![]() |
Vanessa |
Sauti ya Vanessa Mdee ni mpya katika anga la muziki
Tanzania, kwangu mimi ni ushahidi mwingine kuwa kipaji huwa kinatembea katika
familia. Kwa kweli kilichonifanya nitake kusikiliza muziki wa huyu binti ni jina hili la Mdee. Mwaka 1972
nilijiunga na Chuo cha Ualimu
Kleruu Iringa, pale chuoni kulikuwa na magitaa mapya kabisa, hiyo
ilisababisha wote tuliokuwa wapiga magitaa kujenga urafiki na kukusanyika kila jioni kwenye kachumba kadogo na
kufanya mazoezi, kwa kuwa chuo kilikuwa tayari kina mwaka mmoja tulikuta tayari
wananchuo waliotangulia walikuwa wameanzisha bendi, na hapo ndipo nikamuona kwa
mara ya kwanza mtengeneza filamu mashuhuri kutoka Tanga Kassim El Siagi akiwa
anapiga gitaa la solo. Kati ya wanachuo tulioingia mwaka huo pia alikuweko
mmoja aliyeitwa Yusuph Mdee. Tulipatana mara moja baada ya kujiona wote
tunapenda muziki aina moja, haraka tukafanya mpango mpaka kuweza kuishi katika chumba kimoja na magitaa yetu, tulipenda kupiga na kuimba muziki uliokuwa maarufu
wakati huo, muziki wa soul, uliokuwa ukitamba wakati huo na wanamuziki kama
Otis Redding, James Brown, Percy Sledge, Clarence Carter na wengine wengi. Na
pia tulipenda muziki wa bendi wa bendi za Kitanzania zilizokuwa zikipiga muziki
wenye uhusiano na huo, kama Afro70, Safari Trippers, Sparks, Commets na
kadhalika. Yusuph alikuwa wakati huo ametoka Dar es salaam ambapo aliwa mwanamuziki
mzuri wa bendi maarufu ya Upanga iliyokuwa ikiitwa the Groove Makers, ambayo
ilikuwa na wanamuziki maarufu
ambao kwa sasa wana nyadhifa nzito serikalini, hivyo sitawataja hapa, lakini sisi tukawa katika mpango
wa kujaribu kupiga muziki tulioupenda . Yusuph alikuwa muimbaji na mpigaji
mzuri wa gitaa, baadae alijikita zaidi katika uchoraji na hata kufikia kwenda
Italy kuendeleza fani yake hiyo, aliishi Arusha kwa muda mrefu akiwa graphic
artist na DJ maarufu wa wakati wake, urafiki wetu ulidumu mpaka alipofariki Oktober 1999. Kwa kuufahamu uhusiano wa Vanessa na Yusuph nayaona mambo mengi ya Yusuph katika Vanessa japo sidhani kama Vanesa anaona hivyo kutokana na tofauti kubwa ya umri kati ya Yusuph na Vanessa. Uhakika nilionao ni kuwa ikiwa Vanessa ataendelea na ubora alionao sasa ni wazi akiwa na menejment nzuri atafika mbali sana. Wish you all the best Vanessa
Comments