Seleman Kasaloo Kyanga kuzikwa kwa taratibu za dini yake

Mwanamuziki Selemani Kasaloo Kyanga ambaye alikuwa pacha wa Kyanga Songa walizaliwa Kongo mwaka 1957. Walikuwa ni nyota katika bendi zote walizopitia nchini zikiwamo, Matimila, Makassy, Maquis, Sambulumaa, Ngorongoro Heroes, Tancut Alimas, Sandton Sound, Kalunde Band  na bendi nyingine nyingi . Kasaloo aliyetangulia kuingia nchini akifuatana na Skassy Kasambula mwaka wa 1980, aliweza kutingisha anga za muziki kuanzia pale aliposikika kwenye nyimbo zilizorekodiwa na Super Matimila. Kyanga nae akisindikizana na Issa Nundu walifuatia na sauti zao kuanza kusikika katika recording ya Orchestra Makassy na zile nyimbo Olenge,Bembeya,na pia kuimba na Masiya Radi katika nyimbo Tunagombana Bure. Kyanga alifia Kenya na Kasaloo amefariki jijini Dar es Salaam kutokana na mapafu yake kujaa maji. Alikuwa Sandton Sound Band aliyojiunga nayo akitokea Kalunde Band. Kamati ya msiba wa Kasaloo ikiongozwa na King Kiki yenye wajumbe Mzee Mapili, Mzee Manyema, Mbombo wa Mbomboka, Deo Mwanambilimbi, Mzee Jerome, Matunda, Mzee Peter George na John Kitime, imetoa ratiba ifuatayo.

Saa 3-5...Kutayarisha mwili katika hospitali ya Mwananyamala
Saa 7-9 Kuagwa na dua nyumbani kwa marehemu Tiptop Manzese
Saa 10 Mazishi Sinza Makaburini.
Marehemu ameacha wake wawili na watoto 6.
Seleman Kasaloo alibadili dini na kuwa Muislamu katika miaka yake ya mwisho ya maisha, na kutoa wosia kuwa azikwe kwa taratibu za dini yake ya Kiislam.

Comments

KUBIHA Ramadhani said…
RIP Kasaloo hakika mipango ya mungu imetimia hatutaacha kukukumbuka wapenzi wa muziki TANZANIA nakumbuka miaka ya 1988 mapacha wakiwa na TANCUT ALMAS walifunika sana na kutukosha nyoyo zetu , pumzika kwa amani mbele yako nyuma yetu, inshaalah mola akupunguzie madhila ana adha ya kaburi.