwa ajili ya matumizi ya kazi za muziki, lakini mpaka leo dhuluma hiyo inaendelezwa na chombo hicho kwa kutumia kazi za wasanii kwa masaa 24 bila kulipa senti tano. Naongelea kwanza TBC kwa kuwa ni Taasisi iliyo chini ya serikali na ilipaswa kuwa ya kwanza kufuata sheria. Usugu huu wa serikali yenyewe kuendelea kuwaibia wasanii ndio unaovipa vichwa hata vyombo vingine vya utangazaji viendelee kugoma kuwalipa wasanii kwa kisingizio kuwa vyombo hivyo vinawa’promoti’ wasanii.
Mheshimiwa tunajua hili liko katika uwezo wako na tunaimani utalitatua bila wasanii kufikia kulazimika kuonyesha hisia za kuchukia kwao.
Swala la wizi wa kazi za sanaa linalindwa na sheria ambayo iko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara Viwanda na Masoko, hili ni tatizo hivyo kuna umuhimu wa kutafuta njia ya kuwa na kamati ya pamoja ya Wizara mbili hizi. Kuna mengi ya ajabu yamekuwa yanaendelea katika kukwamisha kutekeleza kikamilifu sheria hii. Naomba nitoe mifano, mwaka 2001 ilitengenezwa kamati iliyoitwa National Anti Piracy Committee, mimi ndiye niliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati hii. Kamati hii ilitakiwa kutengeza Regulations za kuwezesha kutekelezwa kwa sheria ya Hakimiliki hasa kipengele kilichotaja kuwa ‘kazi zote za muziki na filamu zitatakiwa ziwe na alama ya kuzuia uharamia wa kazi hizo yaani anti piracy device’.
Kazi hii ilifanyika kwa taabu sana kwa mara nyingi kukosa ushirikiano na Taasisi nyingine za serikali ambazo zilikuwa ni wajumbe katika kamati hii, wajumbe walitoka BASATA, COSOTA, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Forodha, Vyama vya Muziki,wafanyabiashara wasambazaji wa kazi za sanaa, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Elimu na Utamaduni na kadhalika. Hatimae kazi hii ilimalikamilika na Regulation hizo kuwa tayari. Regulations zikielekeza kuwa kazi zote halali za muziki na video zilitakiwa kuwa na stempu au sticker kwa mfano wa ile iliyoko katika vinywaji vikali au sigara, japo hii ilikuwa na masharti tofauti kidogo na hizo stempu au sticker zilizotajwa, na hata jina ikapewa ikaitwa HAKIGRAM. Regulation hii ilitakiwa kutiwa saini na Waziri wa Viwanda na Biashara wakati huo ili ianze kazi, Waziri husika kwa wakati huu akiwa Mheshimiwa Ngasongwa. Mheshimiwa Waziri alifanya kazi yake na alitia saini regulation hiyo ili iweze kutangazwa katika gazeti la serikali na kuanza kufanya kazi, cha ajabu nakala zote zilizotiwa sahihi zilipotea hapo hapo Wizarani!!!!!!!!. Baada ya Uchaguzi 2005 Mheshimiwa Waziri Karamagi alilazimika kutia saini nakala nyingine, na ndipo kilipoanza kizungumkuti cha serikali kutokutoa fedha za kuwezesha kuanza kununua sticker za kwanza za kuwezesha kutekeleza zoezi hilo. Na mpaka leo zoezi hilo halijafanyika. Kama nilivyosema kuna mengi ya ajabu yanayoendelea katika swala la ulinzi wa kazi za sanaa. Miaka miwili iliyopita zikaweko habari kuwa swala hili la kumaliza tatizo la wizi wa kazi za sanaa limeanza tena kushughulikiwa na Ikulu. Kwa mshangao afisa moja aliyejitambulisha kuwa anatoka TRA aliniomba nimueleze matatizo katika tasnia ya muziki kwani katumwa na Ikulu ashughulikie matatizo hayo na kuweza kuanzisha sticker kwenye kila kazi ya sanaa, na kuwa yeye ni mtaalamu sana hata Nigeria walimuita yeye akawasaidia!!!!!nilishangaa kwani hilo jambo lilikwisha tengenezewa hata Regulation ila kutekelezwa kwake ndio kilikuwa kumekwama hivyo sikuelewa kwanini jambo ambalo lingekamilika kwa kupiga simu COSOTA na kupata maelezo na kuanza kutekeleza. Pia hatukuweza kuelewana na Mheshimiwa yule kwa kuwa kwanza alikuwa amekuja sehemu niliyokuwa napiga muziki na ilikuwa ni zaidi ya saa 6 usiku, na pili alikuwa amelewa kwa hiyo ilikuwa ni kazi bure kuelewana nae, nilimwomba anitafute wakati akiwa mzima sijamwona mpaka leo.
COSOTA ndicho chombo ambacho kinashughulikia mambo ya Hakimiliki kwa mujibu wa sheria ya nchi yetu. Katika Bodi iliyoisha muda wake 2006, ambapo pia nilikuwa mjumbe tuliona kuna haja ya kufanya marekebisho mengi katika chombo hiki, ikiwemo kurekibisha sehemu mbalimbali za sheria iliyopo ya Hakimiliki, ili kuwezesha kuweko na ulinzi unaofaa wa haki za wasanii. Jambo hili lilianza kutekelezwa. Katika mkutano mkuu wa COSOTA wa mwaka 2007 ambao ulikuwa ni Mkutano Mkuu wa mwisho kwani haujafanyika mwingine tena, ilichaguliwa Bodi mpya, bodi hii hupitishwa na Waziri wa Viwanda na Biashara baada ya yeye kuteua Mwenyekiti wa Bodi. Jambo la kushangaza miezi kadhaa ilipita hadi kufikia Bunge la Bajeti la mwaka 2008, Mheshimiwa Waziri alikuwa hajapitisha Bodi hiyo, pamoja na kuulizwa swali hilo wakati wa kutoa makadirio ya Bajeti ya WIzara yake Mheshimiwa Waziri alijibu kuwa jambo hilo liko mezani kwake, ushahidi wa Hansard utaonyesha hilo. Hata lilipofika Bunge la Bajeti la mwaka unaofuata 2009, bado Mheshimiwa Waziri alikuwa hajakamilisha kazi hii na aliulizwa tena na Mheshimiwa Martha Mlata(MB), ambaye ndiye aliyekuwa kamuuliza 2008, akajibu kuwa hilo amekwisha lishughulikia, lakini kwa mshangao majina ya wajumbe Bodi yaliyopitishwa si yale ambayo wanachama walichagua kwenye Mkutano Mkuu wa 2007, bali lilikuwa chaguo la Mheshimiwa Waziri.
Huu ni mwaka 2011 mwishoni karibu miaka mitano COSOTA haina Board, Je, ilikuwa inapataje ruzuku? Audited reports zilikuwa zinapitishwa na nani?
COSOTA hukusanya fedha kwa niaba ya wasanii bila Bodi iliyoteuliwa na wasanii kutakuwepo vipi ushahidi kuwa fedha zao zinatumika kadri ya mujibu wa Katiba ya COSOTA. Mipango yote iliyokuwa imeanzishwa na Bodi iliyopita imepotelea wapi? Mheshimiwa narudia tena kuna mambo ya ajabu sana katika utekelezaji wa Serikali katika kulinda haki za wasanii wa nchi hii.
Utafiti uliofanywa karibuni(2009) unaonyesha katika tasnia ya MUZIKI peke yake mapato kutokana kazi hizi ni Tshs Bilioni 78. Pia ikaonyesha ni asilimia 12 tu ya wanaopata fedha hizi wanaolipa kodi. Serikali ingepata kiasi cha Bilioni 18 kutokana na kodi. Mheshimiwa ukikumbuka kuwa Bajeti ya Wizara yako haifiki hata Bilioni 7, nadhani unaweza kupata picha ya ukubwa wa ukwepaji wa kodi, na hapa hakujaguswa sekta inayokuja juu sana ya filamu. Kuanza kufanya kazi zile sticker kungewezesha serikali kupata takwimu ambazo zingewezesha kukusanya kodi stahili. Pia wasanii wangeweza kupata stahili yao ya malipo kutokana na kazi zao. Tumeona viongozi wakuu mkishiriki katika uzinduzi wa album mbalimbali za wasanii, je mnajua kuwa mnaemfanyia promotion si msanii ila msambazaji wa kazi ambaye kama tunavyoona hata kodi halipi?
Mheshimiwa kwa kuwa wasanii tuko chini ya Wizara yako tafadhali sema neno moja tu mambo yabadilike. Pia tunaomba nyinyi Viongozi wa juu kabla hamjatoa matamko kuhusu wizi wa kazi za sanaa tungewaomba mpate taarifa kamilifu kuhusu sekta hii. Kutegemea kupata taarifa sahihi kutoka kwa mfanya biashara anaefaidi mapato kutoka kwa kazi za wasanii na kutegemea atakuwa kweli ni jambo ambalo linashangaza sana
Ni mimi mwanamuziki
John Kitime