Nilibahatika
kuongoza semina ya wasanii mbalimbali kutoka wilaya ya Ilala, ulikuwa ni
mkusanyiko wa wasanii wakiwemo, wasanii wa filamu, ngoma,
muziki wa dansi, wachoraji wachongaji na kadhalika. Hii ni moja ya semina nyingi ambazo zimetayarishwa
na Chama cha Sanaa za Maonesho Tanzania(CHASAMATA). Katika semina hii mada
ilikuwa Athari za rushwa katika tasnia ya Sanaa. Nilianza kwa kueleza uelewa
wangu katika swala hili, ambapo pamoja na mengine nilielezea historia ya rushwa niliyokuwa naifahamu katika tasnia hii ambayo kwa
kweli imeanza miaka mingi sana. Baadhi ya mambo yaliyoleta rushwa katika
historia ya sanaa, ni mlolongo wa vibali kabla ya kila onyesho. Wakati wa enzi
ya chama kimoja, ilikuwa ni makosa kufanya onyesho bila kibali kutoka kwa afisa
utamaduni, hata kikundi kikitaka kutoka nje ya mkoa kilihitaji kuomba kibali cha kutoka
nje ya mkoa kutoka kwa afisa utamaduni mkoa ambaye alitoa kibali hicho ambacho kiliwasilishwa kwa afisa utamaduni wa mkoa unaokwenda ambae nae alitoa kibali
cha kukuruhusu kuingia mkoa wake na kuwaachia maafisa utamaduni wilaya watoe
vibali vya kuruhusu kufanya kazi kwenye wilaya zao, huu ulikuwa uwanja mzuri
kwa kuombwa rushwa ili uweze kuruhusiwa kufanya kazi zako. Sehemu nyingine iliyokuwa na
rushwa ni redio, ambayo hapo awali ilikuwa moja tu RTD, ambayo pia ilikuwa na studio pekee ya kurekodi muziki kwa muda mrefu. Rushwa ilianza pale
ambapo ililazimika kupeleka mashahiri ya tungo za muziki kabla haujarekodiwa,
kamati iliyokuwepo wakati huo, iliweza kukataa au kukubali wimbo urekodiwe
kwenye studio zake baada ya kusoma mashahiri hayo,bila kulazimika kutoa maelezo kuhusu uamuzi huo, hivyo bendi nyingi zilidaiwa kitu kidogo
ili kuhakikisha nyimbo ambazo zimefika kwenye kamati hiyo zote zinapita
zilivyo, ngazi nyingine ya rushwa ilikuwa inakuja katika kuwapa motisha
watangazaji husika kupiga nyimbo katika vipindi vyao, aina ya rushwa ambayo iko
mpaka leo. Watangazaji wamedaiwa kuomba fedha, vocha za simu, rushwa ya ngono, na hata wengine kutaka vikundi kutoka mikoani kuwaletea mchele, mbuzi nakadhalika.
Pia
imedhihirika kuwa bado kuna Maafisa Utamaduni wanapenda rushwa kiasi cha
kuwezesha vikundi kushinda katika mashindano mbalimbali kwa makubaliano ya
kugawana zawadi. Ilitolewa mifano ambapo Afisa mmoja alidai khanga 5 kati ya 20
zilizotolewa kama zawadi kwa kikundi alichokisaidia kushinda na pia alidai
kupewa wheelbarrow ambayo kikundi kilishinda katika mashindano mengine.
Katika
kuchangia mada, jambo ambalo lilikuwa wazi ni kuwa rushwa ya ngono kwa wasanii
wa kike ni adha wanayoipata kila mara. Katika tasnia ya filamu na michezo ya
jukwaani, viongozi wa vikundi, waongozaji wa filamu, producers ndio waliotajwa
kuongoza katika kuomba rushwa ya aina hiyo, na wanawake wote huombwa rushwa hiyo bila
kujali umri, jambo ambalo lilimfanya mama moja mtu mzima atokwe na machozi pale
alipoombwa rushwa hiyo na mvulana ambae alimuona kama mwanawe. Vikundi
vidogovidogo vya mtaani vimekithiri kwa aina hii ya rushwa na hasa katika
maeneo yanajulikana kama kambi au location za filamu, na mara nyingi kwa hadithi za uongo kuwa wataweza kupata kazi katika filamu kubwa. Kwa upande wa wanamuziki
wa kike adha yao huanzia na producers, kisha watangazaji, na hata wafadhili wa
kazi zao kiasi cha mtangazaji maarufu kudai aliamua kuachana na fani ya muziki
kwa ajili ya adha hiyo. Wiki ijayo wasanii wa Kinondoni watakuwa kwenye semina
ya aina hiyo hatimae Temeke, na ndipo yatatolewa mapendekezo ya jumla ya hatua za
kuchukua kuondoa adha hii.
Comments