Str8t Muzik |
Anti virus wakionyesha vitabu vya maisha ya Mbunge Joseph Mbilinyi |
Jukwaani Mheshimiwa Joseph Mbilinyi wa Mbunge wa Mbeya mjini na Mheshimiwa John Mnyika Mbunge wa Ubungo. |
Jana tarehe 26 November 2011 kulifanyika maonesho mawili makubwa ya muziki. Str8t Muzik Inter-College Festival 2011 na lilioitwa Tamasha la Anti Virus. Maelfu ya watu, walikusanyika katika viwanja vya Leaders na viwanja vya Ustawi wa jamii. Kuna watu walitoka hata nchi za jirani kuja kuhudhuria shughuli hizi. Siku hii itakumbukwa pia katika uwingi wa watu waliohudhuria katika show za muziki. Str8t Muziki pamoja na kuwa na wasanii wanachi ilikuwa pia na wasanii kutoka nje Faboulous na DMX, japo DMX hakutokea, kuna maelezo tata kwa nini hakutokea. Tamasha la Anti Virus lilikuwa ni la wasanii wazalendo na wengi ambao wamesha wahi kuwa majina makubwa nchini, na wengine kutosikika kwa muda mrefu, lakini ni wazi umati wa watu ulionyesha kuwa pamoja na vyombo vya utangazaji kuwafuta katika anga zao bado wamo kwenye mioyo ya watu wengi uwingi wa watu katika tamasha hili lililokosa udhamini ni ushahidi tosha wa kisayansi kwa hilo.
Kufanikiwa kwa matamasha makubwa yenye watu wengi kwa wakati mmoja kunafungua ukurasa mpya katika tasnia ya muziki. Kwa muda mrefu sana hili lilionekana kuwa haliwezekani, kabla ya hapa ungeweza hata kunyimwa kibali na ofisi husika ikiwa kuna kibali kilichokwisha tolewa kwa ajili ya tamasha jingine.
Matamasha yote mawili yakuwa katika wilaya ya Kinondoni na yote kufanikiwa kupata watu wengi hivyo basi ni wazi kuwa kuna uwezekanao wa kuweko hata matamasha zaidi bila utata wala kuingiliana ikiwa kila tamasha lina mtazamo wake. Kwa miaka mingi kumekuweko na ‘roho mbaya’ ya kufanyiana fujo ili kusiweko na shughuli zaidi ya moja kwa siku, kuna taarifa za kampuni kukodisha kumbi zilizowazi au zilizotegemewa kutumika ili tu kujaza nafasi hata kama zitabaki tupu. Kampuni moja imekuwa ikilalamikiwa kuwa ilifikia kupandisha mara mbili bei ya ukumbi maarufu ili wasio na uwezo wasiutumie kwa shughuli hasa za muziki.
Kama nilivyosema hapo juu, Tamasha la Anti Virus lilikuwa halina udhamini wa kutoka kati ya makampuni yoyote makubwa yenye kawaida ya kutoa udhamini kwenye shughuli za sanaa, lakini zaidi ya watu alfu kumi walihudhuria tamasha hilo, hiyo ni kurasa nyingine katika tasnia hii, inaonyesha kuwa kunaweza kupatikana na mafanikio katika maonyesho bila udhamini, na pia ni fundisho kwa makampuni yanayodhamini kuwa wakati umefika wa kuwa na mtizamo chanya hata kwa watayarishaji wa maonyesho wapya. Limekuwa tatizo la muda mrefu kuwa kuna watu au taasisi ambazo zimehodhi nafasi ya kupata udhamini wa shughuli za sanaa kwa imani kuwa hakuna mtu au taasisi nyingine inayoweza kufanikisha kazi hizi.
Si rahisi kukuta wanasiasa wakishiriki na wananchi katika burudani za kawaida, labda iwe wakati wa kampeni, au mara nyingine kumtembelea vikundi na kumwaga pesa ili kutajwa kwa kusifiwa na wanamuziki. Kuwepo kwa wabunge kadhaa na pia Mwenyekiti wa CHADEMA katika jukwaa la wasanii ni jambo la kutia moyo kwa wasanii. Pamoja na kuwa ni karata nzuri ya kisiasa kwa viongozi hao lakini pia ni dalili za viongozi kuelewa umuhimu wa shughuli mbalimbali za wananchi. Big up CHADEMA kwa kulitambua hilo.
Comments