Takriban miezi miwili iliyopita Tanzania ilimpoteza kimyakimya moja ya wapiga ngoma bora Tanzania. Mwanamuziki Abdallah Chembe. Chembe ambaye pamoja na vikundi vingine alipitia kwa muda mrefu katika kikundi maarufu cha Muungano Cultural Troupe akiwa msanii wa fani nyingi ikiwemo uigizaji, fani aliyoimudu vizuri kiasi cha kuigiza katika mchezo wa redio akijulikana kama Mzee Bom, jina lililomkaa mpaka alipofariki. Niliwahi kusafiri na Mzee Chembe kwenda kufanya maonesho nchini Ujerumani mwaka 1994, tukiwa pamoja na Mzee Small wa Ngamba, Shaaban Yohana Wanted, Baker Semhando, Abdallah Mgonahazelu, wakati huo Mzee alikuwa na uwezo wa kuona. Kutokana na ugonjwa ambao haukutibika alipoteza uwezo wake wa kuona katika miaka ya 90. Hilo halikumfanya aache sanaa, alijiendeleza kwa kufuata nyayo za mzee Nyunyusa na kufiki kuweza kupiga ngoma 17 kwa wakati mmoja.
Jambo jingine alilokuwa nalo Mzee Bom ni nia ya kurekodi muziki wake kwa kutumia vyombo vya kiasili, alifanya hivyo kwenye mwaka 2000, nyimbo nzuri sana lakini vyombo vya habari hapa vikafanya uchawi wao na kuwanyima wananchi haki ya kuzisikia nyimbo hizo mpaka alipofariki. Vijana aliowaacha wameamua kuendeleza kikundi chao TEN BEST, kwa kufuatia nyayo za Mzee Bom. Ni raha kuwasikiliza wasanii hawa, mfano mwingine wa utajiri tulionao nchini Tanzania. Sikiliza mazoezi hapa.
Comments
Abbu Omar,Prof.Jnr(Mwanamuziki)Tokyo,Japan.