KWANINI MUZIKI WA TANZANIA UNAKWAMA KUINGIA SOKO LA KIMATAIFA?


Historia fupi:

Kabla ya ujio wa wakoloni, historia ya utamaduni katika nchi nyingi za Afrika inafanana sana. Maendeleo ya utamaduni yalianza kuwa tofauti kutokana na wakoloni waliochukua nchi tofauti. Nchi zilizokuja kutawaliwa na Waingereza zilikuwa na safari tofauti kiutamaduni na nchi zilizotawaliwa na Wafaransa. Waingereza walijitahidi kufuta utamaduni wa nchi walizozitawala na kuingiza utamaduni wa Kiingereza. Mifumo ya elimu, na utawala ilisisitiza zaidi katika kuonyesha ubora wa utamaduni wa Kiingereza, na ilikuwa ni ufahari kwa wasomi na watu ambao wanaonekana wa kisasa kuonyesha dharau kwa utamaduni wa asili wa kwao, na hili si siri linaendelea mpaka siku hii ya leo nchini kwetu.
Baada ya kupata Uhuru, tatizo hili lilikuwa wazi kiasi cha Mwalimu Julius Nyerere katika hotuba ya uzinduzi wa Jamuhuri ya Tanganyika tarehe 09.12.1962, pamoja na masuala mengine, aliongelea kuhusu historia ya utamaduni wa Tanganyika. Naye alitamka kwamba nchi isiyokuwa na utamaduni wake haina tofauti na mkusanyiko wa watu ambao hawana roho iwawezeshayo kuwa taifa. Alivilaani vitendo vya wakoloni vya au kuwafanya Waafrika waamini kwamba hawana utamaduni wao wenyewe; ama kuufanya utamaduni wa Kiafrika uonekane kitu cha ovyo. Kutokana na hili, wengi wa waliokuwa wamesoma na kupata elimu ya Kizungu waliojiona kuwa ni “wastaarabu” walijifunza kuwaiga Wazungu kiasi kwamba kuwa Mwafrika msomi kulimaanisha kuwa Mzungu Mweusi. Suala la muziki, kama nyanja muhimu ya utamaduni katika historia ya Tanzania, limekuwa ainisho muhimu la migogoro ya kitamaduni, na Mwalimu Nyerere katika hotuba hii alizungumzia juu ya muziki. Kwa maelezo yake, waliokubuhu katika elimu ya kikoloni walifunzwa kuimba nyimbo za Kizungu, lakini siyo za Wahehe au Wanyamwezi. Walifunzwa kucheza
“rumba”, “cha cha”, “rock ‘n’roll”, “twist, “waltz” na “Foxtrot”. Lakini wengi walikuwa hawajawahi kucheza au hawakujua chochote kuhusu “Gombe Sugu”,
“Mangala”, “Nyang’umumi,” “Kiduo”, “Lele Mama”, au “Mganda.” Wengi wa waliosoma wakati wa ukoloni walijua kupiga gitaa au piano, lakini walikuwa hawajui kupiga ngoma. Haya yalitamkwa mwaka 1962, wakati ambapo kulikuwa hakuna mitandao ya kimawasiliano, video wala televisheni, kama ilivyo leo hii!
Baada ya kipindi hicho kulikuweko na jitihada kubwa za serikali na Chama tawala kuwafanya wananchi wajitambue kupitia utamaduni wao. Mambo mengi yalifanyika kutimiza azma hiyo, wananchi walihamasishwa kuanzisha vikundi vya sanaa katika sehemu mbalimbali, vijijini, sehemu za kazi mashuleni na kadhalika. Mashindano na matamasha mbalimbali yalihamasishwa na vikundi vilipewa nafasi katika hafla mbalimbali  za kuanzia vijijini mpaka kitaifa. Vikundi vya sanaa vya kitaifa  vikubwa pia vilianzishwa , ambavyo matunda yake yanaendelea kuliwa mpaka leo, kwa wasanii kutoka vikundi hivi wamekuwa waalimu wa vikundi vingi sana maarufu hapa Tanzania, na wengine kuendelea kuwa viongozi wa shughuli mbalimbali za sanaa nchini. Muziki ni sehemu ya utamaduni, kwa hiyo ulipitia ngazi zote nilizozitaja hapa juu. Kutokana na hali hiyo, vikundi vya muziki vilikuweko kuanzia ngazi za mitaa na vijiji. Shule zilikuwa na  vikundi vya muziki wa bendi, kwaya, taarab na muziki asili. Lakini licha ya mipango yote hiyo kulikuwa hakuna mpango maalumu wa kusambaza sanaa ya nchi hii nje ya mipaka, kubwa ni kwa sababu nia ya mipango yote ilikuwa ni kuhamasisha wananchi kujitambua.
Wanamuziki walikuwa wakirekodiwa muziki wao katika studio za Radio Tanzania. Na kazi hizi zilirekodiwa kwa kuelewa wazi kuwa zitakuwa kwa ajili ya matumizi ya radio tu na kwa matumizi ya Watanzania tu, hivyo kulikuweko hata kamati maalumu ambazo zilikuwa zikifuatilia maadili ya tungo hizo ili zikidhi hadhi ya Watanzania.  Vikundi ambavyo vilikuwa vikitaka kurekodi nyimbo zao katika santuri vililazimika kuvuka mpaka wa nchi na kwenda kurekodi nchini Kenya ambako kulikuwa na kampuni zenye uwezo wa kurekodi na kuchapisha santuri. Baadhi ya kampuni hizi zilikuwa ni sehemu ya kampuni kubwa za kimataifa za usambazaji wa kazi za muziki na hivyo kuweza kusambaza kazi hata nje ya Afrika mashariki, hili lilifanya baadhi ya wanamuziki wa Tanzania kuanza kufahamika hata Afrika Magharibi. Wimbo Tufurahi Weekend wa Bendi ya Afro70 uliweza kufika katika top ten nchini Nigeria muda mfupi baada ya kutolewa 1972.   Kutoka na matatizo ya kuvunjika kwa Shirikisho la Afrika Mashariki mpaka wa Tanzania na Kenya ulifungwa mwaka 1977 na hivyo kufunga njia pekee ya wanamuziki wa Tanzania kuweza kutoa santuri ambazo ndizo zilikuwa njia pekee kwa wakti huo wa kuwezesha muziki wan chi hii kuvuka mipaka ya nchi hii. Serikali ya Tanzania iaanzisha Tanzania Film Company ilikuweza kuwezesha wanamuziki wan chi hii nao weweze kutoa santuri. Studio zilianzia Mtaa wa Nkhruma na hatimae kuhamia Mikocheni eneo la Cine Club, kwa sasa sehemu hiyo ni sehemu ya bar na mgahawa maarufu. Serikali pia ilijaribu kuanzisha kiwanda cha santuri ambapo majengo ya kiwanda hicho ndipo kilipo Chuo Kikuu cha Uandishi wa Habari!!! Bahati mbaya malengo haya hayakutimia, na teknolojia mpya ya kanda za kaseti ikaingia mwishoni mwa miaka ya 70. Hapo ndipo biashara haramu ya kuuza kazi za muziki ikaanza rasmi.

Biashara huria
Kufunguliwa kwa biashara huria kulikuja lakini kulikuja katika hali ambayo biashara ya muziki Tanzania ilikuwa chini ya maharamia kutokana na kutokuweko na sheria nzuri za Hakimiliki. Kama ilivyo katika jamii yoyote isiyo na sheria ya Hakimiliki biashara hii haramu huwa ya siri sana na isiyo na mpangilio rasmi, hivyo basi taratibu ambazo hutakiwa ziwepo katika nchi yenye mpangilio safi wa Music Industry, hazikutengenezwa na mpaka tunavyoongea leo hakuna taratibu wala mpango wa kuwa na taratibu hizo. Wafanya biashara hawa lengo lao kuu ilikuwa kupata faida tu na si kuendeleza muziki, hivyo hawajawahi kuwa na nia ya kuuza muziki nje ya nchi. Wafanya biashara hawa wamekuwa wakisisitiza muziki ambao wanaona unauzika hapa nchini. Wakijali maneno yaliyomo katika muziki na aina ya muziki walioona unauzika nchini, na kamwe hawakutoa nafasi kwa kazi ambazo pengine zingeuza nje ya nchi.

Vyombo vya habari
Hakuna ubishi kuwa vyombo vya habari vimekuwa vingi sana nchini, lakini pia hakuna ubishi kuwa mchango wake katika kusaidia kukuza soko la muziki nje ya nchi hii umekuwa mdogo sana. Pamoja na matatizo makubwa ya hakimiliki, lakini kumekuweko na tatizo la muda mrefu la wafanyakazi wa vyombo vya habari kujihusiha katika kazi za wasanii binafsi na kutumia nafasi zao kuendeleza au kuangusha wanamuziki. Tumeona watangazaji wengi wakiingia katika kuchukua nafasi za umeneja wa wanamuziki, na hivyo kujikuta wakifanya kazi zao huku wakiwa na ‘personal interests’. Kumekuweko na kampuni za ‘kuendeleza wanamuziki’ ambazo zimekuwa na uhusiano wa karibu sana na vyombo vya habari, hivyo kuwa ni mafanikio kwa wanamuziki wengine na kikwazo kwa wanamuziki wengine. Lakini pia wote hawa wamekuwa na nia tu ya kuuza kazi hizo nchini bila kuwa na lengo wala nia ya kuuza nje ya mipaka ya nchi hii. Rushwa katika vyombo vya habari pia imekuwa ni tatizo la miaka mingi. Rushwa imesababisha  kazi ambazo hazina ubora wowote kupigiwa debe na vyombo vya habari kuwa ndizo bpra, nah ii kufanya hata vijana wenye nia na kipaji cha fani husika kuanza kuiga  na kuendeleza sanaa ambazo hazina ubora uliosifiwa. Pia kusababisha kuangusha wasanii wenye uwezo mkubwa ambao hawana au hawataki kutoa rushwa, popote penye rushwa kamwe hakuna haki. Mara chache sana ukasikia wimbo wa kuweza kuingia katika soko la kimataifa ukipigwa katika redio zetu ambazo nazo zote zimekuwa na utamaduni wa kupenda aina moja tu ya utangazaji, jambo ambalo linazuia maendeleo ya kweli ya sanaa.

Vision ya serikali
Kwa msanii wa kawaida vison ya serikali kuhusu biashara ya muziki kwa ujumla, haieleweki kama ipo. Taratibu za serikali zinaonyesha wazi kuwa nia ya kuu ya serikali ni kukusanya mapato kutoka kwa wasanii na ndio kazi yao inapoishia. Hiyo ndio kazi inayoonekana ya Maafisa Utamaduni kote nchini, ugomvi mkuu ni kuhusu vibali na michango mbalimbali. Sera ya muziki ingekuwa chombo muhimu kwa serikali kupanga taratibu zake kuhusu maendeleo ya muziki. Hapa moja kubwa ni elimu ya muziki ambayo pamoja na kuwa syllabus yake ipo, utekelezaji hakuna. Ni wazi lazima serikali ichukue nafasi yake katika hili.

Wanamuziki
Ni wanamuziki na vikundi vichache sana nchini ambavyo vinania ya kuuza muziki wake nje ya mipaka, mara nyingine unajiuliza kama kweli wanataka kuuza kwa mtu yoyote. Na hili ni tatizo kubwa kuliko yote. Wasanii wengi hujitokeza na kutangaza kuwa wanataka kuingia katika soko la kimataifa lakini matayarisho ya kazi hayaenda na nia ya kazi yenyewe. Wanamuziki wenyewe lazima wafanye mabadiliko makubwa katika taratibu zao, kuanzia kiutawala, kiusanii na kibiashara.

Comments