Count down ya nyimbo 50 toka Clouds Radio


Clouds Radio imeanza taratibu ya kupiga nyimbo moja kwa kila siku kwa siku 50 hadi kufikia siku ya kilele cha kumbukumbu ya miaka 50  Uhuru wa  nchi yetu. Leo nimeusikia wimbo wa  UDA Jazz Band wana Bayankata. Bendi hii iliyokuwa mali ya shirika la Usafiri Dae es Salaam (UDA), usafiri ambao ulikuwa maalumu kwa ajili ya kusafiri watu katika jiji la Dar, walipata umaarufu sana katika wakati wake wakiwa na wanamuziki mahiri waliopitia huko kama Freddy Benjamin ambae baadae alikuja kukamilisha maisha yake Vijana Jazz, Maneno Uvuruge mpigaji maarufu wa gitaa ambae kwa wakati huu yuko katika safari USA wakiwa na King Kiki, na pia huko alipitia Komando Hamza Kalala, ambae pamoja na yeye kuwa mwanamuziki mahiri pia ndie baba mzazi wa wanamuziki maarufu , Kalala Junior na  Totoo Kalala. Hamza Kalala ndiye mtunzi na mpiga solo katika wimbo wa leo katika count down hiyo ya kuelekea siku ya Uhuru. Wimbo huo si mwingine bali ni ule- Tulizaliwa wote. Sehemu ya mashahiri ya wimbo huo ni haya;
Tulizaliwa wote kijiji kimoja,
Lakini ulishindwa kunioa kwa sababu,
Ulisema sina tabia nzuri eeh
Sasa nimeolewa kaka,
Unaanza kuleta chokochoko,
Kujifanya wewe unazo pesa nyingi univurugie.
Wenyewe tumetulia.
Kama ni tabu ni zetu,
Kama unachoringia ni pesa kaka,
Pesa si msingi.
Chorus
Ninachojali ni utu, pia na heshima kwa mume wangu.

Comments

Anonymous said…
Nakumbuka wimbo huu ndiyo ulikuwa wimbo wetu maarufu nilipokuwa ktk bendi ya Uda Jazz 1981,Tuliuita "Nachunga heshima"Nilijiunga baada tu ya Hamza Kalala kuhamia Matimila,ingawa yeye Hamza ambaye ndiye alikuwa mtunzi wa wimbo huu alishaondoka Uda lakini watu walizidi kuupenda wimbo huu kila tulipokuwa tukipiga,huyu nguli ni mtunzi mzuri sana na ana bahati kila wimbo autungao huwa hit.Nkumbuka enzi hizo kumbi zetu maalum tulizokuwa na mashabiki we ngi ni Casanova(Buguruni)upande wa kushoto kama unatokea Ilala,halafu
huko huko Buguruni upande wa kulia ilikuwepo Super Fanaka bar,nadhani hapa ndipo maeneo ilipo club Y2k kwa sasa,pia Kigogo ilikuwa Kigogo lodge na Kigogo CCM,Kawe ilikuwa Salama bar,Mikocheni wakati huo ni kijiji tu ilikuwa Makonde bar,na Msasani ilikuwapo Mpanda bar na baadae ikafunguliwa nyingine Mkirikiti bar.Kama kuna watu wenye kumbukumbu watakumbuka vizuri historia ya viunga hivi vya starehe.Pia bendi tulizokuwa tikipishana nazo humo ni Dar International chini ya uongozi wa jabali Marijani,na Biashara Jazz ya Juma Ubao,ilikuwa raha sana maana ushindani pia ulikuwa mkubwa.
hii ndiyo ilikuwa enzi ya wana "Bayankata"
Abbu Omar,Prof.Jnr(Mwanamuziki)Tokyo,Japan.