Kumbukumbu ya Kifo cha Franco 12 Oktoba 1989




François Luambo Luanzo Makiadi  alizaliwa 6 July 1938, katika kijiji cha Soni Bata magharibi mwa jimbo la Bas Zaire huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Wakati bado mchanga wazazi wake walihamia jiji la Leopodville ambalo sasa linaitwa Kinshasa. Baba yake aliitwa Joseph Emongo alikuwa mfanyakazi wa shirika la reli wakati huo mama yake alikuwa akiuza maandazi sokoni. Alipofikia umri wa miaka saba alitengeza gitaa lake akawa analipiga kwenye genge la mama yake ili kuita wateja.. Mwanamuziki maarufu Paul Ebengo Dewayon ndie aliyegundua kipaji cha mtoto huyu na kuanza kumfundisha rasmi namna ya kupiga gitaa. Mwaka 1950 akiwa na umri mdogo wa miaka 12 alichukuliwa rasmi kama mwanamuziki wa bendi ya Watam iliyokuwa inaongozwa na Dewayon. Kipaji chake kiliwashangaza wengi hasa kwa vile alikuwa akionekana umbo lake kubwa kama gitaa analolipiga lakini akiwa analipiga kwa umakini mkubwa. Akiwa na miaka 15 alirekodi nyimbo yake ya kwanza Bolingo na ngai na Beatrice (Mapenzi yangu kwa Beatrice). Wimbo huu aliutunga alipojiunga na bendi iliyokuwa inamilikiwa na Studio za Loningisa. Kiongozi wa bendi hiyo Henri Bowane ndie aliyeanza kufupisha jina la mwanamuziki huyu na kumuita Franco, jina alilokuja kujulikana nalo maisha yake yote. Mwaka 1955 alianzisha bendi akishirikiana na Jean Serge Essous bendi ilizinduliwa katika ukumbi wa OK Bar, hatimae bendi ilichukua jina la OK Jazz kwa heshima ya bar ambapo ilizinduliwa.Katika muda mfupi ikiwa na mwimbaji Vicky Longomba(Baba yake Lovy Longomba) walianza kuwa bendi pinzani ya bendi kongwe ya African Jazz iliyokuwa inaongozwa na Grand Kalle. Mwaka 1958 Essous na Franco kuwa kiongozi na mtunzi mkuu wa kikundi alichokuja kukijenga kwa kuanzia watu 6 hadi kufikia  watu 30 kwenye mwaka 1980. Franco mwenyewe alikuwa anasema OK Jazz iliweza kutoa album 150 katika miaka 30 ya bendi hiyo.Mwaka 1958 Franco alifungwa kwa mara ya kwanza kwa kosa la uendeshaji mbaya wa gari siku ya kutoka kwake jela ilikuwa kama shujaa katoka vitani. 1960 Vicky Longomba aliacha bendi. Lakini wakati huo Kongo ilikuwa kwenye vuguvugu za kutafuta uhuru na nchi ilikuwa si shwari Franco akahamia Ubelgiji. Baada ya Mobutu Sese Seko kushika nchi na kukawa na amani  katika nchi iliyoitwa sasa Zaire franco alirudi 1966. Akashiriki katika Tamasha la Sanaa Za Afrika lililofanyika Kinshasa 1966 na Franco akawa kipenzi cha serikali ya Mobutu.
Franco hakuwa tu mwanamuziki mzuri bali pia aliendesha vizuri sana biashara zake za kurekodi na kampuni alizozianzisha wakati huo. Alikuwa na lebo kama (Surboum OK Jazz, Epanza Makita, Boma Bango and Éditions Populaires). Katika miaka ya 70 muziki wa Kongo ulishika kasi sana Afrika na Franco akiongoza jahazi kwa nyimbo kama Infidelité Mado,  na akaendeleza kupiga mitindo mbalimbali kama Bolelo na muziki uliotokana na ngoma za asili toka Kongo zikichanganywa na mapigo kutoka Cuba na kuanza upigaji wa gitaa uliokuja itwa Sebene.
 Mwaka 1970 Franco alimpoteza mdogo wake ambaye nae alikuwa mpiga gitaa mashuhuri Bavon Marie-Marie Siongo ambaye alifariki katika ajali ya gari baada ya kuwa akiendesha gari kwa hasira baada ya ugomvi na kaka yake wakigombea msichana ambaye nae alipata kilema kutokana na ajali hiyo. Lilikuwa pigo kubwa kwa Franco kwa miezi kadhaa aliaacha hata kupiga muziki. Baada ya hapo OK Jazz ilibadili jina na sasa kuitwa TP OK Jazz na mwaka 1973 kutoa kibao kingine kilichotikisa Afrika ,AZDA.  Wimbo huu kwanza ulirekodiwa kama tangazo kwa ajili ya  kampuni ya Volkswagen VW. Mahusiano yake na Mobutu yalikuwa na mawimbi mara wakipatana mara wakikosana kutokana na Franco kuwa anatumia nyimbo zake kukosoa serikali ya Mobutu. 1970 Franco alikuwa ni Rais wa wanamuziki wa Kongo na pia kuajiliwa na kampuni ya kugawa mirabaha ya wanamuziki. Aliendelea kutajirika kwa kuweza hata kunua ardhi nchini Ufaransa, Ubergiji na Kongo, na kuwa na nightclub 4 kubwa kuliko zote Kinshasa kwa wakati huo na kufanya club ya
 Kuwa ndio makao makuu yake. Hapo ilijengwa studio kubwa, office na apartment za kuishi kadhaa. Mwaka 1978 alitiwa mbaroni  tena baada ya kugundulika kuwa alikuwa anasambaza nyimbo zenye matusi ambazo hakuzipitisha katika  kamati ya kuchunguza mashahiri kama ilivyokuwa kawaida wakati ule. Kufikia kipindi hiki TPOK Jazz  ilikuwa kubwa kiasi iliweza kumeguka kuwa mbili moja ikifanya kazi Afrika wakati nyingine ikiwa inafanya maonyesho Ulaya. !983 Franco alifanya maonyesho kadhaa Marekani lakini hayakufanikiwa haijajulikana mpaka leo sababu za kushindikana huko. Katikati ya miaka ya 70 Franco alibadili dini na kuwa Muislam na kupewa jina la Abubakkar Siddiki, japo hakuonekana kufuata taratibu zozote za Kiislamu na akaendelea kuitwa Franco. 1980, Franco alitajwa kama ndie Grand Master wa muziki wa Kongo na serikali yake, ghafla na nyimbo zake nyingi zikaanza kuwa zinasifia utawala ulikuweko madarakani. 1985 Franco alitoa wimbo ambao uliuza kuliko nyimbo zake zote
, Mario,  ambao ulikuwa ni hadithi ya mwanaume kijana  ambae alikuwa anategemea akina mama watu wazima wamlee. !987 zilianza habari kuwa Franco anaumwa sana, na kwa mwaka ule alitoa wimbo mmoja Attention Na SIDA (Jihadhari na UKIMWI), wimbo huu ukaanzisha maneno kuwa pengine Franco kasha upata ugonjwa huu. Franco akawa taratibu anakosekana kwenye shughuli za bendi nayo ikaanza kumeguka kutokana na kutokuwa na uongozi thabiti. Franco tena akarudi kwenye dini yake ya awali ya Roman Catholic. Tarehe 12 Oktoba 1989, Franco alifariki katika hospitali moja Ubelgiji. Mwili wake ukarudishwa Kongo, sanduku likiwa limefunikwa bendera ya Taifa lake na kupitishwa katika mitaa ya Kinshasa na kuagwa na maelfu ya wapenzi wake. Serikali ikatangaza siku 4 za maombolezo ambapo redio ya serikali ilipiga nyimbo za Franco tu. Franco alizikwa tarehe17 Oktoba 1989. Alifariki akiwa na miaka 51. Mumgu amlaze pema peponi

Comments