Dushelele wa Ally Kiba na heshima yake katika bendi

Katika muziki kuna njia ya wanamuziki kupeana heshima kutokana na ubora wa kazi au utalaamu. Mara nyingi ukiingia katika onyesho la muziki utasikia wanamuziki wakitambua kuweko kwa mwanamuziki mwenzao aidha kwa kumtaja au kwa kumkaribisha jukwaani ili 'atoe salamu za kisanii'. Hii inaweza kuwa kwa mwanamuziki kushiriki katika wimbo unoendelea au kupiga au kuimba wimbo wake ambao anaona unamtambulisha uwezo wake. Njia nyingine ni kwa wanamuziki kuurudia wimbo wa wanamuziki wengine. Katika nyimbo za wanamuziki wa kizazi kipya, wimbo wa Ally Kiba wa Dushelele ndio wimbo ambao bendi nyingi zimeanza kuupiga katika maonyesho yake katika kipindi hiki. Katika mizunguko yangu nimekwisha sikia bendi tatu zikiupiga wimbo huu vizuri na  katika bendi moja, mpiga solo hutangazwa kuwa yeye ndiye aliyepiga gitaa studio wakati wa kurekodi nyimbo hiyo. Ni wazi ni heshima kubwa kwa Ally Kiba katika jamii ya wanamuziki.

Comments