VITUKO VYA VIONGOZI WA MABENDI-sehemu ya kwanza


Bendi huwa ni kundi la watu, na ili mambo yaende vizuri huwa na viongozi mbalimbali. Katika maisha yangu ya kuwa mwanamuziki nimekwishakutana na viongozi wa aina nyingi sana, ambao kwa wapenzi wa muziki huonekana watu wenye busara na wastaarabu lakini kwa wanamuziki watu hao wanaweza kuwa ni Ze Komedi kwa wanabendi na mara nyingine watu wa kutisha sana. Nikisema viongozi hapa nina maana kuanzia wenye bendi, maarufu siku hizi kama Wakurugenzi, zamani walikuwa wanafahamika pia kama Wenyeviti kwa kuwa bendi nyingi zilikuwa katika mfumo wa klabu. Pia kuna viongozi waliojulikana zamani kama Makatibu wa bendi ambao nafasi yao siku hizi imechukuliwa na mameneja wa bendi. Pia kuna Band leaders, wanamuziki ambao huongoza bendi lakini sio wenye bendi, hawa walijulikana kwa majina kama Vie, hasa wakiwa Wakongo, Marais wa Bendi (prezida), Mkuu wa bendi na kadhalika.
Vituko nitakavyosimulia ni vile ambavyo nimeshuhudia na vile ambavyo nimehadithiwa lakini nimeweza kupata ushahidi kuhusu tukio. Labda nianze na wale wakurugenzi ambao ndio wenye vyombo halafu wanataka kuwa wanamuziki. Hawa kwa kweli ni kundi la wasumbufu sana kwa uzoefu wangu. Miaka mingi iliyopita mheshimiwa mmoja aliweza kununua vyombo ambavyo kwa siku hizi visingefaa hata kwa mazoezi lakini viliwezesha mimi na wanamuziki wenzangu tukawa tunamuabudu mheshimiwa huyu. Yeye alikuwa na baa kadhaa na akaruhusu tuwe tunafanya mazoezi katika baa yake mojawapo, sijui kwanini ghafla nae akataka kujifunza kupiga gitaa la rhythm, kwa kweli mazoezi yalikuwa  yanasimama mara alipofika, maana alichukua gitaa na kuanza kuomba aonyeshwe namna ya kupiga. Nimpe sifa kwamba hakutusumbua bure akaweza kupiga kwa mbali wimbo mmoja wapo na hapo ndipo akadai lazima awe anaipiga katika maonyesho tuliokuwa tunafanya, na wakati huo kulikuwa na mtindo wa kunyamazisha gitaa la solo ili lile gitaa la rhythm lisikike, mheshimiwa hakuwa hata anataka wimbo ufuatiliwe kwa mpangilio, alitoa amri kuwa katikati ya wimbo akikonyeza tu basi aachiwe nafasi awe anapiga rythm awe anasikika peke yake. Haikuchukua muda mrefu tukamkimbia nakumuacha na vyombo vyake. 
 Kuna Mkurugenzi mmoja wa heshima sana aliwahi kuchukua bendi yake ikaenda kwenye ziara nchini Kenya, na kusafiri miji mingi sana, na alipoona kuwa mapato ni kidogo, basi akanunua sufuria ili wanamuziki wawe wakijipikia chakula kwa unga na maharage aliyokuwa akinunua, na malazi yalikuwa kwenye jukwaa mara baada ya kumaliza muziki. Hakukuwa na malipo mengine, bendi ikaanza kusambaratika hukohuko Kenya, kwa kweli hata nae aliweza kurudi nchini kwa chupuchupu, lakini hakubadilika kwa kuwa nilipiga bendi ya kiongozi huyo, nakumbuka siku ambayo mimi na wenzangu wawili tuliacha bendi band. Ilikuwa sikukuu ya Idd, na kulikuwa na kawaida ya bendi kupiga muziki kuanzia saa 9 mchana mpaka saa 2 au 3 usiku. Tukiwa tunaendelea na muziki katika ukumbi wa Makonde Bar Mikocheni, kiasi cha saa moja na nusu usiku kiongozi akaingia na kundi la rafiki zake na wasichana wao, wakacheza sana ilipofika saa 2, akatuambia tufunge muziki, akampa kila mtu shilingi 3 twende kula kwa mama ntilie jirani kisha tuanze tena muziki ambao uendelee mpaka saa 7 usiku. Kwa kuwa kulikuwa hakuna matangazo ilikuwa kama ni party tu ya kiongozi na watu wake, tatizo lilizidi baada ya dansi kukawa hakuna usafiri wanamuziki tukalazimika kutwanga mguu kila mtu kwake. Kesho yake tukamrudishia yunifom za bendi.
 Viongozi wengine hupatikana katika njia za ajabu sana, kuna wakati tulikuwa na kikundi ambacho kilikuwa kimekabidhiwa vyombo na tawi la  TANU Youth League, tatizo letu lilikuwa mahala pa kufanya mazoezi, bwana mmoja ambaye alikuwa mganga wa kienyeji akatupatia nafasi katika nyumba yake aliyokuwa kapanga kwa ajili ya shughuli zake za uganga. Ilikuwa na nafasi kubwa natuliweza kufanya mazoezi, ukarimu huu ulirudishwa kwa sisi kumteua kuwa mlezi wa bendi. Loh mheshimiwa haraka akaanza kutuingiza kwenye mtego wa ushirikina kwa maelezo kuwa kwa kuwa vyombo vimelala kwake lazima tuanze kuoga dawa zake kukwepa wabaya wake wasiopenda mafanikio ya kazi zake na za rafiki zake. Ilifika wakati tukaanza kumpa chochote tulichopata kwa kuogopa kulogwa nae. Salama yetu ilikuja siku alipomtaka binti moja mapenzi na binti alipokataa akatoa nyoka aliyekuwa anatembea nae mfukoni akamtisha naye, binti akakimbilia polisi, mheshimiwa akajakubebwa juu juu japo nyoka alimuachia ili kukosekane ushahidi, nasi tukahamisha vyombo siku hiyo hiyo.
Nakumbuka bendi moja ambayo tulianza wote tukiwa marafiki, tukila pamoja ugali ambao ulikuwa ukipikwa na fundi mitambo wakati mazoezi yanaendelea, bila kujali kiongozi wala mbeba spika. Kiongozi wetu alipatikana kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa na uhusiano na mwenye vyombo, lakini wote tulijisikia kama ndugu na mambo hayo yalienda hivyo mpaka siku moja  tulipoenda kupiga katika ukumbi wa Jeshi Morogoro mjini, ambapo watu walijaa sana kwenye dansi letu na tukapata shilingi 70,000/- hivi wakati huo kiingilio kilikuwa shilingi 50/-. Kiongozi akapagawa, akahama kutoka kwenye guest house tuliokuwa tumefikia na kuhamia hotelini ili kulinda fedha. Tuliporudi Dar sheria zikabadilika, akaitisha kikao na kutoa amri kuwa lazima aamkiwe shikamoo, na kila mtu, kwa kuwa yeye ndie kiongozi, na kuanzia hapo ikawa ukitaka kuongea nae lazima umtaarifu katibu wa bendi kwanza nae ndie anamtaarifu kiongozi wa bendi shida yako, inaweza ikaonekana kama mchezo wa kuigiza lakini hadithi hii ni kweli kabisa. tatizo kubwa la kiongozi huyu ni ushirikina, hakuwa anaamini kuna kitu kinaweza kufanyika bila tunguli. Hata tulipokuwa tumerekodi nyimbo RTD, siku zinapigwa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha misakato, alikuwa na katibu wake wanafukiza madawa kwenye redio iliyokuwa ikitangaza na kupiga nyimbo hizo!!!!!Siku ya kuacha bendi hii ilikuja baada ya bendi kwenda katika ziara Tanga na nikapata malaria kali siku ya kurudi. Kulikuweko na treni ya kutoka Tanga kuja Dar, viongozi walikuwa second class, makapuku tuko third class, ambayo kwa wakati huo ilikuwa hata sehemu ya kukaa ni tabu. Jitihada zote za wenzangu kuomba nisafiri na viongozi second class kwa vile naumwa zilielekea kugonga ukuta mpaka pale walipoanzisha fujo kubwa kwenye treni nikahamishiwa chumba cha ma Vie, niliposhuka salama Dar es Salaam nikaapa na bendi basi.....(itaendelea

Comments

Anonymous said…
Duh mheshimiwa balzi kweli umeyaona mengi. Na kue sagha rhumba vipi? Hebu tupe darasa maana that is my favorite band.