Vituko vya baadhi ya wanamuziki wetu wakiwa nje ya nchi

Ni jambo la kusikitisha lakini kuna wanamuziki wengi wa Tanzania wamepoteza bahati ambazo si tu zingewaweka katika jukwaa la kimataifa, bali hali hiyo ingeweza kuwavuta mapromota wengine waKimataifa kuangalia kwa jicho la makini zaidi waimbaji wa Tanzania. Blog hii inaona ni vyema ingeongelea matukio mbalimbali ya wanamuziki wa Tanzania na vituko vyao jinsi vinavyowakosesha bahati wao na wadau wengine.
1. Mwanamuziki wetu mmoja maarufu alikuwa kapewa nafasi ya kurekodi katika studio moja wakati yuko katika tour huko Ulaya, akawa kakaribishwa katika nyumba ya Mtanzania fulani apumzike kungoja muda wa kwenda studio, kwa vile alikuwa peke yake katika nyumba alianza kunywa kila kila pombe aliyoiona humo ndani, bia za kopo za 7.5%alcohol katoni zima alimaliza peke yake, pombe kali aina mbalimbali alizigida, hatimae akazimika. Wenyeji wake walipofika kumchukua kwenda studio ilishindikana maana kila njia waliojitahidi kumsaidia azinduke ilishindikana ukawa ndo mwisho wa mpango wa kumrekodi huko. Bahati mbaya msanii huyo hata hapa nyumbani umaarufu wake umeshuka, lazima anajutia ulevi wake ambao ulimfanya akapoteza bahatiya kutoka kimataifa.
2. Mwanamuziki mwingine alitoa wimbo ambao ulimletea umaarufu sana, kwa bahati promoter mmoja wa kimataifa akausikia kupitia blog moja. Akafanya taratibu za kuuzungusha kwenye kampuni husika na kila kitu kikawa tayari, hata fedha kwa kurekodi upya na kutengeza video zikapatikana. Baada ya kuwasiliana na mwenye blog, waliweza kupata mtu ambaye  anaemfahamu huko Ulaya. Jamaa yake alieko Ulaya alimpigia simu mwanamuziki wetu na kumwambia kuhusu habari hiyo nzuri, na kumtaarifu kuwa promota atampigia. Kwa kujua kuwa mwanamuziki huyo si mzuri sana kwa lugha ya Kiingereza alishauriwa akishapigiwa amruhusu promoter aendelee na mazungumzo na mipango kupitia huyo mwakilishi wake wa Ulay. Superstar alipopigiwa mara ya kwanza akajibu, 'Niko studio nipigie baadae'. Jibu hili alilirudia kila alipopigiwa na hatimae akawa hapokei simu. Hata alipotumiwa txt message aliipuuza. Promoter huyu ambaye amekwisha weza kuwafikisha wasanii kadhaa kwenye kumi bora nchi za Ulaya akatamka kuwa kafunga faili maana msanii hayuko serious. 

3. Mwimbaji mwingine alikaribishwa Uingereza alipotua huko, aligoma kufanya mazoezi mpaka anunuliwe bangi. Promoter alichanganyikiwa maana anasema hakujua hata hiyo bangi inanunuliwa wapi. Na msanii kagoma mazoezi mpaka anunuliwe bangi. 
4. Mwanamuziki mwingine alifuatwa na watu wenye studio moja toka nchi moja ili akarekodi nchi nyingine. Walilazimika kumfuata ili kumpunguzia usumbufu wa safari kutokana na hali kuwa nchi hizo hazitumii Kiingereza. Mwanamuziki wetu ambaye atayari alikuwa ameshasaini makubaliano ya kurekodi, akapata mpenzi katika onyesho lake la mwisho kabla ya safari. Akawagomea waliomfuata na kuwambia kuwa analala kwa  mpenzi. Kesho yake hakutokea waliomfuata wakarudi mikono mitupu.
5. Mwanamuziki wetu mwingine alipigwa sana na mpenzi wake katika hoteli aliyofikia hadi akashindwa kufanya kazi kutokana na kuvimba uso na pia kuwa katika hali ya kutapika hovyo kutokana na kipigo. Akaishia kuimba nyimbo 3 tu show nzima.

Comments

Anonymous said…
Ulimbukeni ndio unatuponza vijana wa kitanzania. Tunadhani kuwa ni kwenda na wakati kumbe ni ujinga mtupu. Kila mara wanamziki vijana wanalalamika kuwa hawapati mapato mazuri wanadhulumiwa n.k. Kumbe hawajui kuwa ni wao ndo chanzo cha kujifanya kuwa wanaelewa sana kumbe hamna kitu..